*Atoboa siri majaji wengi ‘vihiyo’, washindwa kuandika hukumu

*Aeleza namna wakuu wa wilaya walivyoteuliwa kwa rushwa

*Yumo mwingine aliyehukumiwa kwa ubaguzi wa ukabila

Ifuatayo ni sehemu ya maoni ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, kuhusu Mpango wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha wa 2012/2013. Lissu alitoa maoni haya na kwa kiasi fulani yaliibua mjadala mkali bungeni, huku Serikali ikitaka aondoe baadhi ya maneno, na yeye akakataa. Endelea…

UTEUZI WA MAJAJI

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua ukweli kwamba Rais Kikwete ameteua majaji wengi wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano kuliko marais wengine wote waliomtangulia kwa ujumla wao. Rekodi hii peke yake inaonyesha kwamba Rais anatambua umuhimu wa Mahakama Kuu kuwa na watendaji wa kutosha wa utoaji haki ili kutekeleza dira ya ‘haki kwa wote na kwa wakati.’

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kuteua majaji wengi ni jambo moja. Kuteua majaji wengi wenye uwezo, ujuzi na wanaofaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu ni jambo jingine kabisa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitishwa na dalili zinazoanza kuonekana wazi kwamba baadhi ya majaji walioteuliwa na Rais hawana uwezo, ujuzi na/au hawakufaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji ya Mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa ibara ya 109(6) ya Katiba, mtu anaweza kuteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu ikiwa ana ‘sifa maalumu’, na amekuwa na mojawapo ya sifa maalumu kwa muda usiopungua miaka 10. Sifa hizo, kwa mujibu wa ibara ndogo ya (7), maana yake “ni mtu aliye na shahada ya sheria kutoka chuo kikuu kinachotambuliwa na mamlaka ya ithibati Tanzania, na amekuwa hakimu; amefanya kazi katika utumishi wa umma akiwa na sifa za kufanya kazi ya uwakili au ni wakili wa kujitegemea; ana sifa ya kusajiliwa wakili, na amekuwa na sifa hizo mfululizo kwa muda usiopungua miaka 10.”

Sharti la kuwa na sifa hizo kwa miaka 10 mfululizo linaweza kutenguliwa endapo Rais – baada ya kushauriana na Tume ya Utumishi wa Mahakama – atatosheka kwamba mhusika ana uwezo, ujuzi na kwa kila hali anafaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu na kuna sababu za kumfanya mtu huyo astahili kukabidhiwa madaraka hayo (ibara ya 109(8).

Tume ya Utumishi wa Mahakama inaundwa na Jaji Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufaa atakayeteuliwa na Rais kwa kushauriana na Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi na wajumbe wawili watakaoteuliwa na Rais. Jukumu la kwanza la Tume hii, kufuatana na ibara ya 113(1) (a), ni “kumshauri Rais kuhusu uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu.”

Ni wazi kwamba utaratibu huu wa uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu ulilenga kumwezesha Rais – ambaye si lazima awe mwanasheria na/au mwenye ufahamu wa masuala ya kisheria – kuteua majaji baada ya kupata ushauri kutoka kwa viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania na pia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye anawajibika kikatiba “… kutoa ushauri kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusu mambo yote ya kisheria….” (ibara ya 59(3).

Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Rais hana mamlaka ya kufanya uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu nje ya utaratibu huu uliowekwa na Katiba. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina taarifa kwamba utaratibu huu wa kuteua majaji umeachwa kufuatwa.

Kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo, sasa watu wanateuliwa kuwa majaji wa Mahakama Kuu ambao hawajawahi kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na – kwa sababu hiyo – hawajafanyiwa vetting yoyote na mamlaka hiyo ya kikatiba juu ya uwezo na ujuzi wao na kama ‘wanafaa kwa kila hali kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu.’

Inaelekea watu hao – wengi wao wakiwa wamekaribia muda wao wa kustaafu kwingineko katika utumishi wa umma – wanapewa ‘zawadi’ ya ujaji ili kuwawezesha kupata mafao ya majaji wastaafu ambayo yameboreshwa sana katika miaka ya karibuni. Matokeo yake ni kuwa na majaji ambao wamechoka na hawawezi au hawajui namna ya kufanya kazi ya Jaji wa Mahakama Kuu.

