Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, Hamza Johari amesema, kufuatia huduma waliyoitoa kwa ndege ya Emirates iliyotua nchini kwa dharura, Tanzania sasa imepanda katika viwango vya kimataifa na kufikia asilimia 64 kutoka asilimia 37 vilivyowekwa na Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO).

Ndege hiyo ya gharofa iliyotua kwa dharura nchini, ilikuwa na abiria zaidi ya 400 na wote walihudumiwa katika hoteli mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi huyo amesema, kufuatia hatua hiyo sasa Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) limeandaa tuzo maalum itakayotolewa na Rais wa shirika hilo kwa kumkabidhi Rais John Magufuli na mawasiliano yanafanyika kufuatia ujio huo wa Rais wa ICAO.

Akizungumza na waandishi katika Ofisi za Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), mkurugenzi huyo amesema, kutua kwa ndege hiyo kubwa ya ghorofa aina ya A380 ya Shirika la Ndege la Fly Emirates kumedhihirisha kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na vyombo vyake ni madhubuti katika usafiri wa anga.

Aliongeza pia ndege hiyo kabla ya kuondoka ilijaza mafuta zaidi ya lita 90,000, jambo ambalo limeongeza biashara ya mafuta na kipato kwa nchi.

By Jamhuri