3-Waziri-wa-Ujenzi-John-Magufuli-kush-akitoa-taarifa-kwa-waandishi-wa-habari-hwapo-pichani-leoKamanda-MpingaKwa miaka mingi tulikosa kuisikia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyojaa matumaini.

Wiki iliyopita tuliisikia hotuba ya Rais akilihutubia Taifa kupitia Bunge.

Wananchi waliosikiliza, waliburudika, lakini wapo wanaotia shaka. Hilo ni jambo la kawaida.

Wanatia shaka wakirejea hotuba tamu kama hiyo iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete, Desemba 2005 katika ukumbi huo huo wa Bunge mjini Dodoma.

Wengi walioisikiliza walijawa matumaini makubwa na kuamini kuwa Tanzania mpya yenye “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania”, ilikuwa imewadia.

Miaka 10 baadaye, hotuba ile ya Rais Kikwete, ilionekana kama hadaa tu.

Sitaki kuwa mpiga ramli, lakini tutakuwa tukifanya makosa kumlinganisha Rais Magufuli, na Rais Kikwete.

Rais Kikwete, hakuwa na sababu ya kutumia nguvu nyingi kufikia malengo na ahadi alizowapa Watanzania kwa sababu kwenye kampeni zake ni kama hakuwa na mpinzani. Ushindi wa asilimia zaidi ya 80 alioupata mwaka 2005 si kama huu wa asilimia 58 alioupata Dk. Magufuli mwaka huu.

Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba Dk. Magufuli, anajua ana kazi kubwa ya kufanya ili kuzikonga nyoyo za wapigakura; na kwa sababu hiyo aweze kuomba na kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Kupungua kwa kura za mgombea wa CCM mwaka huu ni matokeo ya misingi mibovu ya uongozi wa Awamu ya Nne.

 

Pamoja na ukweli huo, hauondoi hofu ya wananchi waliyoipata wakati wa Rais Kikwete. Ndiyo maana wanaomtakia mema Rais Magufuli, hawasiti kumkumbusha kadri inavyowezekana kwamba ana deni kubwa kwa Watanzania.

Ana wajibu wa kuwathibitishia kuwa hotuba yake aliyoitoa bungeni ilitoka moyoni, na si hotuba ya kuandikiwa ambayo baadaye anaweza kusema “aliyosoma yalikuwa ya wasaidizi wake”.

Tangu awali niliamini kabisa kuwa Rais Magufuli, anajua anachokuja kuwafanyia Watanzania waliojawa matumaini makubwa.

Nilisema, na naamini Rais Magufuli, si mtu wa kusaka sifa; bali amesukumwa na dhamira yake ya kweli kuuwania urais ili awatumikie Watanzania.

Miaka yake 20 akiwa Waziri katika wizara tatu tofauti, ameweza kusafiri huku na kule nchini. Anazijua shida za Watanzania. Anajua wanataka nini, na hawataki nini. Anatambua kwa kina kabisa namna anavyoweza kuibadili nchi hii kimaendeleo.

Rais Magufuli, anajua Tanzania imejaliwa kuwa na kila kitu cha kutuwezesha kuwa wa kwanza kimaendeleo katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, na hata Kusini mwa Jangwa la Sahara. Tulichokosa kwa muda mrefu ni uongozi thabiti wenye kujali maslahi mapana ya nchi na wananchi wake.

Ametangaza vita ngumu dhidi ya watu hatari. Wauza dawa za kulevya, majangili, mafisadi, wahujumu uchumi, wakwepa kodi, wapenda safari na wahalifu wengine wengi, ni watu wenye uwezo mkubwa wa kimtandao. Wanaweza kulifanya lolote alimradi maslahi yao yadumu.

Vita hii ni ngumu, lakini si kwamba hatuwezi kuishinda. Waliojaribu, akiwamo Rais Kikwete, walishindwa kwa sababu, ama waliogopa, au waliamua kuwa sehemu ya matatizo.

Wenye akili waliposikia maneno ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akisema sasa wakwepa kodi wakuu watashughulikiwa kwa vile Serikali imeamua kumpa ushirikiano, maana ya sentesi hiyo ni kwamba mtangulizi wa Rais Magufuli, alikuwa tatizo.

Mitaani kuna maneno yanasemwa kwamba wafanyabiashara wakuu waliokubuhu kwenye ukwepaji kodi, ama walifanya hivyo kwa kushirikiana na familia ya Rais, au walifanya hivyo kwa kulitumia vibaya jina la kiongozi huyo.

Hawa wa karibuni kabisa wanaobadili majina ya kampuni zao wanatajwa kuwa na uhusiano wa karibu kabisa na Ikulu ya wakati huo.

Kuna kampuni za usafirishaji mafuta zinazotajwa kukwepa kodi kwa kutumia majina ya watoto wa marais waliotangulia. Haya yanazungumzwa mitaani. Si maneno ya porojo kwa sababu hakuna aliyejitokeza kuyakanusha kwa vielelezo.

Biashara ya dawa za kulevya inajulikana inafanywa na nani. Wakubwa wameshatajwa sana. Gazeti la JAMHURI tumeshachapisha hadi majina yao na ushahidi wa matukio yao, lakini hakuna hatua zozote za maana zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Nne.