Madhara ya kukiuka utaratibu huu wa kikatiba wa uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu ni makubwa na yameanza kujitokeza wazi. Kwanza, wapo majaji ambao – kwa sababu ya kutokufanyiwa vetting na Tume ya Utumishi wa Mahakama – hawana uwezo wa kuandika mwenendo wa mashauri na hukumu zinazosomeka kwa sababu ya, ama kutokuwa na uwezo na ujuzi wa sheria, au kutokuwa na weledi wa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha rasmi ya mwenendo wa mashauri na hukumu.

Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kwamba wapo majaji ambao – kwa sababu hizo hizo za kutokufanyiwa vetting juu ya uwezo na ujuzi wao na mamlaka husika ya kikatiba – wameshindwa kabisa kuandika hukumu za kesi walizozisikiliza na hivyo kusababisha mrundikano wa kesi mahakamani usiokuwa na sababu yoyote ya msingi.

Kazi ya Jaji wa Mahakama Kuu, kama ilivyo kazi ya mawakili na wanasheria kwa ujumla, ni kazi ya kisomi. Ni kazi inayohitaji watu wenye uwezo mkubwa kitaaluma na utafiti, weledi wa uchambuzi (analytical skills) na wa kuandika na kuzungumza kwa lugha ya kimombo fasaha. Watu hawa hawaitwi ‘wanasheria wasomi’ kama mapambo tu. Wanatakiwa kuwa wasomi kweli kweli.

Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuwa na majaji wasiokuwa na sifa hizi si tu kunafifisha utoaji wa haki kwa wadaawa katika mashauri yaliyoko mahakamani, bali pia kunaifedhehesha taaluma nzima ya sheria, Mahakama ya Tanzania na mamlaka yao ya uteuzi, yaani Rais mwenyewe. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe ufafanuzi juu ya jambo hili na pia itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu kwamba utaratibu wa uteuzi wa majaji uliowekwa na Katiba utaheshimiwa, kwa Rais kuteua majaji watakaotokana na ushauri wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ili kuondokana na aibu na fedheha hii ya kuwa na majaji wasiojua wanachotakiwa kufanya.

MIKOA NA WILAYA MPYA

Mfumo wetu wa tawala za mikoa na wilaya umefafanuliwa katika ibara 2(2) na 61 za Katiba na katika Sheria ya Tawala za Mikoa, Sura 189 ya Sheria za Tanzania. Mfumo huu ulirithiwa kutoka mfumo wa dola la kikoloni uliokuwa umeangikwa kwenye majimbo na wilaya. Mabadiliko ya mwaka 1962 yaliyofuta majimbo kuanzisha mikoa hayakuwa mabadiliko ya mfumo, bali yalikuwa ni kugawa majimbo – yaliyokuwa makubwa kijiografia – kwenda mikoa iliyokuwa midogo kieneo.

Mambo mengine yote ya kimfumo, kwa mfano, mamlaka ya kugawa maeneo katika majimbo na wilaya na ya kuteua wakuu wa maeneo hayo hayakubadilishwa kimsingi, bali yalihamishwa kutoka kwa gavana wa kikoloni kwenda kwa Rais. Katika mfumo huo wa kikoloni, wananchi hawakushirikishwa kwa namna yoyote katika uamuzi wa kugawa maeneo kuwa majimbo na wilaya.

Dola la uhuru halijabadilisha mfumo huo kwa namna yoyote ya maana hata baada ya nusu karne ya Uhuru. Kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni, wananchi ambao ibara ya 8(1) (a) ya Katiba inadai kwamba ‘ndiyo msingi wa mamlaka yote’, wameendelea kutegemea karama za watawala za kutengewa mikoa au wilaya mpya. Vile vile, malengo ya kuteua wakuu wa maeneo haya nayo hayajabadilika sana.

Wakati ambako wengi wa wakuu wa majimbo na wilaya wa kikoloni walikuwa maafisa wa kijeshi walioshiriki katika vita mbalimbali za kikoloni na kwa hiyo lengo la uteuzi wao, lilikuwa ni kudhibiti wananchi kwa manufaa ya kiuchumi ya kikoloni; wengi wa wakuu wa mikoa na wilaya wa Tanzania ya leo ni makada wa CCM. Mamlaka ya watu hawa hayatokani na wananchi, kwani hawachaguliwi na mtu yeyote; na kwa sababu hizo hizo, hawawajibiki kwa wananchi kwa utekelezaji wa kazi na majukumu yao.

