21101.Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya njema na kutuwezesha kutekeleza makujumu yetu vizuri ya Mkutano wa kwanza wa Bunge la kumi na moja ulioanza terehe 17 Novemba, 2015.Nimefarijika  kuwa  kazi  zote zilizopangwa katika ratiba yetu tumezikamilisha kwa muda mfupi na kwa umahiri mkubwa.

2.Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii ya awali kukupongeza wewe binafsi,kwanza kwa kuchaguliwa na Wananchi wa Jimbo la Kongwa kuwa mbunge wao na pili, kwa kuchaguliwa  kwa kura nyingi za kishindo kuwa Spika wa Bunge la kumi na moja (11) la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nina imani utaliongoza Bunge hili Tukufu na kukidhi kiu ya Watanzania ya kutaka Bunge hili litekeleze majukumu yake kwa weledi na umakini mkubwa wa kuwawezesha kupata maendeleo endelevu.

3.Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu hii fupi napenda kutumia nafasi hii kumshukuru tena Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa imani kubwa aliyoionyesha kwangu kwa kuniteua kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .Namwombea  Mungu ambariki na kumjali afya njema  na nguvu ya kuwatumikia Watanzania. Aidha, naomba niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kunithibitisha kuwa Waziri Mkuu wa Kumi na Moja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kura nyingi hapa Bungeni.

4. Vilevile, nawashukuru Wananchi wote wa Jimbo la Ruangwa kwa kuwa na imani nami na kunichagua kuwa mwakilishi wao.Napenda kukishukuru change change Chama Cha Mapinduzi kwa kuniteua kugombea Ubunge katika jimbo la Ruangwa na kushiriki katika kampeni zilizoniwezesha kushinda na kuwa mbunge wa jimbo. Bila Wananchi wa Ruangwa  na chama changu nisingekuwa na sifa ya kuwa Waziri Mkuu.

5. Ninawashukuru Wazazi wangu kwa malezi na miongozo mbalimbali iliyoniwezesha kufikia hatua hii leo. Ninamshukuru Mwenza wangu kwa ushirikiano, ushauri na uvumilivu wake kwa muda wote ambao tumeishi pamoja. Bila yeye, naamini nisingekuwa hata na hamu ya kushiriki siasa.

6.Mheshimiwa Spika, nimeendelea kupokea salam za pongezi kutoka kwa marafiki, ndugu  na Watanzania wengine. Nawashukuru sana!!  Ninajua kazi iliyo mbele yangu ni nzito na yenye majukumu mazito, lakini kutokana na imani kubwa ushirikiano mliyonionyesha na kwa msaada wa Mungu naamini nitaiweza. Ninachowaomba wote ni ushirikiano wenu.Nami naahidi nitafanya kazi kwa bidii, maarifa na uadilifu kuwatumikia Watanzania wote na sintowaangusha. Awamu ya tano ya uongozi wa nchi yetu ni kazi tu. Mheshimiwa Rais ameshaonesha mwelekeo. Nami nitatekeleza kaulimbiu hiyo kwa nguvu zangu zote. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais.

7. Mheshimiwa Spika, hivi  punde Mheshimiwa Rais ameeleza kwa kina  kuhusu wajibu wetu katika kujenga nchi yetu. Nimpongeze sana Mheshimiwa  Rais kwa hotuba yake nzuri ambayo ndiyo mwongozo wetu katika kuanza kutekeleza majukumu yetu. Kama kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni, naomba niseme machache kwa yale aliyoyasema Mheshimiwa Rais na wajibu wetu kama Wabunge.

8. Mheshimiwa Spika, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lina jukumu moja la kutunga sheria. Sisi kama Wabunge, hiyo itakuwa ndiyo kazi yetu ya msingi.  Lakini ni kazi inayotakiwa kufanywa kwa weledi na umakini mkubwa. Nakumbuka Rais Mstaafu, Mzee Benjamin William Mkapa wakati akifungua Bunge Jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku kama ya leo tarehe 20 Novemba, 2000 alitupa methari ya kilatini inayosema  “ Mabaya wayafanyayo watu huendelea  baada ya wao kuondoka Duniani.Wanaua  baada ya wao wenyewe kufa kwa hisia ya hoja walizozijenga wakiwa hai, na kwa sheria walizozitunga.”

