*Biashara ya magendo yafanywa nje nje

*Maofisa wa TRA, polisi wahusishwa

*RPC, Meneja TRA wakiri hali mbaya

Biashara ya magendo imeshamiri katika mji wa Sirari mpakani mwa Tanzania na Kenya, huku vyombo vya dola vikionekana ama kushindwa au kushirikiana na madalali maarufu kwa jina la “mabroka”. Vitendo hivyo vinaendelea kuikosesha Serikali mapato kutokana na bidhaa nyingi kuingizwa Tanzania na hata kupelekwa Kenya kupitia “njia za panya” bila kulipiwa kodi na ushuru.

Baadhi ya bidhaa zinazohusishwa katika magendo hayo ni mahindi, mifugo kama ng’ombe, samaki, dagaa, saruji, mabati, machungwa na nyanya. Barabara maalumu imetengenezwa ili kuwezesha malori yenye magendo kupita kirahisi.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa madalali wanashinda na kukesha wakifanya kazi ya kuwasaka na kuwarubuni wafanyabiashara wanaohitaji kuingiza bidhaa au kusafirisha kwenda Kenya.

 

Wanawashawishi wafanyabiashara hao kukwepa kutumia taratibu na njia halali kusafirisha bidhaa hizo.Chanzo cha habari kimesema kiwango cha fedha ambacho wafanyabiashara huwalipa madalali, ni kikubwa ikilinganishwa na malipo halali.

 

“Kwa kutojua unakuta mfanyabiashara anawalipa mabroka shilingi laki saba baada ya kumshawishi kutumia njia za panya kusafirisha mali zake, lakini kama angetumia utaratibu na njia halali angelipa hata shilingi laki moja tu,” kimesema chanzo cha habari na kuendelea: “Hawa mabroka ni watu matapeli, wajanja wajanja fulani, hawana idara wala kampuni yoyote, wanarubuni wafanyabiashara kwamba wao ndiyo wenye uwezo wa kuwasaidia kuvusha bidhaa kwa gharama nafuu wakati si kweli.”

 

Madalali hao wanashirikiana na polisi na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuwezesha wafanyabiashara kusafirisha na kuingiza nchini bidhaa kwa magendo.

 

“Inashangaza kuona kwamba polisi wanaotumwa kwenda kudhibiti magendo katika njia za panya, ndiyo wanaokuwa wa kwanza kuvunja sheria kwa kubariki vitendo hivyo haramu, lakini kuna taarifa kwamba askari wanaofanya hivyo wanakula na wakubwa zao,” kimesema chanzo cha habari.

 

Bidhaa nyingi zinasafirishwa nyakati za usiku na alfajiri zikiwa ndani ya malori. Wakati mwingine polisi ndiyo wanaowaelekeza wafanyamagendo njia za kupita.

 

Baadhi ya madalali waliozungumza na JAMHURI kwa sharti la kutotajwa majina, wamesema hawaoni sababu ya kushutumiwa kwa vile wanatafuta riziki, na kwamba hawawalazimishi wafanyabiashara.

 

Meneja TRA azungumza

Meneja wa TRA Mkoa wa Mara, Joseph Karinga, amekiri kushamiri kwa magendo mpakani hapo, licha ya juhudi zinazofanywa na ofisi yake kukabiliana na hujuma hizo.

 

Amesema kukua kwa biashara ya magendo kunachangiwa na urefu wa mpaka wa Tanzania na Kenya, hali inayowawia vigumu kulipatia tatizo hilo ufumbuzi wa kudumu.

 

“Wakwepa kodi wapo siku zote, ndiyo sababu tunakuwa barabarani, ila wanasaidiwa na akina nani, hilo sijajua. Suala la ukwepaji kodi lipo siku zote na sisi tunapambana nalo kila siku,” amesema Karinga na kuongeza: “Mpaka wa Tanzania na Kenya ni mpana, kwa hiyo doria zinafanyika wakati wote, tatizo ukienda njia hii wanapita njia ile, vijana wangu wako kwenye doria wakati wote.”

 

Karinga amesema maofisa wa TRA wamekuwa wakiwasaka madalali hao wanaowashawishi wafanyabiashara kukwepa ushuru kutumia njia za panya bila mafanikio.

 

Kuhusu maofisa wa TRA wanaoshirikiana na madalali hao kwenye magendo, meneja huyo ameahidi kutumia kamati za maadili za Mamlaka hiyo kuchunguza na kuwachukulia hatua watakaothibitika.

 

“TRA kuna kamati za maadili kuanzia ngazi ya taifa, mkoa, wilaya hadi ngazi ya kituo, hata hapo Sirari pia kuna kamati ya maadili, tukiwagundua maofisa wetu wasio waadilifu tutawashughulikia mara moja, lakini ili tutende haki tunafanya uchunguzi wa kina, vijana wangu wanafanya kazi, wako barabarani kila siku, ila sasa mpaka ni mpana,” amesisitiza Karinga.

 

RPC naye azungumza

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, amesema hana taarifa za baadhi ya polisi wanaoshirikiana na wafanyabiashara kufanya magendo mpakani.

 

Hata hivyo, amekiri kwamba tatizo la magendo ni kubwa katika eneo hilo; na kwamba ofisi yake inaendelea kuongeza udhibiti.

 

“Silifahamu tatizo hilo na hatuwezi kuruhusu vitendo hivyo. Magendo yapo sehemu mbalimbali katika barabara za mpakani ukianzia Shirati hadi Masanga, kila mtu anajua hilo, si RPC tu, lakini tukiwagundua askari wasio waaminifu tutachukua hatua za kuwadhibiti,” amesema Kamanda Kamugisha.

 

1549 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!