Gazeti la JAMHURI limepongezwa kwa kuchapisha makala mbalimbali za Mwalimu Julius Nyerere na Ripoti ya Rushwa ya Jaji Joseph Warioba zinazolenga kuwapa wananchi kumbukumbu ya matukio yaliyotokea hapa nchini kwa vipindi tofauti.

Akichangia mada kuhusu uzalendo, uadilifu na utaifa katika kongamano la Maadhimisho ya Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere, lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Samwel Kasori, Amesema analishukuru sana gazeti la JAMHURI kwa kuchapisha ripoti ya Jaji Warioba na kuwafanya wananchi waelewe kinachoendelea.

“Niwashukuru watu wa JAMHURI kwa kuchapisha ripoti ya rushwa ya Jaji Warioba, kwani Serikali haikuona maana yoyote na iliishia kuyachoma moto makabrasha yote na sijui tunakwenda wapi?,” Amesema.

Amesema kwa muda wote amekuwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hadi alipofariki na kwamba mwaka 1964 aliwaeleza askari wetu waende kujenga Tanzania huku maadili, uzalendo na utaifa vikizingatiwa.

Amesema rasilimali kubwa hapa ni ardhi. Mwalimu aliwahi kumwita na kumweleza kwamba anawapenda sana Watanzania, anawahurumia wote na hicho ndicho alichojivunia.

“kwa kuwapenda Watanzania bila kuwaza maslahi ya watoto wangu na familia yangu pengine nitahukumiwa kwenda motoni tu lakini kwa kuwatumikia Watanzania nitakwenda mbinguni,” Amesema Kasori.

Akizungumzia rasilimali ya ardhi, Amesema Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilianzishwa kwa madhumuni ya kuwaandaa wataalamu wetu na wengine kutoka nje ya nchi, lakini Watanzania bado hatujanufaika na elimu inayotolewa na chuo hiki na badala yake wananchi wa Botswana waliosoma hapo wameliendeleza taifa lao kwa kilimo cha kisasa na sisi sijui tunafanya nini?

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, Amesema sifa kubwa ya msingi ni uzee siyo urais, na sifa ya uzee siyo kufanya mambo ya hovyo hovyo.

Katika mada yake alizungumzia miiko miwili ya uongozi na wa kwanza ni ukiwa ni binadamu wote ni sawa na kwamba kama hatuwezi kukubali hilo mtu anaweza akaamua kujitukuza yeye mwenyewe kwa kujiona bora kuliko wengine.

Suala la pili alilolizungumzia ni Katiba ya nchi, ambayo awali ilianza kutengenezwa Katiba ya Chama Cha TANU ndipo baadaye ikafuata Katiba ya nchi ambayo imekuwa ikivunjwa mara kwa mara.

“Rushwa na ukosefu wa maadili ikiwamo ‘upigaji dili’ ni uvunjaji wa Katiba ya nchi na kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake, hivyo nawaomba CCM nendeni mkapambane na wenzenu huko nje kwa hoja,” Amesema Butiku.

Amesema, Mwalimu Nyerere hakuwa mtu wa kujilimbikizia mali wala kuvunja Katiba, alimheshimu na kumthamini kila Mtanzania sawa na ilivyokuwa miiko ya viongozi ilivyoelekeza.

Wilson Mkama, akitoa mada iliyohusu ‘Miiko ya Uongozi na Azimio la Arusha’, Amesema kuna tofauti kati ya taasisi na asasi ambako taasisi inakuwa na malengo ya kudumu na asasi ikiwa na malengo mafupi ya kibiashara yenye kulenga faida kwa haraka.

Amesema ujio wa Azimio la Arusha haukutokana na ajali za nyakati. Katika muda mfupi tu, baada ya Uhuru palianza kuonekana na kushuhudiwa kwa mgawanyiko katika nchi, kati ya walionacho na wasionacho.

“Kundi la walioneemeka lilianza kuibuka miongoni mwa viongozi wa kisiasa na warasimu. Ukweli ni kuwa hawa viongozi walikuwa maskini enzi za ukoloni, lakini ndani ya kipindi kifupi tu cha takriban miaka sita tu ya Uhuru, sasa walianza kujitajirisha wakitumia nyadhifa zao katika chama na Serikali.