Aidha, kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni, wengi wao bado ni wanajeshi. Kwa vyovyote vile, lengo la uteuzi wa wakuu hawa wa wilaya ni kudhibiti wananchi – na katika zama hizi za vyama vingi vya siasa, vyama vya upinzani – kwa manufaa ya CCM. Hii inathibitishwa na matakwa ya Katiba ya CCM yenyewe.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Rais Kikwete – kwa kutumia mamlaka yake chini ya ibara ya 2(2) ya Katiba – amegawa mikoa mipya ya Geita, Katavi, Njombe na Simiyu. Aidha, kwa kutumia mamlaka hayo hayo, Rais Kikwete amegawa wilaya mpya za Chemba katika Mkoa wa Dodoma; Mbogwe katika Mkoa mpya wa Geita; Mlele katika Mkoa mpya wa Katavi; Buhigwe, Kakonko na Uvinza katika Mkoa wa Kigoma; Butiama katika Mkoa wa Mara; Momba katika Mkoa wa Mbeya; Wanging’ombe katika Mkoa mpya wa Njombe; Nyasa katika Mkoa wa Ruvuma; Busega na Itilima katika Mkoa mpya wa Simiyu; Ikungi na Mkalama katika Mkoa wa Singida na Kaliua katika Mkoa wa Tabora.

Sambamba na ugawaji wa mikoa na wilaya mpya, Rais Kikwete pia aliteua wakuu wapya wa mikoa na wilaya husika.

WAKUU WA WILAYA NA CCM

Wakuu wa mikoa na wilaya wote ni, na wanatakiwa kuwa wanachama wa CCM. Hii ni kwa sababu, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977, wakuu wa wilaya wamekuwa ni wajumbe wa vikao vyote vikuu vya CCM katika ngazi ya wilaya. Kwa mfano, kwa mujibu wa Katiba ya CCM Toleo la 1982, Mkuu wa Wilaya ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya (ibara ya 42(3); ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya (ibara ya 44(3); na ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Wilaya (ibara ya 46(3).

Hata baada ya miaka 30 tangu toleo hilo la Katiba ya CCM litolewe, na licha ya miaka 20 ya mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, hali bado iko vile vile kuhusiana na nafasi ya wakuu wa wilaya katika vikao rasmi vya CCM. Ndiyo maana, kwa mujibu wa ibara ya 76(1)(c) ya Katiba ya CCM Toleo la 2010, Mkuu wa Wilaya ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wa Wilaya; ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya (ibara ya 78(1)(c); na ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya (ibara ya 80(1)(c).

Kuna ushahidi wa kutosha kwamba kugawa mikoa na wilaya ni namna tu ya kupata fursa ya kuwapatia makada wa CCM – ambao kwa sababu mbalimbali wamekosa – nyadhifa na marupurupu serikalini kwa kuwateua kuwa wakuu wa mikoa na wa wilaya. Uthibitisho wa kauli hii ni uteuzi wa wakuu wapya wa mikoa na wilaya uliofanywa katika siku za karibuni na Rais Kikwete.

Katika uteuzi huo, kati ya wakuu wa mikoa wapya, wawili ni wabunge wa Viti Maalumu katika Bunge hili hili. Aidha, kati ya wakuu wapya wa wilaya, watano ni wabunge wa Viti Maalumu katika Bunge hili hili; 15 ni waliowahi kuwa wabunge au wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki; na 22 waligombea ubunge, lakini wakashindwa kwenye hatua za kura za maoni za ndani CCM au kwenye Uchaguzi Mkuu.

Aidha, Mheshimiwa Spika, katika hali inayoonyesha kukithiri kwa matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma, wabunge wa Viti Maalumu walioteuliwa kuwa wakuu wa mikoa na wilaya wameendelea kushiriki katika vikao vinavyoendelea vya Bunge hili tukufu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu hawa wakuu wa mikoa na wilaya wabunge wanalipwa mshahara upi wanapokuwa bungeni?

Aidha, Serikali itoe kauli ni kwa nini watu hawa wanaendelea kuja bungeni kuhudhuria vikao vya Bunge wakati wameshakubali uteuzi wao kama wakuu wa mikoa au wilaya? Vilevile, Serikali ilieleze Bunge hili watu hawa wanamwachia nani majukumu yao ya ukuu wa wilaya wao wanapokuja bungeni na kwa nini iwe hivyo? Zaidi ya hayo, kwa vile ibara ya 67(2) (g) ya Katiba inamwondolea mtu sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge “… ikiwa mtu huyo ameshika madaraka ya afisa mwandamizi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano…”,

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama wabunge wote walioteuliwa kuwa wakuu wa mikoa au wilaya bado wana sifa za kuendelea kuwa wabunge.

