Walimu wanapolalamika kwamba wanatumia vitabu vibovu kufundishia, hapana shaka wengi hawajui ukubwa na uzito wa tatizo hili.

Kuna walimu katika shule zetu wanajua mambo sahihi lakini wanalazimika kufundisha mambo potofu yaliyomo vitabuni kwa sababu wasipofanya hivyo wanafunzi wao watashindwa mtihani! Masuala ya mitihani ya Taifa hutoka kwenye vitabu hivi vibovu. Kwa kweli, walimu wana wakati mgumu.

Utitiri wa vitabu uliopo mashuleni kwa somo moja darasa moja umeathiri sana elimu ya Tanzania. Hii ni kwa sababu waandishi wengi wa vitabu hawana ujuzi wa kuandika vitabu, pia hawana ujuzi wa kutosha kuhusu masomo wanayoyaandikia vitabu. Husukumwa kuandika vitabu kwa lengo la kujipatia fedha.

Wachapishaji wa vitabu wametoa vitabu vingi visivyokidhi mahitaji ya elimu, na vinavyosababisha wanafunzi wa shule za msingi kumaliza masomo yao wakiwa wanajua mambo mengi lakini yote potofu. Kwa hiyo, wanajiunga na masomo ya sekondari wakiwa hawajui kitu. Hili ni janga la kitaifa.

Binafsi, masomo yangu ni ya Historia na Uraia. Haya ni masomo ambayo nimeendelea kuyaendeshea semina za walimu na kwa njia hiyo nimejionea mwenyewe, historia iliyopotoshwa vitabuni na inavyoendelea kupotoshwa mashuleni.

Nina mifano hai kutoka vitabu vya historia vya darasa la nne na la sita vilivyochapishwa na kampuni ya vitabu ya Education Books Publishers, mwandishi wao ni N. K. Ndosi. Tuanze kwa kitabu cha historia darasa la nne ambacho katika ukurasa wa 62-63 kinazungumzia viongozi wa jadi wa baadhi ya jamii za wakulima na wahunzi Tanzania.

Wanafunzi wanafundishwa kwamba Mataka alikuwa mwene eneo la Songea kabila la Wayao. Kumbe Mataka alikuwa Sultani eneo la Tunduru. Mwene alikuwa kiongozi wa jadi wa Wafipa na Wamakua. Na eneo la Songea kuna Wangoni si Wayao.

Wanafunzi wanafundishwa kwamba Kimweri alikuwa Zumbe. Kumbe hakuwa Zumbe bali alikuwa Sultani wa Wasambaa. Halafu tunasoma kwamba Said alikuwa Sultani wa Unguja. Na huyu pia ametiwa katika orodha ya viongozi wa jadi wa baadhi ya makabila ya wakulima Tanzania.

Kisha tunasoma kwamba Mangungo alikuwa mtemi eneo la Usagara katika kabila la Waluguru! Huu ni upotoshaji wa kutisha. Sisi sote tunajua kwamba Mangungo alikuwa sultani (hakuwa mtemi) eneo la Mvomero, Kilosa, na hakuwa Mluguru. Alikuwa mtu wa kabila la Wasagara.

Halafu kitabu kinatwambia kwamba, Marere alikuwa mwene eneo la Tunduru kabila la Wayao! Huu tena ni upotoshaji wa kupindukia. Na punde tu tumeambiwa Wayao wapo Songea. Merere hakuwa kiongozi wa Wayao wa Tunduru, alikuwa kiongozi wa Wasangu wa Mbeya. 

Hii ni mifano michache tu katikati ya mifano mingi inayothibitisha wanafunzi wa darasa la nne wanavyoendelea kufundishwa mambo potofu katika historia ya Tanzania kila siku wanayokwenda shule.

Sasa tuangalie kitabu cha darasa la sita. Ukurasa wa pili wa kitabu hiki unamzungumzia Vasco da Gama, kiongozi wa kwanza wa Wareno kuingia Afrika Mashariki. Tunaambiwa kuwa Vasco da Gama alipita Kilwa mwaka 1498, kisha akaenda Bagamoyo na Tanga na kisha akaingia Zanzibar.

Kumbe mwaka 1498 Vasco da Gama hakupita Tanzania, alishuka Mombasa akaendelea Malindi kisha India. Vasco da Gama alifika Kilwa kwa mara ya kwanza Julai 6, 1502.

