Najua kuwa wanahabari tunaombeleza. Tunaombeleza si kwa sababu ndani ya mwezi huu kuna mwenzetu ameuawa, bali mwenzetu Absalom Kibanda ametekwa, ametolewa jicho, ameng’olewa kucha na kukatwa kodole. Amepewa ulemavu wa kudumu.

Ni masikitiko ya mwaka. Mwenzetu Kibanda leo ninavyoandika makala haya, ana upungufu wa kidole kimoja, meno mawili, jicho moja na kucha tatu. Mwishoni mwa wiki alipokutana na wahariri Neville Meena, Jesse Kwayu na Ansbert Ngurumo walipomtembelea hospitalini alitokwa na machozi.

 

Nampa nguvu Kibanda, naipa nguvu familia yake kuwa kwa pamoja tuweke hata misa kumshukuru Mungu kuwa hadi leo naandika makala haya Kibanda yuko hai. Jicho, kidole, meno na kucha ni tunu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Uhai ni zaidi ya hayo.

 

Sitanii, siku zote huwa nasema kuwa uhai ni zaidi ya nguo tunazovaa, pesa tunazomiliki na uzuri kwa maana ya urembo na utanashati tuliojaaliwa nao. Huwa nasisitiza pia kuwa kila binadamu ni mlemavu mtarajiwa. Ulemavu si dhambi.

Ni wazi leo, mwenzetu Kibanda  amekuwa mlemavu wa viungo si kwa kuchagua, bali kutokana na mazingira. Ila kwa vyovyote iwavyo, hali yake itaimarika, atarejea nchini salama. Nasema, jipe moyo Kibanda, wazazi na mke wake mumkubali Kibanda kwa maumbile yake ya sasa.

Hakuna mwenye uhakika wa kuzikwa kaburini akiwa na viungo vyake timamu. Jambo moja tu nakuhakikishia ndugu yangu Kibanda, watesi wako Mungu ameanza kuwalipa. Tena si kwa kipimo kile kile, bali kwa kutumia kibaba walichotumia na nyongeza juu.

Sitanii. Watafahamika mmoja baada ya mwingine, watakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria. Ombi langu kwa Watanzania, tulaani unyama huu. Tuweke siasa zetu kando. Tusihukumiane wala kusukumiana mpira. Sasa narejea kwa Odinga.

 

Kichwa cha makala haya, kinasema “Ikiwa ni mahakamani huru, tutarajie uchaguzi mpya Kenya”. Nataka kuingia katika historia. Nimefuatilia uchaguzi wa Kenya kwa karibu. Binafsi sina chuki na Uhuru Kenyatta wala William Rutto. Nawatakia kila la kheri.

 

Tatizo langu ni ukabila. Kwamba leo Kenya ina marais wanne, na watatu wametokana na kabila la Wakikuyu, huku mmoja tu Daniel arap Moi ndiye aliyetoka katika Wakalenjini, inanipa shida. Naona ni mwendelezo ule ule.

 

Si tu ni mwendelezo ule ule, bali ukiigwa katika nchi zetu za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaweza kuishia pabaya. Hata hivyo, nawapongeza Wakenya. Idadi ya kura alizopata Raila Odinga ni wazi kuwa hata kura za Wakikuyu wanaoamini kuwa hakutahiriwa, walimpigia kura.

 

Sitanii, kama asingepigiwa kura na baadhi ya Wakikuyu na Wakalenjini wanakotokea Kenyatta na Uhuru, ni wazi hata kura milioni tatu asingezifikisha. Ninachosema hapa ni aina ya ushahidi uliowasilishwa mahakamani kuhusiana na matokeo.

 

Kambi ya Odinga inasema katika majimbo zaidi ya 11, idadi ya kura imekuwa kubwa kuliko waliojiandikisha. Hapa sheria iko wazi. Matokeo ya aina hii yanafutwa. Ninachokiona ni kuwa yakifutwa matokeo ya idadi ya kura kuzidi wapigakura waliojiandikisha, Kenyatta kura zake zitapungua.

 

Hesabu zilizopo ni kuwa Odinga atapata kura asilimia 50 kamili, na baada ya kuondoa wapigakura hewa na Kenyatta atapata asilimia 46. Hapa ndipo itakapokuwa fundisho la jinsi demokrasia inavyofanya kazi nchini Kenya.

 

Katiba iko wazi. Chama kinachopinga matokeo kina siku saba za kuwasilisha pingamizi. Baada ya siku saba, Mahakama ya Rufani ndani ya siku 14 inapaswa kuwa imesikiliza kesi na kutoa hukumu. Haya yakifuatwa, tutashuhudia uchaguzi mpya Kenya mwezi Aprili.

1011 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!