…Hivyo hatua ya kwanza kutekeleza mfumo mpya wa utawala kutoka ule wa ukoloni tuliorithi mwaka 1961, na ambao umetumika mpaka wakati ule mwaka 1971, ilikuwa kuteua viongozi wakuu wa kisiasa kwa mikoa na wilaya. 

 

Hawa waliitwa Wakuu wa Mikoa (Regional Commissioners-RCs) ambapo enzi za ukoloni wakiitwa Provincial Commissioners-PCs, Wakuu wa Wilaya ndiyo hao wakiitwa District Commissioners-DCs, sasa sisi tukaja kuwaita Area Commissioners-ACs.

Kwa upande wa uendeshaji Serikali, utaratibu tuliorithi mwaka 1961, watendaji wakuu ofisi ya PC au RC walikuwa ndiyo watawala na wasimamizi wa sheria na taratibu zote za utumishi serikalini. Hawa walijukana kama Maafisa Utawala Mikoa (Administrative Secretaries) wakati kule wilayani wakiitwa Mabwana Shauri (District Administrative Officers). Sisi baada ya Uhuru tukawaita Area Secretaries-AS.

Sasa kwa mfumo huu mpya wa madaraka mikoani, maafisa hawa walipewa kazi za kubuni mipango na kuisimamia kiutawala utekelezaji wake. Mwaka 1972 wakaitwa hivi. Mikoani wakawa Regional Development Directors (RDD) wakati kule wilayani wakaitwa District Development Directors -DDD yaani Wakurugenzi wa Maendeleo Mikoa na Wakurugenzi wa Maendeleo Wilaya. 

Ili utawala uende kweli kwa wananchi, mfumo wa Madaraka Mikoani ukatilia mkazo Serikali za mitaa yaani Local Government. Pole pole kukaandaliwa utaratibu wa kila wilaya kuwa na halmashauri zitakazoongozwa na Mwenyekiti wa kuchaguliwa na hapo ndipo wale DDD sasa wakajaitwa Wakurugenzi Watendaji (District Executive Directors) katika Halmashauri. Siku hizi tunawajua hawa DED (District Executive Directors) katika Manispaa kama Wakurugenzi wa Manispaa (Municipal Directors) au MD wakati katika majiji wanaitwa Wakurugenzi wa Majiji au City Directors (CDs).

Nimeeleza haya yote kwa sababu tu ya kutaka kuonesha mtiririko wa utawala. Wapo viongozi wa kisiasa kwa kusimamia sera na Ilani ya Chama Tawala katika kila mkoa na wilaya. Hawa ni makamisaa na wapo waendeshaji wa Serikali kazi yao kubuni, kupanga na kusimamia utekelezaji wake katika wilaya ndiyo wanaitwa wakurugenzi. Viongozi wote ni wateuliwa wa Rais, hivyo wanapaswa kufuata ule moyo wa kuwatumika wananchi tunaita katika majeshi ‘espirit de corps’ yaani moyo wa mshikamano katika nafasi zao hizo. Ni dhamana walizokabidhiwa na Rais kuendeleza maeneo yao ya utawala. 

Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya wanakasimu madaraka ya Rais, basi ni viongozi mbadala wa Rais mahali. Inaposikika Mkuu wa Mkoa anaitisha kikao cha utendaji ofisini halafu kunasikika wakuu wa wilaya na DED (Wakurugenzi wa Wilaya) hawahudhurii wanatuma wawakilishi, hapo mimi binafsi sielewi. Ningeita ni utovu wa nidhamu tu. Nisingekuwa na neno jingine mbadala.

Unaposikia mtendaji wa halmashauri fulani anapuuza mawazo ya Mkuu wa Wilaya (mwakilishi wa Rais katika wilaya) eti siyo mjumbe halali wa kikao cha Halmashauri, hapo inastajaabisha kweli. Sijui siku hizi dhana ya utawala bora inaitafsirije ile ‘chain of command’ mtiririko wa uamuzi wa utendaji pamoja na ule moyo wa mshikamano. 