9. Tunapoanza kazi hii muhimu, naomba Waheshimiwa Wabunge  tukumbuke maneno ya methari hii katika kutekeleza majukumu yetu  hasa hili la kutunga sheria. Nami nawaombea kila la kheri na fanaka tuwe na busara na hekima katika kutekeleza jukumu hili muhimu.

10.Mheshimiwa Spika, kazi  nyingine kubwa ya Wabunge kwa maoni yangu ni kuwa karibu na Wananchi waliowachagua. Kuna ukweli kwamba, kama Mbunge anafanya kazi yake vizuri, ataweza kuwa karibu na Wananchi waliomchagua kwa kuwaunganisha na Serikali kupitia mawazo yao. Aidha, Mbunge mzuri ni yule anayeweza kuwaeleza Wananchi kile ambacho  Serikali imepanga kukifanya na jinsi ya kutumia raslimali, fursa, mipango na taratibu zilizopo na Serikali kuboresha maisha yao. Ninakumbuka maneno ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akifungua rasmi Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapa Dodoma tarehe 30 Desemba. 2005, alisema na nanuku:-

“Ninyi Waheshimiwa Wabunge,ndio macho na masikio ya Wananchi. Mmeaminiwa na kuheshimiwa.Naomba kila siku mnapoingia au kutoka katika Bunge hili, mnapozungumza humu ndani au mnaposikiliza wengine wakizungumza, mnapokuwa macho au mnapofumba macho kutafakari kwa kina, kila mara mkumbuke imani na heshima hiyo kubwa mliyopewa na Wananchi.” Mwisho wa kunukuu.

11. Maneno haya ya hekima ukiyasoma kwa undani yamebeba hoja na ujumbe mzito sana kwetu. Ni hoja ambayo tunatakiwa tujikumbushe kila mara katika kipindi chote cha miaka mitano cha uhai wa Bunge letu.

12. Mheshimiwa Spika, nafahamu kuwa Mheshimiwa Mbunge anakuwa na majukumu mengi, lakini kubwa ninalolijua ni utumishi wako kwa waliokupa kura.Wananchi wana mategemeo makubwa kuwa kila mmoja wetu atajitahidi kuwa nao ili ashiriki kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo. Aidha, ni lazima sisi kama wabunge kuhakikisha tunarudi majimboni na kufanya kazi na Wananchi ili kuondoa umasikini na kuleta maendeleo. Wakati akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano tarehe 18 Julai, 1975, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema ifuatavyo kuhusu umuhimu wa Wabunge kurudi kwa wapiga kura wao:-

“Wabunge lazima wakati wanatembelea majimbo yao ya uchaguzi; lazima wapatikane kusaidia na kutoa mashauri ya kuwafaa Wananchi  wanaoishi katika sehemu hizo za Majimbo yao.Maana ni sehemu muhimu ya kazi ya Mbunge kuyafahamu matatizo yaliyoko katika Jimbo lake na kujua njia zinazowezekana za kuyatatua matatizo hayo.Kwa kufanya hivyo tu ndipo Mbunge anapoweza kukisaidia chama na Serikali katika ngazi za Mkoani au za Taifa kutatua matatizo kabla hayajawa mabaya mno, na kuwawezesha  wananchi kutumia uwezo walionao  kuleta maendeleo ya kweli.”

13. Mheshimiwa Spika, kila mmoja wetu hapa anafahamu imani kubwa ya wananchi wa majimbo yetu kwa kura tulizopewa za kishindo na wapiga kura wetu. Nawaomba Waheshimiwa  Wabunge tushirikiane na Wananchi wetu ili tuweze kuwasaidia kutimiza kiu yao ya maendeleo na kushirikiana nao kuwawezesha kubadili maisha yao yawe bora zaidi. Wananchi hawategemei kuwa tutaishi Dar es Salaam au Dodoma, bali tutakuwa nao katika majimbo  yetu na kwa wapiga kura wetu. Tukiwa majimboni tujitahidi kushiriki katika vikao muhimu vya kuleta maendeleo.Ninaamini tukiwa karibu na Wananchi katika majimbo yetu tutapata ufahamu wa mambo mengi yanayohusu Majimbo hayo na pengine kupunguza maswali yanayohusu Majimbo yetu tuwapo Bungeni.

