ARUSHA

NA MWANDISHI WETU

Idadi ya wazee nchini Tanzania inakadiriwa kuwa asilimia 11 ya watu wote ifikapo mwaka 2050.
Hali hiyo inasababishwa na ongezeko la idadi ya watu na kuboreshwa kwa huduma za afya nchini.
Mratibu wa Huduma za Afya kwa Wazee kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Edward Mung’ong’o, ametoa taarifa hiyo alipowasilisha mada kwenye kongamano jijini Arusha.
Kongamano hilo ni maandalizi ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee.

Amesema mwaka 2002 idadi ya wazee ilikuwa milioni 1.4, ambao ni sawa na asilimia 4 ya watu wote kwa wakati huo (milioni 33.5).
Dk. Mung’ong’o amesema idadi ya wazee  kwa sasa inakisiwa kuwa milioni tatu, ambao ni sawa na asilimia 5.6 ya watu wote. Inakisiwa kuwa sasa Tanzania ina watu milioni 55.
Kwa upande wa huduma za afya, amesema serikali kwa kushirikiana na Shirika la HelpAge International imepitia na kuboresha mtaala wa kufundishia wauguzi ngazi ya kata ili wapate mafunzo yatakayowawezesha kuhudumia wazee vizuri.

Amesema kwa kushirikiana na HelpAge International, serikali imeandaa mwongozo kwa watoa huduma wa namna ya kutibu magonjwa ya kawaida yanayowasibu wazee.
Kamishna wa Ustawi wa Jamii nchini, Dk. Naftali Ng’ondi, akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, amesema wazee watatumia fursa hiyo kujadiliana kuhusu utekelezaji wa sera na miongozo ya kuboresha hali na maisha ya wazee nchini.

Sera na miongozo hiyo inazingatia utambuzi wa wazee katika halmashauri, upatikanaji wa huduma za afya na ushirikishwaji wa wazee.
Maeneo mengine ni huduma za afya kwa wazee na utekelezaji wa mpango wa huduma rafiki wa afya kwa wazee na mabadiliko ya utaratibu wa uchangiaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii na azima ya serikali kufikia pensheni ya jamii kwa wazee wote.
Kongamano la wazee pia litaangalia sera na mfumo wa kodi unavyozingatia mahitaji ya makundi maalumu, msamaha kwa wazee, mauaji ya wazee nchini na jitihada za kukabiliana nayo.

Kamishna Ng’ondi amesema wazee wana haki ya kuheshimiwa utu wao na kupata stahiki kama binadamu wengine, ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, kupata matunzo katika familia na kulindwa dhidi ya madhara yanayoweza kuwaathiri kimwili, kiakili, kihisia na kisaikolojia.
Wazee wameshiriki kongamano la wazee katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee yanayofanyika kitaifa Arusha kwa lengo la kutoa fursa kwa wazee kujumuika na kujadili changamoto na fursa katika kuboresha maisha yao.
Siku ya Kimataifa ya Wazee huadhimishwa kutokana na Azimio la Umoja wa Mataifa Na. 45/106 la mwaka 1990, linalozitaka nchi wanachama kutenga siku maalumu kutafakari kuhusu mchango wa wazee katika maendeleo ya jamii.

By Jamhuri