WAKUU WA WILAYA WANAJESHI

Kuna utata mkubwa wa kikatiba kuhusiana na baadhi ya wateuliwa wa ukuu wa mikoa na wilaya. Kwanza, orodha ya wakuu wapya wa mikoa na wilaya walioteuliwa na Rais Kikwete inaonyesha kuwapo pia wanajeshi wanane, ambao kati yao watatu wanatajwa kuwa maafisa wastaafu wa Jeshi. Watano waliobaki hawatajwi kama wastaafu na kwa hiyo inaelekea bado wako katika utumishi wa jeshi. Kama tulivyokwisha kusema katika maoni yetu, wakuu wa mikoa na wilaya wanatakiwa kuwa wanachama wa CCM na wajumbe wa vikao vyote vikuu vya chama hicho katika mikoa na wilaya.

Wakati jambo hili linaweza lisizue mshangao katika mazingira mengine, kuwateua wanajeshi kuwa wakuu wa mikoa na/au wilaya katika mazingira ya sasa ya kisiasa, ambapo wanatakiwa wawe wanachama wa CCM na wahudhurie vikao vya uamuzi vya chama hicho ni jambo lenye mgogoro mkubwa kikatiba. Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa ibara ya 147(3) ya Katiba, “itakuwa ni marufuku kwa mwanajeshi yeyote kujiunga na chama chochote cha siasa…”

Ibara ya 147(4) inatafsiri ‘mwanajeshi’ kuwa “… ni askari aliyeajiriwa kwa masharti ya muda au ya kudumu katika Jeshi la Ulinzi, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza au Jeshi la Kujenga Taifa.” Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama wakuu wapya wa mikoa ya Kagera, Wilaya za Kakonko, Kalambo, Kyerwa, Misenyi na Mlele ni ‘wanajeshi’ au walikwisha kustaafu ili Bunge hili tukufu lifahamu kama uanajeshi wao, ukuu wao wa wilaya u-CCM wao vinaendana na matakwa ya Katiba ya nchi yetu.

KUENDEKEZA RUSHWA NA UFISADI

Uteuzi wa baadhi ya wakuu wapya wa wilaya unaashiria kukithiri kwa rushwa na ufisadi na kukosekana kwa maadili kwa mamlaka ya uteuzi. Hapa, Mheshimiwa Spika, tutatumia mifano ya wakuu wa Wilaya ya Kishapu katika Mkoa wa Shinyanga, na Mbarali mkoani Mbeya. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Wilson Elisha Nkhambaku, ambaye ndiye Mkuu mpya wa Wilaya ya Kishapu, aliteuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa mgombea wake wa ubunge katika Jimbo la Singida Magharibi.

Licha ya kuwekewa pingamizi dhidi ya uteuzi na aliyekuwa mgombea wa CCM, Bwana Nkhambaku alifanikiwa kuteuliwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Singida Magharibi kuwa mgombea ubunge wa Chadema katika Jimbo hilo. Hata hivyo, muda mfupi baada ya kampeni za uchaguzi kuanza rasmi, Bwana Nkhambaku alionekana katika mkutano wa kampeni za uchaguzi wa CCM katika Jimbo la Kibaha Vijijini uliohutubiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM Yusuf Makamba na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Lazaro Nyalandu.

Katika mkutano huo, Bwana Nkhambaku alitangaza kwamba amejitoa kwenye kugombea ubunge wa Jimbo la Singida Magharibi kwa tiketi ya Chadema na kwamba alikwisharudi CCM!

Kifungu cha 48 cha Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343 ya Sheria za Tanzania kinaruhusu mgombea ubunge yeyote aliyeteuliwa na Msimamizi wa Uchaguzi kujitoa katika kugombea uchaguzi husika. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kifungu cha 91B cha Sheria hiyo kinatamka wazi kwamba ni kosa la jinai ya rushwa ya uchaguzi kumrubuni au kumshawishi mgombea kujitoa kugombea kwa malipo, au ahadi ya malipo. Kwa mujibu wa kifungu hicho, adhabu ya kosa hilo ni kifungo kisichozidi miaka mitano jela.

