Miezi ya Desemba 2012 na Januari, 2013 imenitia hofu. Imenitia hofu baada ya kuwapo matukio mengi ya wizi, ujambazi na ukatiri dhidi ya binadamu. Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha wamelazimia kuandamana baada ya majambazi kuwa wanawavamia kwenye mabweni yao na kuwapora kompyuta za mkononi, fedha na vitu vya thamani. Imeelezwa kuwa hadi wanafikia uamuzi huo tayari walikwishaporwa laptop zipatazo 300.

Kwa mkoa wa Kagera ndani ya miezi hiyo miwili, polisi wanne wameuawa na wananchi. Mkoani Arusha na Mara, polisi wanne wamekamatwa wakisafirisha meno ya tembo na wengine bangi. Mirungi imeelezwa kushamiri Arusha na Kilimanjaro. Wimbi la ujambazi limeibuka na kuongezeka kwa kasi ya kutisha.


Kabla ya Rais Jakaya Kikwete kuchaguliwa kushika wadhifa huo, majambazi yalikuwa yanatamba hapa nchini. Kikwete akakuteua wewe Said Mwema kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini. Mwema ukatekeleza kwa vitendo ahadi ya Kikwete kwa wananchi kuwa angedhibiti ujambazi.


Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Hili nimewahi kulisema na wala sioni aibu kulirudia kuwa Kikwete amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti ujambazi walau kwa miaka karibu nane sasa aliyokaa madarakani. Ila kwa bahati mbaya, hali imeanza kuharibika.


Huko Tabata risasi zimeanza kusikika tena. Kigamboni majamabazi wamejihalalishia kila mali aliyochuma kwa tabu Mtanzania. Mwanza nako tumesikia mivumo mwishoni mwa mwaka. Taarifa mbaya za polisi kurejea katika mchezo wa kushirikiana na majambazi na kisha kubambikia kesi wananchi zimeanza kufika tena kwenye vyumbo vyetu vya habari.


Mwema ulivyoingia madarakani, posho za polisi zilikuwa zinatolewa kwa wakati. Kwa sasa taarifa zilizonifikia ni kwamba kasma ama nyingi zimefutwa au zinatolewa kama hisani. Ulivyoingia taarifa za magari ya polisi kukosa mafuta ilikuwa zimepotea, lakini hawa askari wako sasa wanalalamika.


Wanasema polisi anakwenda kwenye lindo kuzunguka mji kama Dar es Salaam usiku mzima anapewa mafuta lita 10. Hivi huyu unatarajia apambane na jambazi aliyejaza tenki zima na tena wakati mwingine amekwishalifanyia mbinu gari lake linajaza hadi lita 200 kwa wakati mmoja?

Yapo maneno yanasemwa na mimi sitaki kuyakubali. Wapo wanaosema kuwa Mwema sasa umeona muda wako wa kustaafu umekaribia hivyo umeamua kupumzika kazi. Wengine wanasema kwa uzoefu wakuu wa polisi wengi wanapokaribika kustaafu uhalifu uongezeka.


Wanasema uhalifu uongezeka kwa sababu mabosi wengi wanakuwa wakichuma fedha za kustaafia. Nieleweke vyema, sisemi Mwema naye anachuma kwa sasa, lakini aibu hii ya polisi kukamatwa na meno ya tembo, kuuawa na wananchi wakiwa ‘kazini’ inatia shaka.


Mwema jiulize, ni wapi umelegeza kamba ubane. Utastaafu kwa heshima kubwa ikiwa utaondoka madarakani Watanzania wanaacha milango wazi. Imani uliyoijenga kwa wananchi juu ya polisi, sasa inaanza kupotea kwa kasi, hasa zinaposikika taarifa kuwa polisi wanasindikiza magogo ya mbao, meno ya tembo na kuwajulisha majambazi wapi wakaibe kisha wao wanafika baada ya tukio.


Nasema haya uliyakuta na ukayadhibiti, nguvu uliyokuwa nayo imepotelea wapi? Mwema linda heshima yao. Wabane polisi, lakini wapatie haki zao wachape kazi kwa nguvu na kuijenga Tanzania iliyosalama, kiasi kwamba historia ikukumbuke. Mungu ibariki Tanzania.

1199 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!