KWENYE wallet (pochi ya kutunzia fedha) ya kada wa klabu ya Yanga, Sudi ‘Tall’ Hussein pamoja na kuchukua mambo mengine ndani yake kuna kipande cha gazeti la michezo la MWANAspoti.

Anatembea nacho. Mara nyingi akikutana na mtu anayetaka kujadiliana naye kuhusu masuala ya soka, basi hukitoa na kuelezea wasiwasi juu ya Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ akidai anahujumu soka la Tanzania.

Ni hivi, kabla ya Uchaguzi Mkuu Simba, Kaburu alitangaza neema kwa mashabiki wa Simba akielezea kuwa timu itakuwa inashinda kila mechi ili kuwaletea faraja Wanamsimbazi.

Katika tambo hiyo ya kuomba kura kwa wanachama kabla ya uchaguzi wa klabu hiyo uliofanyika mapema mwaka huu, Kaburu aliahidi kutafuta pointi tatu ndani na nje ya uwanja.

Maneno, “…ndani na nje ya uwanja”, ndiyo hasa yanamtesa Sudi Tall ambaye moja kwa moja anaona wazi aibu inaweza kuanza kutokea Oktoba 18, mwaka huu katika mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga.

Hofu ya Sudi Tall ni kwamba Kaburu ana nyadhifa tano ikiwamo hiyo ya umakamu mwenyekiti wa klabu ya Simba.

Anasema; “Huyu bwana ukiacha umakamu mwenyekiti wa Simba ambao ni cheo cha kwanza, pili ni Mjumbe Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na tatu ni Kigogo kwenye kamati ya mashindano ya TFF ambako ndani yake waamuzi wote wako chini yake.”

“Nne ni Mjumbe wa Bodi inayosimamia Ligi Kuu Bara na zaidi ya hapo ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, sasa wewe unadhani mtu huyu akiamua kuhujumu anashindwa?” anahoji Sudi Tall.

Kwa nyadhifa hizo, Sudi Tall anamuona Kaburu ni mtu hatari na katika hilo hasiti kusisitiza akisema; “Kaka Kaburu ni mtu hatari. We acha tu, atatuangamiza mtu kwa vyeo vyake.”

Sudi Tall anachomeka “fitina” kwamba Kaburu alijiuzulu umakamu mwenyekiti Simba chini ya uongozi wa Ismail Aden Rage, ambako pamoja na sababu nyingine ni kwamba bosi wake alikuwa hawajibiki ipasavyo.

Hii ni kwa sababu Rage alikuwa na vyeo vingi kama vile mwenyekiti wa klabu hiyo, mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Tabora na zaidi ya hapo mbunge wa Tabora Mjini.

Rage kwa sasa si kiongozi wa Simba na mwenye vyeo zaidi ya vitatu ni Kaburu, je atajiuzulu baadhi ya nyadhifa zake ili atimize majukumu yake vema mara baada ya Simba kuwa na mwendo wa kusuasua kutokana na sare?

Wenyeji hao wa mtaa wa Msimbazi wakijiita Wekundu wa Msimbazi wamekipiga mechi tatu hadi Jumamosi iliyopita na kutoka sare katika michezo wa Ligi Kuu Bara. Naam, mpaka sasa Simba imeambulia pointi tatu tu.

Achana na Sudi Tall, baadhi ya wanachama wa Simba wenyewe hawamwangalii vema Kaburu kwani walipata kumweleza wazi kwamba anagawa wachezaji wa timu hiyo.

Shutuma nyingine dhidi yake ni kwamba anauza wachezaji mahiri wa timu hiyo ambao wangeiletea faraja Simba. Shutuma zote hizo Kaburu alizijibu kwenye habari ambayo kipande cha gazeti hilo anatembea nacho Sudi Tall.

Majibu ya Kaburu yalikuwa ni hivi, mosi ni kwamba yeye hagawi wachezaji kama inavyoelezwa na mara zote timu inapokwama yeye hufuatwa ili kuokoa jahazi. Swali la kujiuliza, mbona sasa yuko ndani ya uongozi na matokeo ni ya kuchechemea?

Pili kuhusu kuuza wachezaji, alisema: “Kamati ya Utendaji ya Simba ndiyo inayouza wachezaji kwa makubaliano na kihalali.” Swali la kujiuliza mbona sasa timu ilikuwa imepambwa kwa kuwachukua akina Emmanuel Okwi na Paul Kiongera, mabao hakuna?

Maswali kama hayo yanaibuka kutokana mbwembwe za Kaburu wakati wa kuomba kura kuongoza klabu hiyo akisema, “Simba ilichepuka msimu uliopita hadi kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara.”

Alitaka kuchaguliwa ili angalau tu, airejeshe timu hiyo kwenye kile alichokiita, “Njia kuu.” Alisema kwamba wamchague yeye na Evans Aveva ambaye alichaguliwa kuwa mwenyekiti, ili wairejeshe Simba kwenye mstari sahihi.

Haya! Walichaguliwa, lakini kiko wapi? Je, Wanasimba waamini kwamba Kaburu huyo ambaye huitwa wakati wa matatizo ni ‘kirusi’ kwa Simba na Soka la Tanzania kama ambavyo Sudi Tall anataka watu waamini?

Au zile tetesi kwamba Kaburu amekasirika baada ya swahiba wake, Zdravko Logarusic kutimuliwa na nafasi yake kuchukua Patrick Phiri, kipenzi cha Aveva? JAMHURI na mwandishi wake, hawana majibu labda mpaka Kaburu atakaporidhia kusema kinachojiri ndani ya klabu hiyo.

Kwa maoni na ushauri: 0719 088 111

alfredkadenge@gmail.com

1236 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!