Wiki iliyopita Tanzania imeongeza jiji jingine kwenye orodha yake. Arusha imeungana na majiji mengine yaliyoitangulia- Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Tanga. Mamilioni ya shilingi yametumika kwenye uzinduzi rasmi uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete, wakati wa ziara yake mkoani Arusha. Kitu cha maana zaidi kilichofanywa na Rais Kikwete kwenye ziara hiyo ni uzinduzi wa Chuo cha Nelson Mandela, kitakachosaidia kuibua na kuendeleza vipaji katika fani ya sayansi hapa nchini.

Jambo la kufurahisha zaidi ni pale Rais Kikwete alipoiambia hadhira kwamba ujenzi wa chuo hicho, umefanywa kwa fedha zetu za ndani (Sh zaidi ya bilioni 90) kutoka katika mifumo ya hifadhi ya jamii.

 

Kwa maelezo ya Rais, uamuzi wa kutumia fedha za mifuko ya hifadhi ulikuja baada ya wafadhili, ikiwamo Benki ya Dunia, kutugomea kutoa fedha za ujenzi huo. Hili ni fundisho kubwa kwetu. Hatujui ni kwanini waligoma, lakini ukweli ni kwamba Wazungu wengi hawajawahi kuwa marafiki wa kweli wa Waafrika.

 

Kusikia kwamba tunajenga chuo cha sayansi kwao ni maudhi. Wazungu wangapi wanafurahi kuona Afrika ikikua kisayansi na kiteknolojia? Kama tungewapelekea maombi ya fedha za semina, bila shaka wangetumwagia haraka sana, maana wanataka waendelee kutuona tukiwa wacheza ngoma na tunaoishia kwenye semina, makongamano, warsha na mikutano isiyo na tija.

 

Tunawapongeza sana kwa kutunyima msaada huo, kiasi kwamba tumepata akili ya kutambua kuwa KUJITEGEMEA ni jambo la maana sana kwetu Waafrika. Wazungu wakiendelea kutunyima misaada tunaweza kupata akili ya kujikomboa.

 

Tunasema hivyo kwa sababu ni jambo la ajabu sana kwa nchi tajiri kama yetu, nchi yenye aina zote za rasilimali na maliasili zisizo na mfano, kuendelea kuhemea kwa Wazungu. Aibu.

 

Kwa sababu ya misaada, tumekosa utashi wa kuhakikisha watoto katika Taifa letu wanapata madawati. Tunabaki tukisubiri misaada ya Wazungu kutuletea madawati wakati nchi yetu ina miti na mbao nyingi. Hii ni aibu. Katika hili, tunaomba Wazungu waendelee na msimamo huo huo wa kutunyima ili hatimaye tuweze kutoka kwenye aibu hii ya kuwa ombaomba.

 

Pili, pamoja na ukweli kwamba Rais Kikwete amefanya uzinduzi wa Jiji la Arusha kwa mbwembwe, hatuoni kama kweli mji huo ulistahili hadhi ya kugeuzwa jiji. Tunajiuliza, hivi kigezo kikuu cha mji kupandishwa hadhi ni kipi? Je, ni wingi wa watu? Tunauliza hivyo kwa sababu kwa Arusha, kigezo pekee cha kuifanya japo ikaribie kuwa na hadhi ya kuitwa jiji, ni idadi ya watu.

 

Ukiacha idadi ya watu, Arusha haina sifa nyingine ya kuitwa jiji. Tena, basi si Arusha tu, bali majiji yote ya Tanzania hayana sifa ya kuwa majiji. Kama uchafu na uchovu wa miundombinu vimegeuzwa na kuwa vigezo vya mji kupandishwa hadhi, sawa!

 

Katika Arusha, ebu tujaribu kuangalia maeneo kama Ngarenaro, Sekei, Sanawari, Sinoni, Kimandolu, Kijenge, Mianzini, Unga Limited au Daraja Mbili au hata Luvolosi (Mji Mpya), wapi kuna barabara ya maana? Wapi kuna miundombinu ya majisafi na majitaka? Wapi kuna maeneo ya wazi kwa ajili ya michezo mbalimbali? Wapi katika maeneo hayo ambako kumepimwa na hivyo kulifanya jiji liwe la kisasa, lililopangiliwa vizuri na lisilohitaji mgeni kusindikizwa hadi mlangoni na mwenyeji wake? Jibu ni moja, hakuna.

 

Wito wetu ni kwamba upandishaji hadhi miji usifanywe kisiasa au kuwaridhisha watu kutokana na matamanio yao. Lazima kuwe na vigezo thabiti vya kuufanya mji ustahili kupandishwa hadhi. Hivi wakubwa wa nchi hii wanaposafiri nje hawaoni majiji ya wenzetu? Huwa wanakwenda kujifunza nini? Kwa hili la upandishaji hadhi miji yetu kienyeji, ni rahisi zaidi kusema haya ni “mazizi”, na kamwe si “majiji”.

 

By Jamhuri