Tabia ya Waingereza kuzijua na kuzitetea haki zao, inanipa faraja kubwa sana wana-Jamhuri wenzangu. Watu wakubwa wamejikuta wanaanguka kwa mambo yanayotokana na kushindwa kuheshimu wadogo. Mfano wake ni Mnadhimu Mkuu wa Serikali, Andrew Mitchell, anayetota matatani kwa kuwaita polisi wanaoshika lindo kwenye Ofisi za Waziri Mkuu pale Downing Street kuwa ni “kajamba nani” tu.

Mitchell alifka hapo nyakati za mchana akiwa kwenye baiskeli yake, akataka akatize moja kwa moja kwenye lango bila kuulizwa kitu, askari akamkomalia, ndipo akafoka kwamba yeye ni mkubwa na wao ni walalahoi tu.

 

Niliposikia habari hizo, kumbukumbu ilirejea Dar es Salaam, Mtaa wa Samora mwaka mmoja au miwili iliyopita, ambako waziri mmoja kijana alikuwa anatumia ATM na kung’ang’ania huko. Askari aliyekuwa akilinda hapo aliingia mle ndani na kumwambia waziri atoke nje kwa sababu wateja wengine wanasubiri na wanahangaika juani. Waziri anadaiwa kutoa matusi, akalalamika kwa mabosi, na baadaye askari alipoteza kibarua chake!

 

Tofauti na hii ya London ni kwamba Waziri Mitchell ndiye aliyepo kikaangoni, anatapia kulinda kiti chake, na watu wa kawaida na hata polisi wa ngazi zote wamemkalia kooni. Mitchell ni mtu mkubwa kwenye serikali na pia chama cha Matori (Conservative) kinachoongoza hapa na kile cha Liberal Democratic.


Mitchell licha ya kutetewa na Waziri Mkuu David Cameron kwamba ameshaomba radhi na ni mtu wake muhimu kikazi, mambo yanamwendea kombo. Imebainika hata madai yake kwamba alitoa kauli inayofanana na hiyo lakini hakuwaita hivyo polisi baada ya kazi nzito za siku hiyo, kumbe alikuwa na mlo wa mchana wa gharama kubwa kwenye mgahawa matata wa London.

 

Alipoingia na baiskeli yake pale, kumbe tumboni alishatia kitu cha bei kali, maana mgahawani hapo wanapopaita Cinnamon Club, Westminster, hupati chakula bila pauni 50 (Sh 125,000 au zaidi)!Baada ya sakata hilo kuibuka, Cameron alisema wazi kwamba waziri wake huyu amekwenda kinyume, na hadi leo askari, akiwamo mkuu wa polisi na mkuu wa shirikisho la askari polisi, wamemkalia vibaya.


Wanasema ana bahati kwamba hakukamatwa siku hiyo na kutupwa lupango, maana alikosa adabu na kuvunja sheria kwa matamshi yake. Kama inavyokuwa ikitokea Tanzania, kashfa ya aina hiyo inapoibuka wafanyakazi wa Idara ya Mambo ya Nje alikokuwa akifanya kazi kabla, waliposikia yamemkuta walilipuka na vigelegele.


Hii ni kwa sababu wanasema amekuwa mtu mtata wizarani hapo, akipenda aitwe Secretary of State na kila mtu, anatumia kikombe kilichoandikwa hivyo na anataka wafanyakazi wote wanaume wavae makoti na tai. Hata mazingira ya kazi yanapokataza, alikuwa anasisitiza wavae hivyo, ikishindikana asione mtu hana tai kwenye mikutano anayoongoza.


Lakini unajua nini? Amekutwa zaidi ya mara moja akiwa kwenye mikutano anayoongoza bila hata viatu, akipekua huku kamba anazofungia suruali wakati akiendesha baiskeli zikiwa bado miguuni mwake! Serikali, kama kawaida yake, ilimtetea na msemaji wa idara hiyo akadai hakuna mtu aliyewahi kutoa malalamiko dhidi ya Mitchell, kwa hiyo wasishikie bango jambo lisilo lao.


Hata hivyo, wafanyakazi wizarani hapo wanadaiwa walikuwa wakifaidika na kuwepo kwa Mitchell, kwa sababu ya mtiririko wa posho kwa kazi mbalimbali hapo, bali wanasema ni mtu mgumu kufanya naye kazi. Inadaiwa wapo waliofanya visherehe alipopangiwa kazi mpya ya unadhimu mkuu wa serikali.


Je, tuna nguvu za kusimamia haki zetu kama Waingereza? Tunawaona mawaziri kama miungu watu kiasi cha kuwadharau polisi wetu? Si rahisi kwa askari wa kawaida wa kwetu kutoa malalamiko dhidi ya waziri, maana wanaweza kufukuzwa kazi.

 

Si ajabu hata ma-OCD, RCO, RPC na si ajabu hata IGP hawana ubavu wa kuwasema na kuwachukulia hatua mbele ya mawaziri wanaokosea; wanasema tu ndiyo mzee. Tujifunze na tutekeleze.


[email protected]


 

By Jamhuri