. Wanaohamishwa hawajui watakacholipwa

. RC Dar, diwani wawataka wavute subira

. Tibaijuka, Nagu watafutwa bila mafanikio

Hofu ya kuchakachuliwa fidia imetanda miongoni mwa wananchi wanaohamishwa kupisha ujenzi wa Kituo cha Uwekezaji cha Kimataifa katika Kata ya Kurasini, jijini Dar es Salaam.

Mradi huo utajengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na China katika eneo lenye ukubwa wa hekta 670 (sawa na ekari 1,675). Inaelezwa kuwa kiasi cha Sh bilioni 90.4 kimetengwa kugharimia ujenzi huo.

 

Aprili mwaka huu, nyumba 994 katika mitaa ya Mivinjeni, Shimo la Udongo na Kiungani zilifanyiwa thathmini lakini wamiliki husika hawajafahamishwa kiasi cha fedha watakacholipwa kama fidia ya kuhamishwa.

 

Wamiliki wa nyumba hizo pia wanaishutumu serikali kwa kushindwa kutekeleza ahadi ya kuwalipa fidia husika kati ya Mei na Juni, mwaka huu, badala yake imeendelea kukaa kimya bila kuwajulisha kilichokwamisha utekelezaji wa ahadi hiyo.

 

Usiri wa kiasi cha fedha watakacholipwa na ucheleweshaji wa fidia hiyo vimewasababisha wananchi hao kuhofia uhakika wa maisha yao mapya katika eneo la Uvumba, Kigamboni wanakotarajia kugawiwa viwanja kwa ajili ya kujijengea makazi mapya.

 

Wiki iliyopita, JAMHURI ilizuru Kurasini na kufanya mahojiano maalumu na wananchi wanaosubiri kuhamishwa. Wengi wameelezea kutoridhishwa kwao na usiri wa serikali katika mpango huo.

 

Wataja hofu yao

“Nyumba zetu zimefanyiwa tathmini lakini serikali haijatueleza kila mmoja atalipwa kiasi gani, hizi zinaweza kuwa dalili za kutupunja fidia,” amesema mkazi wa Kiungani, Gabriel Toto.

 

Toto anataja wasiwasi mwingine unaomnyima usingizi kuwa ni huenda mwisho wa siku serikali itawalazimisha kupokea kiasi kidogo cha fedha kisicholingana na thamani halisi ya nyumba zao na kutumia nguvu ya dola kuzibomoa na kuwaondoa eneo hilo.

 

Mkazi wa Mivinjeni, Hajida Yusufu Kaniki, anasema, “Kitu kibaya zaidi ni kwamba walikuja wakatia X kwenye nyumba zetu na kutuzuia kufanya maendeleo yoyote, yaani wametuacha njia panda.”

 

Hadija anaamini kwamba dalili ya mvua ni mawingu, hivyo hatua ya serikali kuchelewa kuweka wazi kiasi cha fedha ambacho kila mmoja wao anastahili kulipwa kinaweza kutoa mwanya wa kuchakachua fidia hizo.

 

Kwa upande wake, mkazi mwingine wa Mivinjeni, Mwanahawa Khamis yeye anahofu kwamba huenda fedha watakazolipwa hazitatosha kugharimia ujenzi wa makazi mapya katika eneo la Uvumba.

 

“Pia nina wasiwasi kwamba hata viwanja tutakavyogawiwa huko Uvumba huenda havitakidhi mahitaji ya kuishi na familia zetu,” anasema Mwanahawa.

 

Gabriel Mbelwa “Bonge”, mkazi wa Shimo la Udongo, anasema, “Serikali imetufumba… hatujui hatma ya fidia za nyumba zetu na maisha yetu ya baadaye, na si ajabu tukaamriwa kuondoka kabla hatujalipwa haki zetu.”

 

Wasimulia wanavyoyumba kiuchumi

Wananchi hao kwa upande mwingine, wameeleza namna wanavyoendelea kuyumba kiuchumi tangu serikali itangaze mpango wa kuwahamisha.

 

“Tangu maofisa wa serikali waweke alama za X kwenye nyumba zetu na kutuzuia kufanya maendeleo zaidi katika maeneo ya makazi yetu, wapangaji wamehama hali ambayo imetukosesha kipato,” anasema mkazi wa Shimo la Udongo aliyejitambulisha kwa jina moja la Ibrahim.

 

Anaongeza, “Kipato chetu kikubwa sisi wenye nyumba kinatokana na wapangaji wa vyumba vya kuishi na kuendeshea biashara lakini wote wamekimbia, tumezuiwa kulima hata bustani ya mbogamboga na matunda, sasa hivi tunakosa fedha za kuwalipia watoto wetu ada za shule, haya ni mateso.”

 

Mwanahawa Khamis anasema, “Tungependa kuona serikali inatulipa haki yetu kwa uwazi na kutupeleka sehemu yenye unafuu zaidi ili tubadilishe maisha yetu yawe bora kwa sababu kitega uchumi inachotaka kuweka hapa kitakuwa na maslahi makubwa serikalini.”

 

Diwani Kurasini azungumza

Alipoulizwa na JAMHURI iwapo anayafahamu malalamiko ya wananchi hao na jinsi anavyoyashughulikia, Diwani wa Kata ya Kurasini, Wilfred Kimati amesema:

 

“Ninachoweza kuwambia wananchi hawa ni kwamba waondoe hofu, ni jambo la kuvuta subira tu, hakuna utapeli kwenye mradi ule.

 

“Fedha na viwanja [watakavyogawiwa] ni haki yao na cheki zao zitatolewa baada ya Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) kuhakiki idadi ya nyumba na viwango vya thamani ya nyumba zao.”

 

Kimati anasema anajipanga kuitisha mkutano wa hadhara wa wakazi wa Mivinjeni, Shimo la Udongo na Kiungani kuwaondoa hofu kwa kuwaeleza kinachoendela katika utekelezaji wa mpango mzima wa kuwahamisha.

 

RC Dar es Salaam anena

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa (RC) wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki amesema uamuzi wa serikali wa kutotangaza mapema viwango vya fedha watakavyolipwa wananchi hao umezingatia taratibu na kanuni za kushughulikia suala hilo.

 

“Tathmini ina utaratibu wake, huwezi kutangaza public (hadharani) kabla ya kupitia process (taratibu), mpaka Mdhamini Mkuu wa Serikali apitie na kuthibitisha,” amesema Sadiki na kuongeza:

 

“Hakuna negotiation (majadiliano) kwenye tathmini. Wananchi wafanye subira tu mamlaka zinazohusika zifanye kazi yake inavyotakiwa.”

 

Juhudi za kuwapata Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu ili wazungumzie suala hilo hazikuzaa matunda baada ya JAMHURI kuwapigia simu zao za mkononi mara kadhaa kwa nyakati tofauti lakini mara zote ziliita na kukata bila kupokewa.

1365 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!