url-1Mwaka 2006 nilipata fursa adhimu ya kuzuru nchini Cuba. Hii ni miongoni mwa safari nitakazokumbuka daima.

Nimekuwa miongoni mwa wafuasi wa siasa za Fidel Castro na wana mapinduzi aina ya Che Guevara.

Tangu nikiwa shule ya msingi nilipenda mno kupata simulizi zilizowahusu makomredi hawa na wengine, akiwamo Mwenyekiti Mao wa China.

Nilipofika Cuba, ilikuwa fursa nzuri ya kuiona nchi niliyotamani kuizuru tangu nikingali mdogo. Bahati mbaya sikuweza kumwona Komredi Castro, kutokana na kuzorota kwa afya yake.

Niliandika makala nyingi nikieleza niliyoyaona nchini humo. Kwa ufupi, Cuba niliyoiona ni tofauti kabisa na ile inayotangazwa na Marekani na washirika wake. Ni nchi ambayo wananchi wake wanaishi kwa uhuru na kwa upendo mkubwa licha ya vikwazo vya kiuchumi walivyowekewa na Marekani kwa miongo mingi.

Cuba, chini ya Castro ndio nchi iliyofanikiwa, pengine kuliko nchi yoyote katika sayari hii, kwenye suala la afya kwa wananchi wake. Idadi ya madaktari nchini Cuba ni kubwa kuliko mahitaji! Ni nchi iliyowekeza zaidi kwenye utafiti, kiasi cha kuiwezesha kupata chanjo za aina fulani fulani za saratani na maradhi mengine yanayowasumbua walimwengu. Komredi Castro alivyougua, hakwenda kutibiwa ng’ambo! Haya ni mafanikio makubwa na uthibitisho wa kujitegemea kwa nchi hiyo kwenye nyanja karibu zote.

Cuba ndio nchi iliyofanikiwa kufuta ujinga kwa kiwango cha kuifanya UNESCO iitambue na iipe heshima ya kipekee. Kama Marekani, adui mkuu wa Cuba, anakiri mafanikio hayo na kuisifu, hapo msomaji unaweza kujua ni mafanikio makubwa kiasi gani. Elimu nchini Cuba ni bure kuanzia msingi hadi chuo kikuu.

Sote tunatambua namna Cuba ilivyo mahiri kwenye nyanja ya michezo. Mabondia wa nchi hiyo wamekuwa tishio katika mashindano mbalimbali.

Urafiki wa Tanzania na Cuba ni wa kihistoria. Bahati mbaya kizazi cha sasa cha Watanzania hakipewi fursa ya kuelezwa ukweli huu. Kama kuna dhambi mbaya inayopandikizwa kwenye ubongo wa vijana wetu, ni hii ya kuwanyima historia. Cuba si tu kwamba ni rafiki wa kweli wa Tanzania, bali ni kinara wa ukombozi katika Afrika na ulimwengu wa wanyonge.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Komredi Castro walikuwa, na bila shaka wanaendelea kuwa marafiki wakubwa hata huko waliko sasa.

Nchini Tanzania, Cuba imefanya kazi kubwa ya kutusaidia kwenye mapambano dhidi ya maadui ujinga, maradhi na umaskini.

Shule za sekondari za Kibiti, Ruvu na nyingine kadhaa-Bara na Visiwani- ni uthibitisho halisi wa urafiki wa Tanzania na Cuba.

Cuba imewapata mafunzo Watanzania wengi kwenye sekta za michezo, afya, kilimo, ulinzi na usalama; na kadhalika. Kuna Watanzania maelfu kwa maelfu waliopata na wanaoendelea kupata mafunzo ya ngazi na fani mbalimbali nchini Cuba.

Madaktari wa Cuba wamekuwapo nchini mwetu wakitoa huduma za tiba katika hospitali mbalimbali. Wametupatia makocha wa ngumi, riadha na michezo mingine mingi. Ni ukweli ulio wazi kuwa wakati Cuba ikiwa na mkono wake kwenye sekta ya michezo, ndipo Tanzania ilipovuma kweli kweli kwenye anga za kimataifa.

Cuba imekuwa rafiki yetu mkuu kwenye masuala ya ulinzi. Kuna mamia kwa mamia ya Watanzania waliopelekwa Cuba kupata mafunzo mbalimbali ya kijeshi. Wapo wataalamu wengi wa nchi hiyo wanafika kuwapa mafunzo ya kisasa wapiganaji na makamanda wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kijijini Butiama, Castro alianzisha kituo cha mbegu bora za ng’ombe. Hadi leo eneo kilipokuwa kituo hicho linaitwa ‘Cuba’. Kuna taarifa kuwa kwa sasa nchi hiyo inasaidia ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere, katika eneo hilo.

Cuba wamekuwa marafiki zetu na ndio maana wakaamua kutusaidia ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza viuatilifu ili kukabiliana na mbuzi waenezao malaria. Kiwanda hicho kilichopo Kibaha mkoani Pwani, kinapigwa vita na wenye viwanda vya dawa za kutibu malaria kwa sababu wanajua ufanisi wake utakuwa pigo kwa soko la dawa zao!

Kwa wa Afrika, kazi iliyofanywa na Komredi Castro kwenye ukombozi wa bara hili, haina mfano. Akiwa bega kwa bega na Mwalimu Nyerere, Castro alitoa msaada wa hali na mali kufanikisha ukombozi wa mataifa mengi ya Kusini mwa Afrika. Ni ukweli ulio wazi kuwa kama si juhudi za Castro na Mwalimu, pengine hadi leo mataifa hayo yangekuwa chini ya utawala wa kimabavu wa wazungu walowezi na makaburu.

Mandela anasifiwa kwa sababu wazungu ndio walioamua kumkweza. Wamempa kwa kuwa hakutaka kulipa kisasi kwa wazungu. Ukweli ni kuwa nyuma ya Mandela wapo ‘waliomtengeneza’. Yawezekana wakawapo wengi, lakini miongoni mwao Komredi Castro na Mwalimu Nyerere, wako mbele kabisa.

Tunaweza kusema na kuandika mambo mengi mno ya Cuba na Castro kwa Tanzania na Afrika; itoshe tu kusema mwanamapinduzi huyu alikuwa rafiki wa kweli wa Tanzania na Afrika.

Pamoja na mengi mazuri aliyoyafanya kwa Tanzania na kwa Afrika, tukiri kuwa hatukumpa heshima stahiki kiongozi huyu shupavu. Msiba wa Castro tumeupokea na kuushiriki kama msiba wa ‘kibaka’! Serikali yetu haikuonesha kuguswa vilivyo na msiba huu. Hatukumtendea haki.

Fidel Castro alistahili kuenziwa walau kwa kupeperusha bendera yetu ya Taifa nusu mlingoti, hata kama ni kwa siku moja. Nayasema haya nikirejea namna Wacuba walivyoupokea na kuuomboleza msiba wa Mwalimu Nyerere! Wengi walilia kwa kumpoteza rafiki wa kweli.

Kama tulishindwa japo kushusha bendera (jambo ambalo halina gharama yoyote), walau basi tungepata uwakilishi mkubwa kwenye mazishi yake.

Rais John Magufuli, angeweza kuwa bize na masuala ya nchi, lakini akafanya kama anavyofanya mara nyingi – akamtuma Makamu wake au Waziri Mkuu. Laa, hilo kama lisingewezekana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa angeifanya kazi hiyo. Na kama wote hao wangekuwa ‘bize’, basi angetafutwa mzee mmoja mstaafu-Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa, au Mzee wa karibuni, Jakaya Kikwete – akatuwakilisha kwenye msiba huo. Kufanya hivyo kungetusaidia kuendelea kudumisha urafiki wetu wa kihistoria na ndugu zetu Wacuba.

Uamuzi wetu wa kuupitisha msiba huu kimya kimya kana kwamba aliyefariki ni ‘mtu wa kawaida tu’, unaweza kuwa na athari kwenye ushirikiano wetu na taifa hilo. Waswahili walisema akujuaye wakati wa dhiki ndiye rafiki wa kweli. Wacuba si kwamba hawana kumbukumbu. Wanayo orodha ya nani walifanya nini walipoondokewa na Baba wa Taifa lao. Hili wanaweza kuliweka kwenye rekodi na matokeo yake yakawa kuzorota kwa urafiki wetu.

Naamini hatujachelewa. Kuna mambo mengi, makubwa na mazuri yanayofanywa na Serikali yetu. Kuna miradi mingi inajengwa. Si vibaya katika hayo makubwa yanayoendelea, siku moja tukaamua kulikumbuka jina la Castro kwa kuliweka kwenye mradi mmoja unaolingana na heshima yake; kama sehemu ya kumuenzi na kutambua mchango wake kwa Watanzania, Waafrika na walimwengu wanyonge.

Bado tuna mambo mengi mazuri tunayoweza kujifunza kutoka Cuba kwa hiyo hatuna budi kuuendeleza urafiki wetu kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo. Bado naamini Komredi Fidel Castro hakutumtendea haki. Tusijitenge mno na marafiki zetu waliotufaa wakati wa dhiki. Waswahili walisema ‘usitukane mkunga na uzazi ungalipo’. Bado Wacuba tunawahitaji maana safari yetu ya maendeleo ndio kwanza imeanza. Pumzika kwa amani Komredi Castro. Umetimiza wajibu wako. Kama ilivyo kwa Mwalimu Nyerere, historia yako haitofutika milele.

2257 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!