14. Mheshimiwa Spika, tumepata kura nyingi zilizotupa ushindi mwaka 2015, na kwamba kazi ya kutafuta kura za mwaka 2020   tunaianza sasa kwa kufanya kazi ya uwakilishi kwa umahili mkubwa. Wito wangu  kwenu  Waheshimiwa   Wabunge ni kwamba, sasa wote kwa pamoja tushirikine na Serikali na Wananchi waliotuchagua kujenga nchi yetu. Masuala  ya makundi ya kisiasa kati yetu sasa yaishe na tufanye kazi kwa maendeleo ya faida ya Taifa letu.

15.Mheshimiwa  Spika, Waheshimiwa Wabunge wanalo  jukumu la kuisimami  na kuishauri Serikali ili kuhakikisha kuwa matatizo na kero mbalimbali za Wananchi zinatatuliwa. Aidha kazi  ya Mbunge ni kuisimamia Serikali kuhakikisha luwa inatoa mchango wake kikamilifu katika kuboresha maisha ya Wananchi kwa kutumia nguvu kazi na raslimali tulizonazo. Ni matarajio ya Serikali kuwa itapata taarifa na ushauri kutoka kwa Waheshimiwa  Wabunge juu ya maeneo yanayohitaji kupewa msukumo ili kuongeza kasi ya maendeleo ya Taifa letu. Kwa upande wake, Serikali itafanyia kazi taarifa na ushauri huo. Lengo ni kuitoa  Tanzania kutoka kwenye dimbwi la uchumi ulio nyuma na tegemezi na kuiingiza katika mkondo wa uchumi imara, endelevu, unaokua na wa Taifa linalojitegemea. Jukumu hilo ni letu sote Watanzania.

16. Twendeni kwenye Majimbo yetu tuanze kazi kwa bidii, ushirikiano na upendo. Kila mmoja akifanyakazi kwa kujituma, nina imani Taifa letu litasonga mbele na maisha ya watu wetu yatabadilika.Mwanazuoni mmoja, Bwaba Ralph Bunche aliandika:

To make our way, we must have firm solve, persistence  and tenacity. We must gear ourselves to work hard all the way. We can never let up!

17.Mheshimiwa Spika, anachosema Mwanazuoni huyu ni kwamba, tukitaka  kusonga mbele kwa mafanikio lazima tuweke dhamira ya kweli na tukomae nayo kwa kufanyakazi zaidi na kwa bidii zote.Mheshimiwa Rais ameshatupatia nguvu mpya ya kwamba “Hapa ni Kazi tu”. Tuweke dhamira na pasiwe na yeyote wa kuturudisha nyuma.

18. Mheshimiwa Spika, narudia kuwaombeni kwamba sasa uchaguzi umekwisha, wote tuseme kwa dhamira moja kuwa “ yaliyopita si ndwele tugange yajayo”. Twendeni sasa tukashirikiane na Wananchi kufanya kazi. Turejeshe ushirikiano na mshikamano. Tuwasaidie na kuwaongoza  Wananchi kutatua matatizo yao. Tusibaki tunatafuta mchawi.

19. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuomba ushirikiano wa Watumisho wote wa Serikali katika kutekeleza ahadi za Mheshimiwa Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati na baada ya kampeni za Uchaguzi, Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Dira ya Maendeleo. Tufanye kazi kwa bidii na kuwatumikia Watanzania kwa kasi na umakini wa hali ya juu.

20. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru wote waliotuwezesha kukamilisha shughuli zilizopangwa kwenye mkutano huu wa kwanza wa Bunge la Kumi na Moja kwa ufanisi mkubwa. Ni dhahiri tumeanza vizuri na ninaamini tutaendelea vizuri!

21. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nawatakia safari njema na naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liahirishwe sasa hadi siku ya Jumanne, tarehe 26 Januari, 2016, saa tatu asubuhi litakapokutana tena hapa Mjini Dodoma.

22.Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

By Jamhuri