Taifa letu Tanzania lipo katika mchakato wa kuandika Katiba mpya. Mchakato huu umekwishafikia hatua nzuri. Tayari Tume imepata wajumbe 32 wakiongozwa na Jaji Joseph Warioba. Tume hii imesheheni watu muhimu na jamii inaiamini kweli. Mimi ni mmoja wa watu wanaoiamini. Jaji Warioba naamini anaifahamu vyema Katiba yetu na pia Katiba za mataifa mengine.

Itakumbukwa mwaka 1977 wakati inaandikwa au inatungwa Katiba tuliyonayo sasa, yeye ndiye aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ndiye aliyepeleka ombi la kuandika Katiba mpya nyumbani kwa Mwalimu Julius Nyerere kule Msasani na akakubaliwa iandikwe Katiba mpya. Nimerejea kipande hiki kidogo kwa nia tu ya kukufanya wewe msomaji ikiwa hukubahatika kupata nakala zilizotangulia, walau sasa uwe na picha halisi.

Makala iliyopita, nilisema leo nitazungumzia jinsi mfumo mpya au Katiba mpya itakavyoweza kutubakiza wamoja, kwani kati ya watu wanaonipigia simu wengi wanahoji mapendekezo yangu ya kurejesha Serikali ya Tanganyika yatawezaji kuiacha Tanzania likiwa taifa imara. Hapa nasema wala tusipate mpasuko wa roho hata chembe.

Kubwa ni kuhakikisha kuwa tuna sheria na mfumo imara. Wapo wanaosema Tanganyika itakuwa na nguvu kubwa ya kifedha hivyo itamsumbua Rais wa Jamhuri ya Muungano. Mimi nasema hili si kweli. Huu ni uvivu wa kufikiri. Ninayo mifano hai. Leo katika Tanzania, halmashauri tajiri kuliko zote ni Tandahimba (Mtwara) kutokana na mauzo makubwa ya korosho na ya pili ni Ilala. Wilaya kama Geita ya Mkoa wa Geita ina utajiri mkubwa kuliko mikoa kama saba ikiunganishwa.

Hata hivyo, kutokana na sheria zilizopo hatujasikia Wilaya ya Tandahimba ikijitangaza kuwa Jamhuri kutokana na utajiri wake. Pia wazo kwamba Zanzibar uchumi wake ni mdogo, si la kukumbatia sana. Pale Zanzibar kuna mafuta. Siku urasimu uliopo na ukiritimba ukiondolewa Zanzibar wakachimba mafuta, ndani ya mwaka mmoja watakuwa kama Dubai.

Tena Zanzibar leo tunaopambana nao kupata asilimia 4.5 ya misaada ya kimataifa, watakuwa na fedha nyingi hadi watato misaada kwa Tanganyika, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Marekani. Tuache roho mbaya, tuwe na fikira endelevu, nchi yetu ipae kiuchumi. Hivi leo tunapobishania mafuta ya Zanzibar ilhali hata mafuta yenyewe hayajachimbwa tunapata faida ipi?

Hivi ikiwa Zanzibar watabaki na mafuta yao, nasi tukabaki na gesi yetu Mkuranga, Songosongo, Mnazi Bay na mafuta yetu pale Mtwara, Kigoma kwenye Ziwa Tanganyika na ule mlima wa dhahabu ambayo mkondo wake unaanzia Mbeya, unakatiza pori na kupita Geita ukaishia kwenye Ziwa Victoria tutapta hasara gani?

Hapo sijataja madini ya tanzanite, nickel kule Kabanga Ngara, ambako mradi huo ukianza pekee unahitaji megawati 800 za umeme na kujengewa njia ya reli, sijataja madini ya urani, ambapo yapo Bahi, Mtwara, Singida na Bukoba, hivi tunaogopa nini? Tunaogopa nini kuwapa watu fursa ila tukatunga sheria itakayoepusha mzozo.

Hapo juu nimetumia mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba na Ilala ya Dar es Salaam ambayo ni ya pili kwa kuwa na pato kubwa nchini. Mbona wilaya hizi hazijajitangaza kama Jamhuri. Haziwezi kufanya hivyo kwa sababu zinaongozwa na sheria. Tanzania hii hatupaswi kuwa masikini. Kinachotuchelewesha ni uongozi mbovu na mfumo usiotabirika wa kuongoza nchi hii.

Ikumbukwe ule mkutano wa Berlin, uliofanyika kati ya Oktoba 1884 hadi Februari 1885, ulifanyika nyumbani kwake Ujerumani. Mkutano huu uliigawa Afrika katika makoloni. Mimi natokea Bukoba. Huwa tuna msemo kuwa “Owawe kashuntama omunshongo totaa shabo.” Maana yake ni kwamba ndugu yako akikaa unakoanzia mto, huwezi kuteka tope. Siamini kama Ujerumani katika ugawaji wa makoloni ya Afrika, wao waliamua kuteka tope kwa kuichukua Tanganyika.

