Jumamosi hii Watanzania wakaazi wa Zanzibar wanasherehekea miaka 49 ya Mapinduzi yaliyofanyika Januari 12, 1964 baada ya kuwapo sintofahamu kutokana na uchaguzi uliovurundwa na mkono wa wakoloni kukandamiza wazawa wafuasi wa African Shiraz Party (ASP). Tunafahamu historia hii inafahamika vyema kwa kila Mtanzania kwenye kufuatilia historia. Tunafahamu pia malengo ya msingi ya kufanyika kwa mapinduzi haya.

Mapinduzi Matufuku yametokea baada ya Mzee Abeid Amani Karume na wazawa kushindwa kuvumilia unyanyasaji uliokuwa ukifanywa na Sultani. Mgawanyiko ulikuwa mkubwa kwa kiwango cha wazawa kukataa kununua bidhaa kwenye maduka ya Waarabu wakitumia msemo wa ‘gozi zuia pesa’. Ni unyanyasaji huo uliowafanya Watanzania wa Zanzibar kuchukua majambia, mapanga na marungu kupindua serikali dhalimu.

 

Tunachokiangalia leo ni nia ya kufanya mapinduzi na iwapo Zanzibar leo iko huru kushinda wakati wa Sulutani. Hakika kwa miaka 49 Zanzibar imepiga hatua kubwa kimaendeleo. Idadi ya familia zenye huduma ya umeme na maji Zanzibar kwa asilimia ni kubwa zile za Tanganyika. Barabara za lami kwa Zanzibar zimetandaa maeneo mengi ukilinganisha na maeneo mengine ya Tanzania. Nyumba bora zimejengwa kuliko wakati wote wa historia ya Tanzania katika kipindi hiki cha miaka 49.

 

Hata hivyo, yamekuwapo maneno ya hapa na pale. Karafuu limekuwa zao ambalo soko lake halitabiliki. Utalii nao kuna nyakati baadhi ya Watanzania wakaazi wa Zanzibar wamekuwa wakiutia doa kwa kuzusha vurugu zisizo na kichwa wala miguu. Imani kali za kidini zinaonekana kupenyezwa na baadhi ya watu wenye kuitakia mabaya nchi yetu. Misimamo ya kidini imekuwa ikipewa kipaumbele kana kwamba inaongeza shibe kwa wanadamu, kumbe inahatarisha safari yetu ya ahera.

 

Tumeshuhudia ndani ya miaka michache iliyopita, baadhi ya Watanzania wakaazi wa Zanzibar, wenyewe wanajiita Wazanzibari wakitumia nguvu kubwa kujitambulisha na Zanzibar kuliko Tanzania. Hata Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Amani Abeid Karume, imeshiriki dhambi hii kwa kufanya mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar (1984) na kutamka kwenye Ibara ya Kwanza kuwa nchi hiyo imerejeshwa kwenye hadhi iliyokuwanayo mwaka 1964 kabla ya Muungano wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika.

 

Harakati zinazoendelea ni nyingi na zinatukumbusha maneno ya Mwalimu Julius Nyerere. Kwamba wale wanaodhani ni Wazanzibar (kwa ulevi tu wa madaraka), baada ya muda wakiishaitenga Zanzibar na Tanganyika watakuta kumbe si wote si Wazanzibari. Watakuja kuna Wazanzibari na Wazanzibara. Wakimaliza mgogoro huo, watakuja kuna Waunguja na Wapemba, kisha watajikuta kuna Wamakunduchi na Wangazija. Dhambi hii itaisambaratisha Zanzibar.

 

Watanzania yatupasa turejee katika malengo ya msingi ya Mapinduzi kuwa ni maendeleo kwa wote, umoja, amani, upendo na mshikamano. Tuwakatae wote wenye kuchochea machafuko. Mungu ibariki Zanzibar, Mungu ibariki Tanzania. Tunasema hongera Rais Dk. Ali Mohamed Shein na hongera Watanzania wakaazi wa Zanzibar.

 

Ends…

By Jamhuri