Wizara ya Nishati na Madini imetangaza kupunguza gharama za kuunganishia wateja wake umeme. Gharama hizo zimepungua kwa wastani wa asilimia 30 na 77. Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, bungeni mwishoni mwa wiki.

Tunaupongeza kwa dhati uamuzi wa Wizara hii. Gharama za kuunganisha umeme kwa muda mrefu zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi wengi vijijini na mijini kupata umeme. Hali hiyo ilichangiwa na uamuzi mbovu wa Serikali wa kuuza shamba la miti ya nguzo za umeme kwa raia wa kigeni. Hakika uamuzi huo ulikuwa hujuma kubwa kwa  Watanzania.

 

Kwa weledi wowote wanajua kuwa fedha za Tanesco hazitokani na kuunganishia wateja wake njia za umeme, bali zinatokana na matumizi ya umeme. Kwa sababu hiyo, kitendo cha kuwakomoa wananchi katika gharama za kuwaunganishia umeme si tu kwamba kilikuwa cha uonevu, bali kililenga kuwafanya Watanzania wengi waendelee kuikosa huduma hii muhimu.

 

Matarajio yetu ni kuona kuwa unafuu huu unawafikia walengwa, ikiwa ni pamoja na Wizara na Tanesco kupambana na watumishi wake wanaoomba rushwa kwa wateja wanaohitaji umeme na warasimu wenye visingizio vingi visivyokuwa vya maana. Aidha, kwa namna ya pekee tunawapongeza wabunge jasiri walioamua kupambana na wabunge wenzao wapenda rushwa.

 

Kwa miaka kadhaa sasa Tanesco imekuwa kichaka cha wafanyabiashara na viongozi wala rushwa kujinufaisha wao wenyewe na familia zao. Haikushangaza kuona kuwa baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando, kusimamishwa kazi kutokana na tuhuma zilizo wazi kabisa, kumejitokeza wabunge wala rushwa walioamua kumtetea.

 

Wabunge hao pia waliamua kuwa watetezi wakuu wa kampuni zilizoendelea kuinyonya nchi yetu kwa kuiuzia Tanesco mafuta kwa bei ghali mno, ilhali kukiwa na kampuni zinazouza kwa bei ndogo. Moto huu ulioonyeshwa na wabunge hawa jasiri unapaswa kuendelezwa ili liwe fundisho kwa wafanyabiashara na watumishi wengine wa umma wanaolikamua taifa letu. Tunaunga mkono juhudi zozote za kuendelea kupambana na mtandao huu dhalimu, ambao kwa miaka mingi umejijengea mazingira ya kuliibia Taifa letu.

 

Hata hivyo, tunaamini kuwa vyombo vya dola kwa upande wake navyo vitahakikisha vinaanza uchunguzi na ikibidi kuwachukulia hatua wahusika wote. Kuna habari za uhakika kwamba hata baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Tanesco wamo wanaojihusisha na biashara ndani ya kampuni hiyo na nyingine zenye nasaba na Tanesco. Hao nao hawana budi kuwajibishwa.

 

Muda wa kuendelea kuleana huku wananchi wakizidi kuumia umekwisha. Tunawapongeza Waziri,  naibu mawaziri na watendaji wote wa Wizara ya Nishati na Madini waliodhamiria kuwatumikia Watanzania kwa moyo wa dhati. Ni wajibu wa wananchi nao kuwaunga mkono. Wawasifu pale panapostahili na wawakosoe pale panapostahili kukosolewa. Kwa pamoja tutaijenga nchi yetu.

By Jamhuri