Mwalimu aliliona tatizo kabla kabisa na ndiyo maana katika maelezo yake pale 1972 alisema hivi namnukuu tena ‘nor is it the intention of these proposals to create new LOCAL TYRANTS in the persons of Regional and District Development Directors. These officers will have overall responsibilities but DECENTRALIZATION exercise is based on the principle that more and more people must be trusted with responsibility.’ (Nyerere: Uhuru na Maendeleo Uk. 247). 

Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi; Mwalimu alionya kuwa mfumo ule wa kupeleka madaraka mikoani haukuwa na maana ya kujenga au kuwaweka madhalimu au madikteta kwa majina yale ya wakurugenzi wa mikoa na wakurugenzi wa wilaya maafisa hawa watawajibika katika mambo yote kwa hiyo madaraka mikoani ni zoezi linalodhamiria kuwahusisha watu wengi kuwajibika.

Mimi bado sijaelewa haya yaliyotokea kule mkoani Mwanza au kule wilayani Gairo, ambapo mfumo ule wa madaraka mikoani haukudhamiria kuleta mifarakano katika mikoa au wilaya, bali kinyume chake ulidhamiria kurahisisha uendeshaji wa kazi katika wilaya na mikoa. 

Katika miaka ile ya kwanza kwanza ya Uhuru wetu, migongano ya madaraka ilieleweka lakini siku hizi, miaka 55 ya utawala, na miaka 45 ya huo uendeshaji Serikali kwa ule mfumo wa madaraka mikoani, jamani mbona haieleweki? Labda kuna watu wanalewa na madaraka tu. Siyo kawaida katika nchi yetu yenye sifa ya utawala wa haki na wa sheria kutokea mambo kama haya wala hatupendi yatokee. 

Aidha, hata kule kusikia tu Rais akisema kuna mikwaruzano katika muhimili wa sheria (Judiciary) eti kati ya Mwanasheria Mkuu (AG) na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), hili nalo haliwezi kuelezeka katika nchi yenye kujigamba ina utawala bora na wa sheria. 

Hii mikwaruzano inazidi kuchelewesha haki kutendeka. Pale haki inapochelewesha si ndipo haki inapokosekana? Ukiritimba katika kesi ni njia mojawapo inayochelewesha utekelezaji wa haki za binadamu kwa raia.  Nadhani ucheleweshwaji wa kesi mbalimbali huko mahakamani unasababishwa na hili. Si ajabu pale Polisi wanaposema upelelezi bado unaendelea kumbe wanangojea uamuzi kutoka kwa DPP. 

Nadhani Watanzania wa leo wataendelea kujielimisha kwa kufuatamawazo yale ya waasisi wa Taifa hili. Waliamua mfumo wa Serikali unaowezesha wananchi kubuni, kupanga na kutekeleza uamuzi wao kwa faida yao wenyewe na siyo kugombania utambulishi eti ‘who is who in this or here’. Hapana. Hiyo haikuwa maana ya kubuniwa mfumo mzima wa Serikali kwa ile ‘decentralization’ na kuachilia mbali ule mfumo wa wakoloni tuliorithi mwaka 1961 katika nchi yetu. 

Ni matumaini yangu TAMISEMI na Judiciary watatatua upuuzi huo ulioanza kujitokeza hapa nchini. Aidha, Serikali itawadhihirishia wananchi utawala wa sheria na wa haki. Hapo unatakiwa mshikamano kati ya wawakilishi wa Rais na waendeshaji kwa utawala, ambao wote ni wateule wa Rais. HAPA KAZI TU siyo cheo cha nani ni nani katika mkoa au wilaya. Maendeleo ya nchi hii yataletwa na wananchi wote wazalendo thabiti. 

 

Mungu ibariki Tanzania. 

1615 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!