Siti alikuwa maskini wa sura lakini tajiri wa sauti. Alikuwa kinanda Afrika Mashariki na watu wakampenda. Alikuwa na kinywa cha mbubujiko mkubwa wa muziki. Alighani katika taarabu kwa miaka thelathini.

Alitumia ulimi wake kuvuta walio mbali kumsikiliza na wa karibu kumzungumza. Majivuno na makeke yalikuwa haramu kwake. Maneno na sauti yake murua yalikuwa kama ua la waridi katika umbo la mvuto na rihi nzuri.

Kuna methali ya Kiswahili isemayo: “Chanda chema huvikwa pete.” Msanii huyu wakati wa uhai wake hakutumia ulimi wake kama pilipili kuwasha vinywa vya watu ili vipate kusema maneno machafu na ya karaha.

Kutokana na methali hii nimeamua kumsifu na kumpongeza mwimbaji huyu aliyekitangaza na kukitukuza Kiswahili, kipawa chake, Uafrika wake, Kisiwa chake cha Unguja na nchi za Afrika Mashariki kwa taadhima kubwa. Waimbaji wangapi hapa nchini hivi sasa wana mtazamo kama huu?

Watunzi na waimbaji wa nyimbo wa leo wanajali ubora wa tungo zao, uimbaji wao na thamani ya vipawa vyao? Iwapo ndiyo.  Ni sababu zipi zinazofungia nyimbo zao na wao kusulubiwa? Iwapo hapana, yapi yanayowasibu hata washindwe kuwa kama Siti bint Saad?

Ikumbukwe Siti alipoimbwa: “Siti bint Saad, ulikuwa mtu lini, kama si sauti ungekula nini?”  Yeye akajibu: “Si hoja uzuri, na sura jamali. Hasara ya mtu kukosa akili?” Majibu haya, yake mwenyewe yalisumbua fahamu zake. Ikambidi aitake radhi hadhira yake.

Katika kuomba radhi bila kigugumizi na shaka, alisimama mbele ya hadhira na kuimba:

Si kusudi langu,  Kuvunja watani,

Enyi Walimwengu, Mwajua yakini,

Apendalo Mungu, Haliwezekani.

Je, waimbaji wangapi nchini wanamaizi tungo zao ziko safi au chafu?

Naomba nieleweke, Siti katika fasihi hii ni kielelezo cha ushahidi wa watunzi na waimbaji kama vile: Daima Abdallah, Kida Waziri, Tabia Mwanjelwa, Marijan Rajabu, Mbaraka Mwinshehe, Salum Abdallah, Frank Joseph Humphrey na wengine, nyimbo zao zimejaa maudhui yenye mafunzo na hekima pamoja na ladha isiyo chuja wala kuchosha kusikia.

Kwa mfano wimbo ‘Malaika’ utunzi wake Frank J. Humphrey (marehemu) chotara wa Kichaga na Kiswidishi, umenakiliwa, umeboreshwa na kuimbwa na waimbaji mbalimbali duniani kwa sababu ya maudhui yake. Baadhi ya waimbaji ni Miriam Makeba, Fadhil Williams, Raaj Gambhir, Lata Mangeshkar na Bonney M.

Wimbo ‘Yalaiti’ umeimbwa na Siti bint Saad na kurekodiwa katika studio ya Kampuni ya Santuri ya Kolumbia (Columbia) ya Bombay, India, mwaka 1930. Umeboreshwa na kuimbwa na waimbaji mbalimbali katika sherehe za harusi na kwenye majumba ya burudani.

Baadhi ya waimbaji wa wimbo huu ni Asha Abdallah (Bi Malika) na MwanaFA, akimshirikisha Linah. Wimbo halisi ni huu hapa.

Yalaiti kupenda pasi kifani,

Tofauti sikutilii moyoni,

Sikuachi leo na kesho peponi.

Aaaaah Aaaaah…

Yalaiti pendo langu la moyoni,

Tofauti wala shaka sina ndani,

Sikuachi leo na kesho peponi.

Sikitiko nikipita mlangoni,

Zamu yako nawe wajua yakini,

Siniache leo na kesho peponi.

Jicho langu halifunga mlangoni,

Nyonda wangu natizama simuoni,

Nia yangu leo na kesho peponi.

Naamini wasanii wote wa nyimbo ziwe za taarabu, reggae, dansi, hip hop na kadhalika mmenifahamu. Nawaomba tungo zenu zitoe mafunzo mazuri na kukanya maovu. Zenye kusifu na kuhimiza kazi, utu na juhudi zetu, maombolezo, malezi,  adabu na mapenzi yetu.

Mkizingatia utunzi na uimbaji mzuri mtawezesha na kufungua soko lenye tija, kwa sababu nyimbo zitapendwa na kununuliwa. Msiache kuboresha nyimbo za watangulizi wenu kwa kuweka vionjo vipya au vya kisasa katika mapigo ya ngoma (rhythm), sauti tamu zinazofuatana na wimbo (melody).

By Jamhuri