Antoine Griezmann alifunga mabao mawili na kuwawezesha Atletico Madrid kuwachapa Marseille 3-0 mjini Lyon, Ufaransa na kushinda Kombe la Europa League mara yao ya tatu katika kipindi cha miaka tisa.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa alianza kwa kufunga dakika ya 21 na kisha akafunga la pili dakika ya 49.

Nahodha wao Gabi alifunga bao la tatu dakika ya 89 na kuwawezesha vijana hao wa Madrid kushinda kombe hilo ambalo pia walilitwaa miaka 2010 na 2012.

Matokeo yangelikuwa tofauti iwapo mshambuliaji wa Marseille Valere Germain angetumia nafasi yake mapema kwenye mechi kabla ya Griezmann kufunga.

Nahodha wa Marseille Dimitri Payet aliondoka uwanjani akichechemea kutokana na jeraha baada ya kukaa uwanjani nusu saa, na sasa huenda akakosa kushiriki Kombe la Dunia.

Bila kiungo wao, Wafaransa waliwatishia Atletico mara moja, mshambuliaji wa zamani wa Fulham Kostas Mitroglou alipogonga mlingoti wa goli kwa mpira wa kichwa.

Atletico wamekuwa moja ya klabu ambazo zimekuwa zikifanya vyema sana Ulaya miaka ya karibuni.

Walifanikiwa kuzima ubabe wa Barcelona na Real Madrid La Liga kwa kushinda ligi 2013-14.

Kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili ligi kuu Uhispania wakiwa wamesalia na mechi moja na wamo mbioni kumaliza katika tatu bora kwa msimu wa sita mfululizo.

Katika kipindi hicho, wamefika fainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mara mbili, ambapo walishindwa na wapinzani wao wa jiji Real Madrid.

Meneja wao Diego Simeone alitazama mchezo huo kama shabiki kwani anatumikia adhabu ya mechi nne baada ya kuadhibiwa wakati wa mechi kati ya nusu fainali kati ya Arsenal na Atletico.

“Nina furaha sana,” alisema Griezmann baada ya mechi.

“Nimekuwa nikitia bidii kwa sababu ya tukio hili kwa miaka mingi. Niliondoka nyumbani nilipokuwa na miaka 14 juu ya hili. Tutasherehekea. Familia yangu iko hapa.”

 

By Jamhuri