Unapomfuga mbwa lazima atabweka tu, kwa sababu kubweka ni moja ya sehemu ya makuzi yake.

Mimi ni mbwa niliyefugwa na taifa hili, ni lazima nibweke, siasa si uadui, isipokuwa hoja. Siasa ni sehemu ya maisha ya binadamu. Mwanafalsafa Hegel anasema: “Binadamu ni mnyama wa kisiasa.”

Hizi siasa za kushambuliana kwa mapanga na risasi ni siasa zinazopandikiza chuki ya kudumu kwa kizazi cha sasa na kijacho. 

Ni hatari kwa taifa kuamini mawazo fulani na kupuuza mengine. Ni hatari kwa taifa kuwachukia wasema kweli, ni hatari zaidi kwa taifa kuwa na watu wanaojulikana na wasiojulikana. 

Kuna matukio ya Watanzania kutekwa, kuteswa na wengine kuuawa, nyumba tunayojenga ni moja, kwa nini tunagombea fito? 

Taswira ya kisiasa katika taifa letu sasa si salama, hilo liko wazi, sihitaji kusimulia. Vyama vya upinzani sasa vinapitishwa kwenye tanuri la moto. 

Wanahabari wengine wametoweka. Wengine wameamua kuisifia serikali tu. Naomba kusema jambo hili; ‘tumepoteza tunu ya kuvumiliana.’ 

Jambo hili si sifa njema kwa taifa letu linalosifika kuwa kisiwa cha amani. Kuna dhambi ya ubaguzi imeanza kutunyemelea. Mwalimu Julius Nyerere alipata kutoa onyo la ubaguzi akisema: “Dhambi ya ubaguzi haiishi hata siku moja.”

Mwalimu Nyerere alipenda sana mawazo ya kukosoana. Alifahamu kwamba kwa kila anayemkosoa kuna jambo la kujifunza kutoka kwake. 

Leo hii hali ya taifa letu ikoje? Mwenye macho haambiwi tazama, mwenye njaa hakumbushwi kula. Leo hii kuikosoa serikali yetu ni dhambi. Ni serikali gani duniani ambayo haikosolewi? 

Leo hii katika taifa letu kuna ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa kutoa maoni, siamini kama baadhi ya watu

ndio wana mawazo sahihi ya kuliongoza taifa hili. 

Ajabu ni kwamba katika taifa letu pale mtazamo wako unapokuwa wa tofauti na watu wengine, unabatizwa majina kama; ‘mhaini’, ‘mchochezi’ kwa kutaja machache. 

Na unapoonekana una msimamo thabiti wa kuipinga ama kuikosoa serikali yako wanatokea watu ‘wasiojulikana’ kukunyamazisha. Katika uhalisia wake lazima tujiulize, kwa nini wale watu wanaoonyesha msimamo wa kuipinga serikali maisha yao yanakuwa hatarini? 

Nje ya demokrasia urais hauko salama, nchi haiko salama wala mihimili yote mitatu ambayo ni Bunge, Mahakama na Serikali. Taifa lolote ambalo watu wake wanafumbwa midomo ni taifa bubu. 

Usalama na ustawi wa taifa ni pale watu wanapokuwa na uhuru na haki ya kutoa maoni yao waziwazi. Mwalimu Nyerere anasema hivi: “Demokrasia ya kweli ni lazima ihitaji kila mtu aweze kusema kwa uhuru kabisa na mawazo ya kila mtu lazima yasikilizwe. Hata kama mawazo ya mtu huyo hayapendwi kiasi gani au walio wengi wanadhani amepotea kiasi gani, si kitu.”

Vyovyote iwavyo, bado Tanzania ina kazi kubwa ya kuyafikia maendeleo ya uhakika na kamwe umaskini hauwezi kuondolewa kwa kaulimbiu tata au zile zenye kubebwa na mihemko ya wanasiasa. 

Ningeulizwa leo ni taifa gani ningependa tujenge, ningejibu: “Taifa la wapenda haki, linalojiendesha kwa tafiti za kisomi, taifa la watu wanaojali usawa miongoni mwao na kutendeana mema, taifa la watu wanaopenda kusema ukweli wakati wote, taifa la watu jasiri.”

Nihitimishe makala yangu kwa kuwaomba wasomi wa Tanzania wazitoe akili zao likizoni na kuzileta kwenye taifa lao. Taifa linahitaji mgongano wa kifikra. Mgongano huu wa kifikra utaliingiza taifa katika mijadala itakayoleta mawazo mbadala.

By Jamhuri