Aidha, Mheshimiwa Spika, kifungu cha 21(1)(b) cha Sheria ya Gharama za Uchaguzi, 2010 kinakataza mtu yeyote, moja kwa moja au kwa namna nyingine yoyote, yeye mwenyewe, wakala wake au kupitia chama chake cha siasa, kwa niaba yake kutoa au kusaidia kutoa au kumpatia wadhifa au sehemu ya ajira mpiga kura au mtu mwingine yeyote kwa nia ya kumshawishi mpiga kura huyo kuacha kupiga kura au kumrubuni kutenda kitendo hicho.

Vile vile, kifungu cha 21(1)(f) cha Sheria hiyo kinatamka kwamba ni rushwa ya uchaguzi kwa kila mpiga kura ambaye amepokea au amekubali kupokea wadhifa, sehemu au ajira kwa ajili yake mwenyewe kwa ajili ya kuacha kupiga kura wakati wowote wa uchaguzi. Kwa mujibu wa kifungu cha 94 cha Sheria ya Uchaguzi, makosa haya mawili ya jinai yana adhabu ya faini isiyopungua shilingi laki tano au kifungo cha kati ya mwaka mmoja hadi mitatu jela au vyote viwili kwa pamoja.

Hoja hapa, Mheshimiwa Spika, ni kwamba uteuzi wa Wilson Elisha Nkhambaku kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu ni ushahidi wa wazi wa rushwa ya uchaguzi. Ni wazi kwamba mtu huyo alirubuniwa au kushawishiwa kujitoa kugombea ubunge kwa niaba ya Chadema. Hilo lilikuwa kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu cha 91B cha Sheria ya Uchaguzi.

Sasa mtu huyo amepewa wadhifa wa Mkuu wa Wilaya. Nalo ni kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu cha 21(1)(b) na (f) cha Sheria ya Gharama za Uchaguzi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama ni sera ya Serikali hii ya CCM kuhonga wagombea wa vyama vingine kwa kuwapa nyadhifa katika utumishi wa umma ili wajitoe kama wagombea wa vyama vyao. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi bungeni kama mtu aliyepokea rushwa ya wadhifa ili ajitoe kuwa mgombea ubunge anastahili kupewa wadhifa wa Mkuu wa Wilaya au wadhifa mwingine wowote katika utumishi wa umma.

KUENDEKEZA SIASA ZA KIBAGUZI

Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni imeshangazwa na kusikitishwa sana na uteuzi wa Bwana Kifu Gulamhussein Kifu kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali. Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, Bwana Gulamhussein Kifu alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini. Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi wake yalipingwa katika Mahakama Kuu na baadaye katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Mnamo tarehe 18 Juni 2002, Mahakama ya Rufani ya Tanzania katika Shauri la Rufaa Na. 2 la 2002 katika Manju Salum Msambya dhidi ya Mwanasheria Mkuu na Kifu Gulamhussein Kifu, ilifuta matokeo ya uchaguzi wa Bwana Gulamhussein Kifu kwa sababu Mahakama ya Rufani ilithibitisha kwamba mtu huyo alifanya kampeni kwa misingi ya ukabila.

Mahakama ya Rufani ilinukuu kauli ifuatayo ya Bwana Gulamhussein Kifu wakati wa kampeni za uchaguzi huo: “… Waha wenzangu tuelewe kwamba mwaka huu ni mwaka wetu kujikomboa. Tumetawaliwa na kabila la Wabembe kwa muda mrefu. Kabila la Wabembe tunajua ni watu wa Kongo siyo wa Tanzania. Ni ajabu Waha tulio wengi katika jimbo hili tuendelee kutawaliwa na kabila chache. Muha popote alipo ahakikishe anipigie mimi Muha mwenzie. Angalieni wanakuja watu huku. Yuko mtu aliyepandikizwa na Msambya. Huyu mtu anakuja na Kabourou…. Kabourou na Msambya wote ni damu ya Kongo, wote ni Wanyakumawe.

Katika mkutano mwingine wa kampeni, Mahakama ya Rufani ilithibitisha kwamba Bwana Gulamhussein alitamka maneno yafuatayo: “Tumetawaliwa na wageni kwa muda mrefu … umefika wakati wa kujikomboa kutoka kwa wageni kutoka Kongo…. Ni wakati mzuri kunichagua mimi kama Muha, Muha mwenzenu … kwa kuwa sisi ndiyo tulio wengi katika jimbo hili.” Sasa mtu huyu aliyepatikana na hatia ya kufanya siasa za kibaguzi za aina hii ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kwamba uteuzi wa Bwana Gulamhussein Kifu uko sambamba na matakwa ya Katiba yetu inayopinga aina zote za kibaguzi.

‘KUSOGEZA MAENDELEO KWA WANANCHI’?