Baada ya kubaini hali hii na hatari iliyokuwa mbele yake, Mwalimu Amesema palikuwa hapana budi kuchukua hatua kwa kuamua lengo jipya la Taifa letu.

Pamoja na kujengwa katika misingi ya Imani ya TANU na Madhumuni yake ya kuanzishwa Azimio la Arusha, lilitoa sifa kuu zinazotofautisha nchi ya kijamaa na nchi nyingine, kwa kubainisha sifa kuu nne zinazoendana na ujenzi wa Ujamaa, ambazo ni: hakuna unyonyaji; njia kuu za uchumi ziwe chini ya wakulima na wafanyakazi; demokrasia na Ujamaa ni Imani,”Amesema.

Kuhusu Azimio la Arusha Amesema Februari 25, 1991, Mwenyekiti wa CCM wakati huo, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, alijaribu kuibua dhana ya ‘lazima twende na wakati’ na umuhimu wa kuchambua kwa undani mazingira ya kisiasa na kiuchumi yaliyokuwa yanaikabili nchi yetu lakini haikufua dafu na pia kwa wasomi mwitikio ulikuwa hasi.

“Nimesema ni vyema nizungumze nanyi leo ili niweze kusahihisha matangazo ya vyombo vyetu vya habari kuhusu maamuzi (uamuzi) ya Halmashauri Kuu ya Taifa yaliyofanyika katika kikao chake cha Zanzibar hivi karibuni. Nataka kwanza tuelewane kabla ya kusema lolote kwamba, siasa yetu bado ni ile ile haikugeuka hata kidogo. Ni ile ile ya Ujamaa na Kujitegemea.

Kule Zanzibar, tulizungumza mambo mengi miongoni mwake ilikuwa kutoa tafsiri ya baadhi ya vipengele vya Katiba ya CCM vilivyochukuliwa kutoka Azimio hilo ili twende na wakati,” inaeleza sehemu ya hotuba ya Rais wa Awamu ya Pili, Alhaj Mwinyi.

Mkama Amesema mara zote yanapofanyika maamuzi (uamuzi) makubwa kama haya ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha, na kuleta mabadiliko katika ‘Gund norm’ iliyokuwa inajengwa Tanzania, mara zote mabadiliko kama haya hayawezi kupitishwa ‘Nemine Contradicente – with no body saying no’.

Pia akimnukuu Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Amesema alikiri kwamba yeye alikuwa ‘anamheshimu Deng Tsiao-Ping … je, Nyerere angefufuka ungesemaje?’ Mkapa akamjibu … angesema kwamba mimi nimegawiwa mengi yaliyokuwa katika sekta ya umma. Na angefadhaishwa na ukweli kwamba, mimi nimefanikiwa kujenga tabaka la mabepari matajiri.

Ibrahim Kaduma katika mada yake ‘Kuhusu Maadili ya Viongozi Nchini Tanzania’, Amesema katika suala zima la uwajibikaji wa pamoja viongozi wanafiki waogopwe kama ukoma.

Kaduma Amesema maadili ya uongozi maana yake ni misingi, taratibu au kanuni za uongozi zinazoweza kuwa za kitaaluma, kitaasisi au kitaifa, ambazo kila kiongozi anapaswa kuziheshimu.

Akitoa mfano Amesema, madaktari wanakuwa na kanuni ambazo zinatawala taaluma zao ambazo zimeainishwa katika chama chao cha madaktari wa binadamu au wa wanyama, na mwanachama anapokiuka kanuni hizo anaadhibiwa kufuatana na ukiukaji wake kwa kufukuzwa uanachama au kunyang’anywa cheti chake na wanasheria, wahandisi na wengineo wanazo kanuni za kazi zao.

Amesema kutokana na uadilifu aliokuwa nao mwalimu Nyerere, aliamua kuacha kazi yake ya ualimu katika Sekondari ya Pugu mwaka 1955 na kuajiriwa na Chama cha TANU, akiwa Rais Mtendaji, pia aliachia nafasi nyingi za uongozi alizokuwa nazo kwa hiari yake mwenyewe licha ya kwamba alikuwa na nguvu na umaarufu kama kiongozi.

