Iddi Simba lazima ashitakiwe upya

Ugeni mkubwa uliofika hapa nchini umeshaondoka. Ugeni huo ni wa Rais Barack Obama wa Marekani, Rais mstafu George W. Bush wa Marekani, marais zaidi ya 10 kutoka mataifa mbalimbali Afrika na duniani kwa jumla, pamoja na mawaziri waandamizi kutoka mataifa mbalimbali.

Msimamo wetu wakati wa ujio wa wageni hao ulikuwa kwamba tuache mambo yetu ya ndani kwa muda, ili kutoa fursa ya wageni na wenyeji wao kujadili masuala yaliyokuwa mbele yao. Ahadi yetu ilikuwa kwamba baada ya wageni hao kuondoka, ilikuwa ni vema na haki kurejea kwenye masuala yetu ya ndani ya nchi.

 

Yapo mambo mengi yaliyokuwa yameahirishwa. Miongoni kwa hayo ni milipuko ya mabomu mkoani Arusha, sakata la gesi mkoani Mtwara, na mengine mengi. Miongoni mwa hayo mengi, limo suala la Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kumwachia huru aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Iddi Simba, na wenzake.

 

Simba na wenzake walikuwa wakituhumiwa kulisababishia shirika hilo la umma hasara ya Sh zaidi ya bilioni nane kutokana na uuzaji hisa kwa bei ya kutupa. Pamoja na tuhuma hizo, Simba aliingiziwa Sh milioni 320 katika akaunti yake binafsi, jambo ambalo lilikuwa na harufu ya kukosa uadilifu. Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alifanya ukaguzi na kujiridhisha kuwa upo ushahidi wa kutosha wa kumshitaki Simba na wenzake.

 

Lakini katika namna ya kushangaza, DPP, kwa mamlaka aliyonayo (ambayo hayahojiwi), alimwachia Simba na wenzake. Uamuzi huo umewashitua wananchi wote wema walioamua kushiriki mapambano dhidi ya ufisadi. Ni uamuzi wa kutia shaka kwa sababu vielelezo vya namna Simba na wenzake walivyofanya hujuma kwa UDA, viko wazi kabisa.

 

Kuachiwa kwao si tu kumeibua mjadala, bali kumewafanya wananchi wenye kuuchukia ufisadi na uporaji rasilimali za umma kukata tamaa. Wanasema kama Simba, kwa ushahidi uliopo ameachiwa, nani atabanwa? Je, vita dhidi ya wahujumu uchumi ni kwa ajili ya masikini tu?

 

Msimamo wetu kwenye jambo hili uko wazi. Tunatoa wito kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha zinaifufua kesi hii mapema iwezekanavyo ili watuhumiwa wajibu mashitaka. Ushahidi gani zaidi ya huu uliopo wa kuliuza shirika kwa bei ya kutupa? Ushahidi gani zaidi ya huu wa Simba kuingiziwa fedha kwenye akaunti yake binafsi?

 

Tunasema wazi kwamba kama Simba ameachiwa huru, basi hakuna sababu ya kuendelea na kesi nyingine za uhujumu uchumi na ufisadi zinazowakabili Watanzania wengine. Hakuna sababu ya kuendelea na kesi hizi kwa sababu kinachoonekana hapa ni mazingaombwe tu ya kuwapumbaza Watanzania kwamba Serikali iko mstari wa mbele kupambana na ufisadi, wakati watuhumiwa wenye ushahidi wa wazi wakiachiwa.

 

Tunahitimisha kwa kurejea wito wetu kwamba Iddi Simba na wenzake ni sharti mashitaka dhidi yao yafufuliwe. Aidha, vyombo vya dola vichunguze mazingira ya kuachiwa kwa watuhumiwa hawa. Bila kufanya hivyo vita dhidi ya ufisadi itakuwa ni danganya toto.