Hawa ndio maadui wa Uislamu Tanzania

Tunapo kuwa tunajiuliza mhemko wa udini unatoka wapi au nani wameusababisha na kuuasisi si vibaya tukajua maadui wakuu kwa upande wetu waislamu. Ukimjua adui ni rahisi kupambana naye na ni nusu ya ushindi kwenye vita ya kutafuta haki au usawa au kuondoa tunao uita unyanyasaji kwa waislamu au mfumo kristo kama wengine wanavyo penda kuita (Mimi sio muumini wa dhana ya mfumo kristo) maana nimeona wakati wote waislamu wenzangu wakishika nafasi kubwa serikalini, kwenye mashirika ya umma na hata mashirika binafsi. 

Siuoni mfumo kristo kama unavyoitwa au kama baadhi ya waislamu wenzangu wengine wanavyotaka kuaminisha umma wa kiislamu juu ya hii dhana. Nasema sioni kwa kuwa bado naamini katika uwezo na si mfumo kristo, si uoni kwa kuwa hii nchi niya wakristo, wapagani, waislamu, wahindu na dini nyingine.

 

Si uoni mfumo kristo kwa kuwa nimeshuhudia watu kama kina omari mahita, na said mwema wakiwa viongozi wa vyombo ambavyo mara kadhaa vimesababisha mauwaji ya waislamu wenzetu na ndugu zetu wakristo pia.

 

Mtanisamehe bure wenye mtazamo tofauti na wangu lakini siuoni mfumo kristo nikimuangalia jk na makamu wake, si uoni mfumo kristo nikimuangalia wajina wangu Mohamedi sheini na sharif hamad, si uoni mfumo kristo nikimuangalia Chande othman yule jaji mkuu na Othamani Rashidi mkurugenzi wa usalama wa taifa, si uoni hata nikiungalia kwenye wizara na taasisi nyingine za serikali.


Wanao ongela mfumo kristo hawana udhibitisho wa kutosha kuhalalisha madai yao ambayo kwa sasa nayaita hayana mashiko bali yametawaliwa na ukame wa maono na kiangazi cha fikra kinacho piga macho pazia mchana wa jua kali.


Kwa waislamu na wasio kuwa waislamu, Lazima tutambue kuwa adui wa waislamu sio wakristo, wapagani, wahindu,au dini nyingine zinazopatikana kwenye huu ulimwengu.

Lazima tujue kuwa sisi ni ndugu tunaohitaji kuishi kwa upendo na kuvumiliana bila kuathiri imani zetu, na ikitokea lazima tutafute njia za amani kupata suluhu.


Kwa mtazamo wangu hawa ndio maadui wakubwa wa uislamu kwa Tanzania.

1. Adui namba moja kwa waislamu ni kutokuwa na mashule na vyuo vingi vyenye kutoa elimu bora kwa vijana wa kiislamu na hata wale wa upande wa pili wanaokuja kuitafuta elimu.

 

Najua kuna watu watapinga sana lakini ukweli mchungu lazima tuuseme ili tupate pa kuanzia, mtakuwa mashahidi hata shule tulizo nazo hazifanyi vizuri sana kwenye mitihani ya kitaifa lakini pia hata mashule yetu hayana mfumo wa kuandaa masheikh walio iva kwenye elimu dunia na akhera.

 

Mimi napendekeza harakati zetu ziwe kwenye kujenga mashule ya viwango pamoja na kuajiri walimu bora bila kujali dini zao ili kuwaandaa vijana bora wanao endana na kasi ya sayansi na teknolojia kuelekea soko la ajira ya ushindani na pia viongozi bora wa dini.


2. Ni kukubali kufanywa nyezo ya ccm kupata uhalali wa kutawala kwa kura za waislamu. Lazima tujue kuwa ccm wametutumia vya kutosha na kutudanganya vya kutosha, sasa tuseme basi! Mfano:~ Wametudanganya swala la mahakama ya kadhi wakati wa kampeni 2010 waislamu waliotaka tuwe na kadhi kwa kauli hadaa ya ccm wakapiga kura za kuhadaiwa lakini baada ya matokeo wakatugeuka! Huku ni kuonekana kuwa tu-malofa wa kudanganywa, tuunge mkono chama ambacho hakita tugawa lakini pia ambacho hakita tugawa na kuharibu umoja wetu wa kitaifa.


3.Bakwata imekuwa ni kama taasisi ya ccm, wanamuweka wanaye taka wao. Lazima tupiganie bakwata kiwe chombo huru cha waislamu na tuweke viongozi wenye maono mapana tunao taka sisi sio ccm hii itasaidia kurejesha imani kwa bakwata.

 

Napendekeza Qualification ya kuongoza Bakwata iwe ni pdh kwa kuangalia uwezo wa elimu akhera na elimu dunia lakini pia pamoja na uwezo wa kuongoza na kusimamia mambo. Chuo kikuu cha mum kinaweza kusaidia kuratibu kupatikana wataalamu na watendaji wengine wa bakwata ambao nao kiwango cha chini cha kuanzia kiwe shahada moja na kuendelea.


4.Kutokufuata mafundisho ya mtume. Mtume wetu Muhammad S. A. W alikuwa mwema, mwingi wa hekima na busara. Lazima tuyafuate mafundisho yake na kukumbushana mema na kukatazana mabaya, uislamu haujajengwa kwenye misingi ya uhasama, vurugu, fujo, chuki na mambo mengine mabaya.

 

Uislamu umejengwa kwenye misingi ya usafi wa matendo mema, kumcha Mungu, ukarimu, na kuhurumia na kuwajali wengine. Tukiyafanya haya tutawaepuka wale wanao utumia uislamu wetu kama daraja ambalo baadae hutuchafua wote. Mfano wale walio ingia kuchoma na kuvunja kanisa na kuiba sadaka, baadhi ya vifaa vya kanisa na mikate.


“Uislamu ni unadhifu” hii ni moja ya tafsiri ya hadithi za mtume wetu kipenzi Muhammad S. W. A. Tuyafuate mafundisho yake kwa matendo ili tumuenzi kipenzi chetu.

Wakatabahu.

Mohamedi Mtoi ameandika makala hii katika mitandao mbalimbali ya kijamii.