Tanganyika yetu ni nchi tajiri. Kuirejesha ikapata usimamizi wa karibu, kutatuwezesha watu wake kusimamiwa kwa karibu wakafanya kazi kwa nguvu, maliasiri lukuki zilizopo ziendelezwe na kuvunwa hatimaye tuwe na taifa lenye nguvu ya kiuchumi. Ni matamanio yangu kuwa Katiba mpya irejeshe sheria ya viboko iwe haki mpya kwenye Katiba. Asiyefanya kazi achapwe viboko. Hii iwe haki ya kikatiba.

Kwa nia ya kulinda umoja wetu, masuala ya msingi kama sarafu, uhamia, uraia, ulinzi na usalama, elimu, uhusiano wa kimataifa na mengine yenye sura ya kitaifa yabaki kuwa ya Serikali ya Muungano. Hapa Serikali ya Muungano inapaswa kusimamia Sera na si utendaji. Utendaji utabaki chini ya hizi Serikali za Tanganyika na Zanzibar.

Tutakuwa na shule za kitaifa. Shule hizi zitatumika kukutanisha watoto wa mikoa mbalimbali ya Tanganyika na Zanzibar. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), itabidi lirejeshwe kwa mujibu wa sheria. Watumishi wa umma itabidi tuwe na kitu kinaitwa Quarter System. Kwamba kwa nia ya kudumisha utaifa wetu, iwepo idadi ya Watanganyika watakaokwenda kufanya kazi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kinyume chake.

Haya na mengine yatakayoainishwa, yatumike kujenga umoja wetu. Kubwa tusing’ang’anie hali ya kusema lazima tuendelee na mfumo wa zamani. Tuwe tayari kujaribu mambo mapya.

Najua wapo watu wanaodhani Katiba mpya itakuwa na mambo yote mapya, nadhani fikira za aina hii nazo si sahihi. Ni ukweli ulio wazi wala usiohitaji kupakwa sukari, kuwa tangu kifungu cha kwanza hadi cha 30, yakibadilika mambo mengi ni kufuta maneno Ujamaa na Kujitegemea na kuweka Sera mpya tutakayokuwa tumeichagua, na kueleza muundo wa Serikali badala ya mfumo wa Serikali mbili hivyo Katiba itatamka rasmi Serikali tatu.

Hapa nazungumzia Sura ya Pili sehemu ya tatu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) yenye vifungo ambavyo huenda tusitengue hata kimoja kuanzia Kifungu cha 12 kinachoeleza HAKI YA USAWA hadi kifungu cha 32 kinachozungumza jinsi ya KUTANGAZA HALI YA HATARI. Hivi vinaendana na tamko la kimataifa la haki za binadamu.

Niliahidi kuwa nitaanza kujadili Katiba yetu tuliyonayo, kwa nia ya kukupa mwanga wewe msomaji. Katika Katiba yetu kama nilivyotangulia kusema nina tatizo na Katiba iliyopo kuanzia kifungu cha 33, ambayo ni Sura ya Pili ya Katiba inayomhusu Rais. Katika makala yaliyopita nilidokeza kuwa kuna hatari ya kukuta tunatumia sanduku la kura kumwingiza mfalme madarakani.

Kiungu cha 34.-(1) kinasema: “Kutakuwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano, na pia juu ya mambo mengine yote yahusuyo Tanzania Bara.”

Kifungu hiki mimi nasema hapana. Ya Mungu mpe Mungu na ya Kaizali mpe Kaizali. Hivi leo Zanzibar ikigombana na Tanganyika (kwa mfano) watakimbilia kwa nani kusuluhishana? Hili nimelifafanua vyema katika makala zilizopita kuwa ni hatari Rais anayesimamia mambo ya Tanganyika huyo huyo kuwa ndiye anayesimamia mambo ya Muungano. Najua miaka ya nyumba kwa kuandika haya tayari ningekuwa gerezani, lakini si vyema tukafikishana mahala tukaogopa kufikiri na kueleza fikira zetu bayana. Nasema hapa walikosea na nafasi ya kusahikisha makosa hayo ni sasa.

Wiki ijayo, nitaendelea kuchambua vifungu vya SURA YA PILI ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayozungumzia SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO SEHEMU YA KWANZA na mamlaka ya RAIS.

Makala zilizopita, nilikuwa najenga msingi, sasa naamini baada ya msingi imara umefika wakati sasa niweke tofoli, baadae niezeke bati na hatimaye tuweze kuingia ndani ya nyumba isiyo na nyufa. Usikose nakala ya toleo lijalo ambapo nitachambua kwa kina kifungu cha 36 kinachompa madaraka ya kutisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

1352 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!