Kuna dhana imejengwa na kuaminishwa kwa wananchi kwa miaka kwamba lengo la kugawa mikoa au wilaya mpya ni “… kusogeza na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi”, na kwa hiyo inaonekana kama jambo jema. Ndiyo maana suala la kutenga maeneo katika wilaya au mikoa mipya limejitokeza sana katika chaguzi za miaka ya karibuni kama sehemu ya ahadi za kampeni wagombea urais wa CCM.

Dhana hii haina budi kuhojiwa na ukweli wake, kama upo, kuthibitishwa. Kwanza, nchi zote jirani na Tanzania ambazo zina mikoa au majimbo machache zaidi yetu hazina tofauti kubwa ya kimaendeleo na nchi yetu. Nyingine kama Kenya, kwa mfano, yenye majimbo 11 na ambayo sehemu yake kubwa ya kaskazini na kaskazini mashariki ni nusu jangwa ina uchumi mkubwa kuliko wa Tanzania ambayo sasa ina mikoa ishirini na saba.

Pili, hakuna ushahidi wa kuthibitisha kwamba kugawa mikoa au wilaya mpya kunaongeza bajeti ya maendeleo ya maeneo husika hasa hasa katika miradi ambayo ina umuhimu kiuchumi au kijamii kwa wananchi. Badala yake, ushahidi uliopo unaonyesha kwamba gharama za uendeshaji wa Serikali – yaani bajeti ya matumizi ya kawaida – zinaongezeka pale ambapo mikoa na wilaya mpya zinapotengwa.

Kwa mfano, kwa mujibu wa Juzuu ya III Makadirio ya Matumizi ya Kawaida ya Mikoa kwa mwaka huu wa fedha 2012/2013, bajeti ya matumizi ya kawaida ya mikoa katika mwaka wa fedha 2010/2011 ilikuwa shilingi trilioni 1.887 na shilingi trilioni 2.321 katika mwaka wa fedha 2011/2012. Hii ilikuwa kabla ya kuongezwa kwa mikoa minne mipya na wilaya mpya kumi na tisa.

Hata hivyo, baada ya kuongezwa kwa mikoa mipya minne, bajeti ya matumizi ya kawaida ya mikoa katika mwaka huu wa fedha imepanda hadi kufikia shilingi trilioni 2.882. Hii ndiyo kusema kwamba katika kipindi cha miaka miwili 2010/2011 – 2012/2013, bajeti ya matumizi ya kawaida imeongezeka kwa takriban asilimia 53. Kwa mujibu wa makadirio haya, bajeti ya matumizi ya kawaida ya mikoa mipya minne ya Geita, Katavi, Njombe na Simiyu ni shilingi bilioni 257.443 kwa mwaka huu peke yake.

Kwa upande mwingine, bajeti ya matumizi ya kawaida ya wilaya kumi na tano zilizotajwa hapo juu ni shilingi bilioni 2.502 kwa mwaka huu wa fedha. Kwa hiyo, kwa mujibu wa makadirio haya, gharama za kuendesha Serikali katika maeneo haya mapya kwa mwaka huu wa fedha peke yake ni takriban shilingi bilioni 260.

Kwa ulinganisho, kwa mujibu wa Juzuu ya IV Makadirio ya Matumizi ya Miradi ya Maendeleo kwa Wizara na Mikoa kwa mwaka huu wa fedha inaonyesha kwamba bajeti ya maendeleo kwa ajili ya mikoa mipya minne iliyogawanywa mwaka huu ni shilingi bilioni 60.021. Hii ni sawa na asilimia 23.3 ya bajeti ya matumizi ya kawaida kwa kipindi hicho hicho. Makadirio haya hayaonyeshi fedha yoyote iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika wilaya mpya 19 zilizoanzishwa.

Kwa ushahidi huu, Mheshimiwa Spika, dhana kwamba kutenga mikoa na wilaya mpya ni kusogeza maendeleo kwa wananchi ni kivuli cha kisiasa tu chenye lengo la kuhalalisha ongezeko la matumizi ya watawala. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba wakati umefika kwa nchi yetu kuweka utaratibu wa kikatiba na kisheria utakaodhibiti – kama si kupunguza – ongezeko la maeneo ya kiutawala ambayo si tu ni mzigo kwa walipa kodi, bali ni mzigo kwa uchumi kwa ujumla kwani yanatumia rasilimali ambazo zingeelekezwa katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

 

 

By Jamhuri