Ombi langu la tatu, ni kwa watumiaji wote tujiepushe na matumizi mabaya ya kwenye barabara ikiwa ni pamoja na kumwaga oil, kuchimba michanga kwenye madaraja, kung’oa alama za barabarani, hasa sisi ndugu zangu Wasukuma na mimi ni Msukuma, zile alama ‘reflector’ huwa tunaziiba kwa kuziweka kwenye baiskeli zetu.

Huu ni uvunjaji wa Sheria namba 7 ya mwaka 2013. Niwaombe msing’oe hata zile nati zilizofunga madaraja yale, kwa ajili ya kupeleka kwenye tela za ng’ombe.

Mimi ni mfugaji pia ninafahamu, usifungue nati ya kwenye daraja. Ukishafungua likija gari kutoka kule halitajua kama nati za pale zimefunguliwa, daraja linaanguka unaua watu. Ni lazima tuheshimu alama za barabarani, tuheshimu mali zote za barabarani kwa faida ya Watanzania wote. Tusiwe wabinafsi.

Lakini hii barabara inatakiwa idumu kwa miaka mingi, ili fedha zilizotumika hapa kama bilioni 90 Wasukuma wanasema ‘Value for money’ iweze kuonekana. Kwa hiyo, mnawajibika ndugu zangu wanaSimiyu, wanaBariadi kuitunza barabara hii.

Serikali imetimiza wajibu wake kwa kutengeneza hizi kilometa 71.8 kwa fedha zake, hizi fedha zimechangiwa na Watanzania wote, wa Kigoma wamechangia hapa, wa Musoma wamechangia hapa, wa Kilimanjaro wamechangia hapa, wa Dar es Salaam wamechangia hapa, wa Chato wamechangia hapa, wa Musoma wamechangia hapa ili kusudi ninyi watu wa Bariadi mpate barabara. Muitunze. Bariadi oyee, Simiyu oyee…

Tutakapoitunza hii barabara itadumu kwa muda mrefu na hizo fedha zingine kama nilivyotoa maagizo kwenye wizara inayohusika, nitatangaza tenda ndani ya wiki moja wiki mbili hata mwezi wataandaa zile ‘documents’ ili barabara iliyobaki pale nayo ianze kutengenezwa.

Nitoe wito, mahali itakapopita barabara, wale ambao wako ndani ya mita 22.5 kila upande waanze kuondoa majengo yao. Ninajua ninyi mnaweza msifurahi sana, lakini ni lazima niwaeleze ukweli. Hii ni kwa mujibu wa Sheria namba 7 ya mwaka 2003.

Msije mkachelewesha mradi huu wa barabara. Watu wa Simiyu wanahitaji barabara kuliko nyumba moja aliyokaa ndani ya ‘road reserve’ au mnasemaje niache kujenga kwa sababu ya nyumba mbili zimekaa kwenye road reserve? Wangapi wanataka tuendelee kujenga?  Wenye nyumba mmesikia, Simiyu oyee…

Tunataka Simiyu iwe mpya, na mimi ninavyoiona Simiyu hii kwa kweli mnaenda speed nzuri hongereni sana. Na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ninakupongeza, mimi niko mgumu sana kupongeza watu, lakini unavyoenda, unaenda vizuri. Ninaomba wakuu wa mikoa wengine waige pia mfano wako.

Wewe umepanga kila wilaya kuna kitu cha kufanya, Maswa kuna kiwanda cha chaki, wapi kuna kiwanda sijui cha maziwa, huu ni utaratibu mzuri na hivyo wewe umeanza kutekeleza serikali ya viwanda kwa vitendo. Ukishafanya hivyo umetengeneza ajira za Watanzania na hicho ndicho tunachokitaka.

Jukumu la Serikali ndugu zangu wanaSimiyu ni kutengeneza miundombinu, tukishatengeneza barabara tumewasaidia Watanzania maskini. Tukishaleta umeme tumewasaidia Watanzania maskini, tukishaleta hospitali tumewasaidia Watanzania maskini, tukishaleta maji tumewasaidia Watanzania maskini, jukumu la Serikali si kuleta chakula. Kwa sababu Serikali haina shamba la kulima. Ni lazima niwaambie ukweli, na ukweli utabaki kuwa ukweli. Na kwenye maandiko Baba Askofu yuko hapa wanasema ‘na asiyefanya kazi na asile’, maana yake asipokula si afe? 

