Mapinduzi, mageuzi na mabadiliko ni baadhi ya istilahi za kisiasa ambazo kiongozi wa siasa anazitumia katika kushawishi na kuhamasisha wanasiasa wenzake na wananchi kufanya mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika nchi yao.

Bayana iliyoko ni kwamba istilahi zote hizi zina maana moja ya mabadiliko kisiasa.

Ni aina gani ya mabadiliko ambayo kiongozi anataka yawepo kwa kupitia katika chama chake cha siasa, akiwa na malengo yake ya kushika dola, au kuondoa uongozi wa mamlaka iliyoko madarakani na kuweka mpya.

Istilahi hizi ni muhimu na ni mwongozo mzuri, si kwa mwanasiasa tu, bali hata kwa kiongozi wa serikali, mtumishi wa umma, mkulima, mfanyakazi, mfanyabiashara na mtu mwingine yeyote anayetaka mabadiliko ili kufurahia maendeleo yake, utulivu na amani katika jamii au nchi.

Usipojua maana, kanuni na mbinu ya kutumia istilahi yoyote kati ya hizi unaweza usifanikiwe katika shughuli zako za kijamii na kitaifa. Unaweza pia kujiangamiza au kuiangamiza jamii au taifa. Ni vema hekima na busara zikatumika angalau kutambua maana ya mabadiliko.

Mageuzi ni mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi, kitamaduni katika jamii kutoka mfumo mmoja kwenda mwingine. Chama cha siasa kilicho hai, na uongozi imara hufanya mageuzi katika miundo na mifumo ya uongozi na utendaji kazi za chama. Fikra madhubuti hufanya mageuzi madhubuti.

Mabadiliko ni hali ya kitu kuwa tofauti na kilivyokuwa hapo awali. Mabadiliko ya kisiasa ni mapinduzi ya kiuongozi, mabadiliko ya kiuchumi ni kupanda au kushuka  kwa uchumi na mabadiliko ya kitamaduni ni uigaji wa mfumo mpya wa maisha.

Katika Mwongozo wa TANU wa mwaka 1971, tunaelezwa: “Mapinduzi ni mabadiliko ya haraka katika jamii ambayo yanawanyang’anya wachache madaraka waliyokuwa wakiyatumia kwa manufaa yao na kuyaweka madaraka hayo mikononi mwa walio wengi ili kuendeleza masilahi yao.” Mwisho wa kunukuu.

Kwa hiyo tunasema mapinduzi ni mabadiliko muhimu na ya haraka namna watu wanavyofanya katika mbinu na hali, kama vile kilimo, viwanda, elimu na kadhalika. Na ni mabadiliko katika namna nchi inavyofanya yanayohusu mabadiliko katika mifumo ya aghalabu ghasia au mapigano.

Baadhi ya viongozi wa siasa wanatumia istilahi hizi kufanya ghasia au mapigano, kuchafuana kitabia na kutukanana, wakiamini kufanya haya ndiyo mabadiliko katika chama cha siasa au katika uongozi wa nchi. Jambo usilolijua ni kama usiku wa giza.

Mbinu za kufanya ghasia au mapigano hazifai katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia, uliojaa silaha kali za maangamizi. Ni kuchafua mazingira, kuharibu miundombinu iliyoko na kuua viumbe vilivyomo duniani. Hakika, mchimba kisima huingia mwenyewe.

Kadhalika kuchafuana tabia na kutukanana kunajenga chuki, uhasidi na kisasi cha milele, mambo ambayo si malengo ya kutaka mabadiliko. Malengo na madhumuni ya kufanya mabadiliko ni kupata mafanikio bora zaidi, na kuishi kwa upendo, amani na usalama katika umoja na mshikamano.

Viongozi wenye taaluma ya siasa na maadili ya uongozi kamwe hawageuzi mageuzi, mapinduzi au mabadiliko kuwa zana za kuua wananchi. Wanaoweza kufanya hivi ni wale viongozi mazuzu na uchwara, ambao kwa kweli hawastahili kupewa madaraka ya kuongoza katika vyama vya siasa.

Viongozi wa siasa waliotumia istilahi hizi kinyume cha matumizi halali wamezitumbukiza taasisi na nchi zao katika zahama na shaka isiyokwisha kila uchao. Yamkini, wamezitumbukiza nchi zao katika vita, na wao kukosa asali na kupata shubiri. Mtaka yote kwa pupa hukosa yote.

Ukweli, makazi salama hayapatikani. Miundombinu inaharibiwa, ufukara unatawala, amani inatoweka na mauti yanazunguka kama pia. Haya ni mabadiliko katika mabadiliko. Wananchi wa Tanzania tunataka mabadiliko. Je, ni mabadiliko ya aina gani?

By Jamhuri