Kitengo cha Dawa za Kulevya kinafanya kazi kubwa mno, lakini kazi hiyo imefifishwa na mamlaka za juu katika nchi hii. Kuna watuhumiwa wameachiwa kwa amri za watawala. Kuna kesi zimefutwa katika mazingira ya rushwa ya wazi. Kuna wahalifu katika biashara hiyo wanaolindwa na mfumo mzima wa Serikali na Mahakama. Haya yako wazi.

Tunapoyasema haya, tunayasema kwa nia njema, na si kwa sababu tunamchukia au kumwonea wivu Mheshimiwa Kikwete na familia yake.

Kiongozi wa nchi anaposema anawajua wafanyabiashara wa dawa za kulevya, na kwamba orodha yao anayo; lakini akaweza kung’atuka bila kuwashughulikia wauaji hao, wananchi hawawezi kumsema vizuri. Kuhoji udhaifu huo si kwamba anachukiwa.

Rais wa nchi anaposema ana majina ya majangili 40; lakini akaondoka madarakani bila kuwashughulikia, hawezi kusimama leo na kuonyesha uchungu kwa rasilimali za nchi yetu. Wananchi wanapohoji mambo haya, wana haki ya kufanya hivyo kwa sababu walimpa dhamana kubwa ya kulinda ustawi wa Taifa letu.

Hotuba ya Rais Magufuli, imefufua matumaini ya Watanzania kwa Serikali yao ambayo kwa miaka mingi yalipotea. Watu wanaoihama au wanaoisema vibaya CCM na Serikali yake, wanafanya hivyo kutokana na aina ya uongozi.

Rais Magufuli, ana kazi kubwa. Lakini kazi hiyo itakuwa kubwa zaidi endapo wananchi watamwacha mwenyewe aendelee kuhangaika na mambo yanayolikabili Taifa letu.

Wananchi wana mchango mkubwa sana katika kulibadili Taifa letu kutokana hali ilivyo sasa na kwenda kwenye hali nzuri zaidi kimaendeleo.

Tumeona kumbe kuna mambo yanawezekana kutendwa ndani ya muda mfupi. Nakumbuka wakati fulani Dk. Magufuli, akiwa Waziri wa Ujenzi ndiye aliyeasisi mpango wa ujenzi wa barabara wa design and build. Alichukua uamuzi huo kwa kuamini kuwa ili tuweze kwenda na kasi ya maendeleo ya dunia, hatuna budi kujenga barabara zetu kwa kasi kwa utaratibu huo badala ya ule wa wafadhili ambao upembuzi hadi ujenzi uliweza kudumu kwa miaka hata 15 au 20!

Hivyo hivyo, amethibitisha kwa vitendo kuwa tukiamua, zahanati, vituo vya afya na hospitali zote nchini zinaweza kuwa na vitanda na huduma nyingine kwa muda mfupi. Nani aliamini Muhimbili inaweza kupata vitanda 300 na magodoro kwa idadi hiyo ndani ya siku mbili?

Kasi hiyo hiyo ikielekezwa kwenye shule zetu, mwanafunzi gani wa Tanzania ya leo ataketi chini kwa sababu ya ukosefu wa madawati? Tanzania yenye misitu ya kila aina, watoto wetu kukaa chini ni jambo la fedheha.

Kwa kasi hii hii aliyoionyesha Rais Magufuli, kijiji au mtaa gani utasubiri fadhila za wawekezaji kujengewa vyoo? Kweli Tanzania inahitaji mfadhili wa kutupatia huduma ya mahali pa watoto wetu kujisaidia? Aibu iliyoje!

Mambo yameanza kubadilika. Tumuunge mkono Rais Magufuli, kwenye mapambano haya ya kuijenga Tanzania mpya. Amesisitiza tudai stakabadhi kila tunaponunua bidhaa. Tufanye hivyo sasa. Kuendelea kulalama tu bila kuchukua hatua za kuiunga mkono Serikali yetu kwa mambo ya msingi, si kuitendea haki.

Kabla ya mwezi mmoja kumalizika, tayari kuna mambo mazuri yameanza kuonekana. Inawezekana kabisa katika kipindi cha miezi sita ijayo Tanzania itakuwa nyingine kimaendeleo.

Rais Magufuli, sasa ana kazi ya kuunda Baraza la Mawaziri. Aunde Baraza bila kushinikizwa. Aweke wachapakazi hodari watakaomsaidia.

Wapo waliohudumu kwenye mabaraza yaliyopita. Sasa wanajitahidi kweli kweli kuona wakirejeshwa. Anajua aina ya utendaji kazi wao. Wamo wachapakazi hodari, lakini wengine bure tu. Wapo walioondolewa kwa sababu ya majungu, lakini wanafaa sana. Aunde Baraza kulingana na mahitaji ya nchi yetu.

Kama nilivyoahidi katika safu hii, kazi yetu ni kuendelea kukusaidia kwa kukupatia  taarifa zitakazokusaidia kunyoosha mambo. Rais ajitahidi kujenga mfumo imara ili hata atakapoondoka madarakani,  mambo yajiendeshe kwa mfumo usioyumba. Mungu akubariki.

1706 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!