Ukurasa wa 10 kitabu kinasema kwamba Sultani wa Oman alianza utawala wa kikoloni Zanzibar. Waarabu hawakuendesha utawala wa kikoloni Afrika Mashariki. Utawala wa kikoloni uliendeshwa na Wajerumani na Waingereza.

Ukurasa wa 11 kitabu kinatwambia kwamba mwaka 1844 wamisheni wa kwanza kutoka Ujerumani walifika Tanganyika na kwamba walikuwa wamisheni wa Church Missionary Society (CMS). Tunaendelea kuambiwa kwamba wamisheni hao wa CMS ndiyo walioanzisha misheni ya kwanza Magila, Mkoa wa Tanga.

Ukweli ni kwamba alikuwa mmisheni mmoja tu wa CMS, Johann Krapf, aliyefika Afrika Mashariki mwaka 1844. Hakufika Tanganyika. Alikwenda moja kwa moja Rabai, Mombasa, alikoanzisha  misheni ya kwanza ya Kikristo Afrika Mashariki. Basi, misheni ya Magila haikuanzishwa na wamisheni wa CMS. Ilianzishwa na mmisheni wa Kanisa la Anglikana, Charles Allington, tena haikuanzishwa mwaka 1844 bali ilianzishwa Januari 20, 1868.

Ukurasa wa 18 unatwambia kuwa Ujerumani iliendelea kutawala Tanganyika hadi mwaka 1918. Kumbe tayari mwaka 1917 Waingereza walikuwa wameanza kutawala Tanganyika makao makuu ya awali ya utawala wao yakiwa Lushoto. Wajerumani walifukuzwa kabisa Tanganyika Novemba 13, 1917 wakati Waingereza walipoteka mji wa Masasi wakaingia Msumbiji.

Katika ukurasa wa 47 tunaambiwa kwamba Abushiri bin Salim alianza kupambana na Wajerumani mwaka 1886, kumbe alianza kupambana nao Septemba 8, 1888. Ukurasa wa 48 unasema kwamba Machemba alianza kupambana na Wajerumani mwaka 1890 akipinga kodi ya nyumba waliyoanzisha. Kumbe Wajerumani walianzisha kodi ya nyumba mwaka 1895 na ni mwaka huo Machemba alipoanza kupambana nao.

Katika ukurasa wa 51 tunasoma kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa Mwenyekiti wa TANU kumbe alikuwa Rais wa TANU.

Ukurasa wa 58 unazungumzia Mkutano wa Katiba ya Tangangika. Tumeambiwa kwamba mkutano huo ulifanyika Lancaster, Uingereza mwaka 1960. Mkutano huo ulifanyika Dar es Salaam, Tanganyika. Tena si mwaka 1960 bali ni Machi 27-29, 1961.

Ukurasa wa 69 unataja mimea miwili iliyomo katika nembo ya Taifa kuwa ni pamba na kahawa! Kumbe ni pamba na karafuu. Na katika ukurasa wa 79 tunasoma kwamba Azimio la Arusha lilitangazwa Arusha wakati lilitangazwa Dar es Salaam.

Kwa kweli nafasi haitoshi kuorodhesa upotofu wote wanaofundishwa watoto wetu kwa kutumia vitabu hivi vya Education Books Publishers. Jambo moja linashangaza, vitabu hivi vilipitishwa na wasomi Wizara ya Elimu. Vilipitishwa kihalali au kwa rushwa?

Ukweli ni kwamba Wizara ya Elimu imeshindwa kuwatumia vizuri waandishi bora wa vitabu wenye ujuzi wa kutosha wa kuandika vitabu na ujuzi wa kusoma wanayoyaandikia vitabu.

Tukirudi nyuma, tutaona kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli imeanza kutoa elimu bure. Hili ni jambo zuri. Lakini elimu hii ni bure katikati ya uzushi na upotofu mtupu uliomo vitabuni kama nilivyothibitisha.

Katika mazingira hayo, hapana shaka Serikali ya Rais Magufuli itachukua hatua za makusudi zitakazotumbua mashuleni majipu haya ya vitabu haraka iwezekanavyo ili watoto wetu wapate elimu bora.

Wakati huo huo, Serikali ifikirie upya suala la waandishi wa vitabu kupitisha miswada yao kwa wachapishaji wa vitabu. Baadhi yao ni wezi sugu wa kazi za waandishi ambapo vitabu vikipitishwa na Wizara ya Elimu huvichapisha na kuviuza bila kumlipa chochote mwandishi. 

Haya ni majipu ambayo siku zake za kutumbuliwa zinahesabika.

By Jamhuri