Mwaka 2004 aliyekuwa Rais wa Tanzania , Benjamin Mkapa alimleta nchini mtaalam wa uchumi, Prof. Hernando de Soto Polar (75 – sasa) kuzungumza jinsi ya kuwaondoa Watanzania katika lindi la umaskini. Nilipata fursa ya kuwapo kwenye mkutano huo uliofanyika katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam. Prof. de Soto alizungumza kwa angalau saa 3 hivi, ukichanganya na maswali, ila sijawahi kusahau mhadhara wake.

Sitanii, Prof. de Soto siku hiyo alizungumzia uwezeshaji wa wananchi na umiliki wa ardhi. Alisema wananchi walio wengi si maskini. Alisisitiza kuwa Tanzania inakabiliwa na umaskini wa fikra. Alisema: “Kila Mtanzania au karibu kila familia ya Kitanzania inamiliki nyumba au kipande cha ardhi, lakini bado hawa wanahesabiwa katika kundi la watu maskini… si sahihi.”

Profesa huyu alifafanua kuwa umaskini unaowakabili wananchi unatokana na kumiliki “mitaji iliyokufa.” Kwa maana kuwa nyumba, ardhi au mali kadhaa wanazozimiliki hazitambuliki popote na hilo ndilo chimbuko la umaskini kwa walio wengi. Prof. de Soto alisisitiza kuwa ni vyema Serikali ikachukua juhudi za makusudi kupima ardhi wanazomiliki Watanzania ikawapa hati.

Yeye alikuwa akitumia maneno “formalization of the informal sector.” Akimaanisha kurasmisha mali zisizo rasmi. Duniani kote uraia/utajiri wa watu unahusishwa na uhusiano wa vinasaba vya ardhi (jus soli). Benki karibu zote hapa nchini zinashindwa kukopesha Watanzania kwa kuwa hawana hati miliki. Hii maana yake ni kuwa benki inajiuliza ikiwa Serikali yako haijakutambua na kukumilikisha ardhi, yenyewe itakutambuaje kukupa mkopo?

Sitanii, suala hili la uaminifu/dhamana kuthibitisha kuwa kweli wewe ni mkaazi halali wa eneo fulani na unaweza kuaaminiwa ukakopeshwa kwa mawazo kuwa utarejesha ulichokopa limekuwa chimbuko la umaskini kwa Watanzania walio wengi. Hata pale Benki zinapojitoa muhanga kukopesha, zinakopesha kwa riba kubwa maana kiwango cha wakopaji ‘kutokomea kusikojulikana’ ni kikubwa.

Kichwa cha makala hii, kinasema “Hakika Lukuvi anawezesha Watanzania”. Nimemuona Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi anavyozunguka nchi nzima kutatua migogoro ya ardhi. Nimeshuhudia jinsi Lukuvi alivyolipa kipaumbele suala la kuhakikisha wananchi wanapimiwa maeneo yao na hatimaye kupewa hati za kumiliki ardhi.

Ameagiza halmashauri zote nchini kupima viwanja na kuhakikisha watu wanamilikishwa ardhi. Binafsi naamini anachofanya Waziri Lukuvi kinaendana sawia na dira ya Rais John Magufuli ya kujenga Tanzania ya Viwanda. Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa hatua ya kumiliki viwanda inaanza na hatua ya kwanza, ambayo ni hatua ya kumiliki ardhi.

Asikudanganye mtu, hakuna mtu yeyote anayeweza kuamka asubuhi, akaokota Sh bilioni 50 akaanzisha kiwanda. Sisi kwetu Bukoba kuna msemo kuwa “Kalitunga agila obwemelo.” Msemo huu unamaanisha kuwa kutajirika ni lazima uwe na msingi. Katika biashara msingi ni ardhi iliyopimwa. Kadri Watanzania wengi watakavyokuwa na hati za kumiliki ardhi, ndivyo watakavyoweza kumiliki biashara kubwa.

Lakini pia, sisi Watanzania hata baada ya kuzifahamu hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika kufikia hatua ya kukopesheka, tunapaswa kuanza biashara kidogo kidogo. Si vyema sana ukachukua fedha za mkopo ndipo ukaanza kubuni biashara ya kufanya. Mkopo wenye ufanisi unauchukua kuendeleza biashara unaoifahamu.

Kwa mfano, ukiwa katika biashara ya kuranda mbao, unaweza kuchukua mkopo kununua mashine bora ya kurada inayotoka Italia, badala ya kuendelea na mashine uliyoanzia maisha inayowezekana isiwe na uwezo mkubwa ulioyochongewa na SIDO. Mbele ya safari, unaweza kujifunza teknolojia ya kutengeneza mashine zenyewe, hivyo ukakopa kununua mitambo ya kutengeneza mashine.

Sitanii, ni kwa utaratibu huo utakuza biashara. Lakini ukiona jirani ana daladala, kila siku unaona linatoka na kuingia ukawa unamhesabia faida, nawe ukakurupuka ukachukua mkopo na kununua daladala, unaweza kufika wakati ukakufuru. Utakuta mara dereva anakwambia trafiki kampiga  ‘bao’, mara unaambiwa imekata belt ya wiper, na kwa kuwa utakuwa hujui kitu utatoa hela hadi utakoma.

Naomba kuhitimisha kwa kusema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli, uamuzi iliouchukua wa kumtaka Waziri Lukuvi kupima viwanja vyote nchini kama alivyoahidi ni sahihi na ni nguzo ya kuelekea uchumi wa viwanda. Rai yangu ni wananchi kujitokeza kwa wingi kupima viwanja vyao na kwa kufanya hivyo watakuwa wamejijengea mtaji wa kudumu kwa nia ya kuondoa umaskini. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri