Krismasi ni somo la mpango mkakati

Na Padri Dk. Faustin Kamugisha

Usikate kanzu (mbeleko) kabla mtoto hajazaliwa.  Ni msemo ambao unatuweka katika utamaduni wa kutopanga kabisa ya kesho. Matumizi ya kipindi cha Krismasi huacha mifuko ya pesa imesinyaa kwa baadhi ya watu kila mwaka. Lakini ukweli ni kuwa Krismasi ni somo la mpango mkakati. Krismasi haitokei kama dharura. Inajulikana kuwa kila tarehe 25/12 ni  Sherehe ya Kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo. Krismasi inatufundisha kuwa Mungu wetu ni Mungu wa mipango, hachezi bahati na sibu, hakurupuki.
Alipanga juu ya Krismasi kwa kutumia mtindo wa kupanga ya kesho kutokana na nyufa ulizonazo, kasoro na udhaifu uliopo. Baada ya wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva au Hawa kutenda kosa la kutomtii Mungu, Mungu alipanga kuziba ufa. Usipoziba ufa utajenga ukuta.
Mungu alipanga kuwakomboa wanadamu. Alipanga kumtuma Mkombozi, ndiyo maana miaka ilihesabiwa kwa kurudi nyuma. Maneno Kabla ya Kristo (K.K) kuzaliwa yanatumika.
“Wakati maalumu ulipotimia, Mungu alimtuma mwanae aliyezaliwa na mwanamke ili apate kuwakomboa waliokuwa chini ya sheria (Wagalatia 4: 5).” Mungu anatupa mfano wa kuwa na mipango ya muda mrefu kutokana na udhaifu uliopo. Udhaifu uliokuwepo ni dhambi ya asili.
Isaya alitabiri: “Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli (Isaya 7: 14).”
Katika maneno hayo Kanisa Katoliki linaona tangazo la fumbo juu ya uzazi wa Yesu Kristo. Utabiri huu ulitolewa mwaka 736-700 K.K. Kuna aliyesema: “Mungu kila mara ana kitu kwa ajili yako, ufunguo wa kila tatizo, mwanga kwa kila kivuli, faraja kwa kila huzuni na mpango kwa kila kesho.”
Ndugu msomaji kuwa na mpango wa kila kesho. Kuwa na mpango wa kila mwaka. Kuna kampuni yenye mpango wa miaka 100 kwa nini usiwe na mpango angalau wa miaka kumi?
“Usifanye mipango midogo, haina uchawi wa kusisimua damu,” alisema Daniel Burnham. Mpango wa ukombozi wa mwanadamu ni mpango mkubwa sana. Ulisisimua damu ya mitume wake. Mipango uliyo nayo je, inasisimua damu yako kuitekeleza?
Kanisa Katoliki linaamini kuwa Mungu ni mmoja – nafsi tatu. Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Mkakati ni chaguo zuri sana. Mungu Mwana alijifanya mtu. Ili kuelewa jambo hili, hadithi ifuatayo itasaidia:
Kuna Mkristo mmoja aliacha kwenda kanisani kusali na alikuwa haelewi ni namna gani Mungu Mwana anaweza kujifanya mtu. Siku ya Krismasi hakwenda kanisani kusali.
Mvua ilinyesha sana. Kuku wake walikuwa nje lakini walinyeshewa mvua. Alijiambia: “Ningekuwa na uwezo wa kuwa kama kuku nikaongea lugha yao wangenielewa. Ningewasaidia.” Tafakuri hiyo ilimfanya atafakari kwa nini Mungu alipata mwili akazaliwa na kukaa na sisi ili kutukomboa.
“Usipofikiri juu ya wakati ujao huwezi kuwa nao.” (Dwight D. Eisenhower). Panga utakavyoishi miaka ijayo. Panga kila mara. Shughulikia vipengele vyote katika mpango mkakati. Muweke Mungu katika mipango yako. Muombe akusaidie.
Somo la pili la Krismasi ni kuwa popote ngaa. Hata kama umezungukwa na wabezaji ngaa. Yesu alizaliwa horini. Alizungukwa na wanyama kama ng’ombe na punda. “Mtoto Yesu anapata joto kutoka kwa ngombe na punda.” Ng’ombe ni alama ya bidii katika kazi; kukubali kubezwa hata pale tunapofanya kazi njema, kunawakilishwa na huyo punda ambaye hufanya kazi lakini hakuna anayemjali (Mt. Gaspari del Bufalo).
Kuna methali ya Tanzania isemayo: “Asiyeweza naye hudharau.” Hata kama unadharauliwa na wasioweza, endelea kungaa. Tumweke Yesu katika Krismasi. Ni vizuri mtoto Yesu akaonekana kwenye kadi za Krismasi badala ya ndege. Kristo anayezaliwa ni mfalme wa amani. Tuitunze amani. Hata kama hautapata zawadi kuwa na amani si sherehe yako ya kuzaliwa.

Mwisho

By Jamhuri