Watu wengi wamekuwa wakisema na kujiaminisha kauli kama hizi: “Tumia fedha kupata fedha,” “Siwezi kuanza biashara wakati sina fedha,” “Bila chochote ni vigumu kupata kitu,” “Wenye fedha ndiyo wanaofanikiwa,” na nyingine nyingi zinazofanana na hizo.

Kiharakaharaka kauli kama hizo zinaonekana kuwa sahihi na zinazokubalika, lakini zina sumu kubwa katika maendeleo ya mtu anayehitaji kuanza ama anaeendelea na juhudi za kujikwamua kiuchumi kwa kuongeza kipato.


Kabla ya kuendelea zaidi, naomba nitoe kisa kutoka kwenye Biblia. Historia ya Wanaisraeli inaonesha kuwa kuna wakati wakiwa utumwani katika nchi ya Misri, kulitokea mabadiliko ya kiutawala baada ya Farao aliyekuwa anawatetea kufariki. Farao ‘mpya’ alikuwa mkorofi, aliwatesa sana kutokana na kuwapa kazi ya kufyatua matofali ya kujenga mapiramidi yote yanayoonekana Misri hadi leo.


Enzi hizo alitokea Nabii Musa aliyetumwa na Mungu kuwaokoa awapeleke nchi ya Kaanani. Harakati za Nabii Musa zilimwongezea chuki Farao dhidi ya Waisraeli na aliapa kuongeza mateso. Awali walikuwa wakifyatua matofali kwa kutumia majani yaliyoandaliwa na wasimamizi wao (wawakilishi wa Farao).

 

Baada ya hasira ya Farao kuwaka, aliamuru mambo mawili. Mosi, Waisraeli wasiandaliwe tena majani ya kufyatulia matofali. Pili, kila Muisraeli aongezewe maradufu idadi ya matofali aliyokuwa akifyatua awali wakati akipewa majani. Huu ulikuwa wakati mgumu sana kwao, hasa ikizingatiwa tangu wazaliwe walijua haiwezekani kufyatua matofali bila kutumia majani.

 

Lakini kutokana na adhabu na mateso ya Farao, Waisraeli walitafuta mbadala na kujikuta wakiendelea na kazi ya kufyatua matofali – tena kwa idadi mpya waliyopangiwa. Kilichowasukuma hadi kutafuta mibadala ni adhabu na mateso waliyokuwa waliyopata kwa kushindwa kutekeleza ufyatuaji matofali.


Tunapata mambo matatu kutokana na kisa hicho. Mosi, ili mtu upambane kupata kitu inategemea na nguvu iliyopo nyuma yako inayokusukuma utafute kitu hicho. Pili, utegemezi unapoondoka akili huwa inakusanya uwezo usiotumika kuhakikisha unaanza kujitegemea. Tatu, ‘nguvu ya asili’ (Mungu) huwa inafanya kazi na watu wanaopanga, kufikiri na kujishughulisha.


Nianze na nguvu inayokuwapo nyuma ya mtu kutafuta kitu fulani, ambapo kwa hapa tunaongelea kutafuta fedha. Kuna nguvu mbili zinazoweza kusukuma mtu kutafuta fedha, ya kwanza ni ile ambayo kwa Kiingereza inaitwa, “Push Power” na ya pili ni ile inayoitwa “Pull Power”.  Katika nguvu ya kwanza unasukumwa kuondoka katika mazingira duni, wakati ile ya pili inakuvuta kuingia katika mazingira bora zaidi hata kama haupo katika hali mbaya sana kimaisha.


Iko hivi, unaweza kuzaliwa katika mazingira ya umaskini wa kutupwa na umaskini ukawa unakutesa na kukuumiza kichwa sana. Unapojaribu kutoka katika lindi la umaskini unakuwa unatumia nguvu ya ‘push power’. Lakini unaweza ukawa umezaliwa katika mazingira ya kawaida ama ya kitajiri isipokua ukatamani kufanikiwa na kufikia hatua fulani ya kibiashara ama ya kimaisha. Kitendo cha kuvutwa na mafanikio yaliyopo mbele yako ndio tunakiita ‘pull power’.


Kuna utafiti niliowahi kuusoma unaoeleza nadharia ya watu wa kabila la Wakinga na Wachagga walivyofanikiwa katika ujasiriamali. Utafiti huu ulieleza kuwa wakinga wamekua wakifanikiwa kibiashara kutokana na ‘push power’ wakati Wachagga wanafanikiwa kutokana na ‘pull power’.


Inapotokea ukawa na moja kati ya hizi nguvu kwa kiwango kikubwa na cha kutosha, ni rahisi na tena inawezekana ukapata upenyo wa kuzalisha fedha ama kupata mafanikio pasipo kuwa na fedha.

1178 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!