Hongera Nassari, hongera Chadema

Wapigakura wa Arumeru Mashariki wameamua. Wamemchagua mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joshua Nassari kuwa mbunge wao. Nassari amewashinda wagombea wengine saba wa vyama vya siasa, akiwamo Sioi Sumari aliyekuwa akiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwa namna ya pekee tunampongeza Nassari na Chadema kwa ushindi huo, katika uchaguzi uliokuwa wa ushindani mkali. Tunawapongeza wananchi wa Arumeru Mashariki kwa kutumia haki yao ya kikatiba ya kumchangua kiongozi wanayeamini kwamba anaweza kutatua kero kubwa za ardhi, maji, barabara, huduma za afya na nyingine nyingi.

Uchaguzi wa Arumeru Mashariki ulikuwa wa aina yake. Tumeshuhudia baadhi ya wanasiasa wakienda nje ya mada na kuanza kushambuliana.  Katika hili, CCM hawawezi kukwepa lawama. Baadhi ya wapigadebe wa CCM walidiriki kutoa kauli za matusi na nyingine ambazo kwa mtu mweledi, ilikuwa vigumu kuamini kama kweli waliokuwa wakizitoa ni viongozi kutoka chama kinachotawala.

Kwa mfano, tangu mwanzo hadi mwisho wa kampeni walisema Chadema ni chama kinachotetea ushoga, Katibu Mkuu wa Chadema eti aliiba fedha za ujio wa Baba Mtakatifu, Yohane Paulo II; mgombea wa Chadema ni gunzi, Chadema ni chama cha vurugu, Vincent Nyerere si mmoja wa wanafamilia ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere; na maneno mengine mengi yasiyokuwa na maana.

Kwa mara ya kwanza, Chadema walionekana kujikita zaidi kwenye sera na ahadi za kupambana na changamoto zinazowakabili wananchi wa Arumeru Mashariki, badala ya matusi.  Ni vema wanasiasa wakatambua kuwa wananchi wanabadilika sana. Wameanza kutambua pumba na mchele.  Matokeo ya Arumeru Mashariki yanaonyesha kuwa CCM wameanguka kwa kura nyingi katika maeneo ya vijijini.

Hii ni tofauti kabisa na hapo awali ambako kura nyingi za ushindi kwa CCM zilitoka maeneo hayo. Hii ni dalili kwamba wananchi wameanza kung’amua kuwa CCM hawana hatimiliki ya kuliongoza taifa hili milele. Kama chama hicho kitalitambua hilo, kitajirekebisha. Kushindwa kwa CCM Arumeru Mashariki kunapaswa kuwa funzo kwa chama hicho.  Lazima wanachama na viongozi wake waketi na kuona kama kweli ugomvi miongoni mwao una tija kwao na kwa taifa.

Ugomvi usiokuwa na maana unaoendelea baina ya makundi ndani ya CCM ni mwanzo wa kifo cha chama hicho. Chadema wameshinda. Huu si wakati wa kusherehekea ushindi. Ni wakati wa kutafakari ni kwa namna gani wanaweza kuanza kutekeleza ahadi zao kwa kasi ya hali ya juu. Wakumbuke kuwa muda walionao ni mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, hivyo wanapaswa kuanza mapambano sasa hata kabla ya Nassari kuapishwa bungeni wiki ijayo. Kwa mara nyingine tunampongeza Nassari kwa dhati kabisa tukiamini kuwa aliyoyaahidi kwa wananchi atayatekeleza kwa kasi itakayomsaidia kuomba ridhaa ya kukalia kiti hicho tena mwaka 2015. Hongera sana Nassari. Hongera sana Chadema.