Kwa hiyo, niwaombe Watanzania tufanye kazi, na ninafahamu katika maeneo haya kuna maeneo ya Tanzania baadhi mvua huwa zinachelewachelewa na kuna maeneo mvua zimenyesha hazikutosha. Ni lzima sasa sisi Watanzania na wakulima tujipange namna ya kufanya akili na mvua. Tumezoea kulima mahindi, mahindi yanahitaji maji mengi. 

Kwa hiyo, badala ya kulima mahindi ambayo yatahitaji miezi sita, saba ndipo yazae, lima mtama, lima ulezi, lima viazi, lima matikiti maji utauza utanunua, lima mpunga kwenye majaruba kama mvua zitanyesha. Huo ndiyo wito wangu kwenu.

Ninafahamu wapo wanasiasa wengi, wachache ambao hao wanafikiri mzee bure hajatoka kichwani mwao. Kila kitu kikitokea Serikali fanya hii, kila kitu kikitokea Serikali fanya hii. 

Serikali ninayoiongoza mimi haitatoa kila kitu, mlinichagua niwaambie ukweli na ni lazima niseme ukweli. Kwa hiyo, niwaombe ndugu zangu; mfanye kazi. Wapo watu nimeangalia kwenye njia, wapo watu pale nimepita nimekuta vitunguu vimelimwa vingi sana na nyanya. Lakini katika shamba hilo hilo la vitunguu na nyanya ambapo nyanya zimestawi vizuri, katika Jimbo la Busega pale wapo wengine ambao wamelima mahindi ambayo yamekauka, ni kando kando ya ziwa. 

Ameshindwa hata kwenda kuchota tu ndoo (anaongea Kisukuma) anataka serikali imletee chakula, sileti chakula. Nasema sileti chakula.

Lakini ninafahamu, wapo wafanyabiashara wengine wachache waliokuwa ‘wamezoea’, nasema waliokuwa wamezoea panapotokea matatizo kidogo tu ya ukame wanatumia vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na magazeti wanayoyaamini wao, sio magazeti yote pamoja na baadhi ya wanasiasa kuzungumza Tanzania kuna njaa.

Lakini lengo lao wameleta mahindi ambayo yana quality ya hovyo kutoka Brazil wanataka wasamehewe kodi wayauze Tanzania ikose kodi. Yuko mmoja ana tani 21,000 Dar es Salaam, nimemwambia tunazikata kodi kama kawaida.

Nataka niwaeleze huo ndiyo mchezo wao, andikeni kuna njaa, andikeni nini nini nini. Anayejua njaa ni Rais, wala sio gazeti fulani.

Mimi ndiyo nimepewa dhamana ya kuwaongoza Watanzania wote, nikamsikia mtu mmoja kule Mvomero naye walimlipa hela akazungumza kuna ng’ombe 17,000 wamekufa. Ati wamekosa maji na majani! 

Wewe ng’ombe 17,000 wamekosa maji na majani …. (anaongea Kisukuma) inakufa ya kwanza, inakufa ya pili umeangalia tu, inakufa ya tatu umeangalia tu. Kwanini usikodi gari ukapeleka kwenye mnada ng’ombe 1,000 ukapata pesa?  

Lakini mtu anazungumza mpaka povu linamtoka. Zimekufa ng’ombe 17,000. Elfu kumi na saba ng’ombe? Inakufa ya kwanza umeangalia tu, inakufa ya pili imekosa maji wewe umeangalia tu.  Zinafika mpaka 20 zimekosa maji umeangalia tu, mpaka 30, mpaka 100, mpaka 1,000, mpaka 17,000 wakati magari masemitrela yapo hapo? Si nenda ukazibebe ukauze.

 

>>ITAENDELEA

By Jamhuri