“Mwalimu hakung’ang’ania madaraka na wakati wote alipenda kusikiliza mawazo ya wengine hata waliompinga. Lakini ukosefu wa maadili unaojitokeza sasa unatokana na kuacha misingi hii yote iliyokuwa inafundishwa katika Chuo cha Kivukoni,” Amesema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, Amesema lengo la Mwalimu Nyerere kuwapeleka watu kujifunza katika chuo hicho lilikuwa kwamba wajifunze uzalendo kwa nchi yao.

Akitoa mada kuhusu Maadili na Miiko ya Uongozi nchini, Amesema watu walipelekwa katika chuo hicho walifundishwa kozi kuhusu uzalendo kwa mwaka mmoja na baada ya hapo walipelekwa vijijini kwa ajili mafunzo kwa vitendo yaliyochukua muda wa mwezi mmoja.

“Walipohitimu mafunzo yao hapa chuoni, walipelekwa katika vijiji mbalimbali na kupangiwa kazi na wenyeviti wa vijiji huku wakichunguzwa mwenendo wao na baada ya kuhitimu walipangiwa kazi katika taasisi za umma kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi.

Kulikuwa maadili ya uongozi na miiko ya uongozi, lakini ilipoachwa kufuatwa baadhi yao walithubutu hata kujipatia nafasi za uongozi kwa njia ya rushwa wakiwamo walioomba nafasi za kuwania ubunge ndani ya chama.

Miiko hii na maadili ya uongozi ipo ndani ya CCM, ndiyo maana wale wote waliokuwa wamejipatia kura kwa njia za rushwa, hatukuwapitisha na badala yake tuliwachukua wale waliokuwa na idadi ndogo ya kura.

Pamoja na mada na michango mbalimbali iliyotolewa na washiriki wa kongamano hilo, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ambaye alimwakilisha Rais John Magufuli, Amesema Chuo hicho cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilikuwa kinatoa makada wazuri wakati huo kikiwa Chuo cha CCM, lakini mwishoni kilisahaulika na kutaka kufa kabisa.

Rais huyo mstaafu Amesema ameridhishwa sana kwa kurejeshwa upya kwa mafunzo ya miiko ya uongozi na maadili ya viongozi, ambayo ni tunu kwa kiongozi yeyote.

Mkapa Amesema Baba wa Taifa alikuwa anasoma sana makala za kimataifa na kitaifa tofauti na ilivyo kwa Watanzania wengi ambao ni wavivu wa kusoma na wanachosubiri ni kutoa makala zao katika mitandao ya kijamii na TV ambao nao hawapendi kusoma. Kwa hiyo, anaacha kusikiliza mada zao.

Amesema Mwalimu alikuwa hodari sana wa kusikiliza sana watu wengine kabla ya kuongea, aliwasikiliza waliokuwa wanampinga na wale waliokuwa wakimuunga mkono.

“Elimu yetu bado haiko kwenye misingi mzuri. Marekani hakuna mtu anayehesabiwa amefaulu elimu yake ya juu bila kufahamu historia ya Marekani, Waafrika si kwamba hatutaki kujifunza historia yetu bali za wazungu,” Amesema Mkapa, aliyekuwa mgeni rasmi katika kongamano.

Amesema anasikitishwa na jinsi elimu yetu ilivyo kwa sasa, ambako mwanafunzi anamaliza elimu ya chuo kikuu lakini haelewi Kawawa alikuwa ni nani? Sera aliyotuachia Mwalimu Nyerere ni Kujitegemea.

John Shibuda, yeye Amesema, wanasiasa wengi wanapenda kuitwa wanasiasa wakati hawaelewi maana ya siasa.

Jaji Joseph Warioba Amesema Mwalimu Nyerere hakuwa mkabila, wala mdini kwani alimjali kila Mtanzania, alitaka kuwainua watu wa chini, alikuwa mcha Mungu, mchapakazi na mwadilifu.

Jaji Warioba Amesema, pamoja na yote hayo hakuacha uhusiano na rafiki zake wengi na kucheza bao na watu wa kawaida waliokuwa miongoni mwa marafiki zake.

Amesema, Mwalimu Nyerere alikuwa na utaratibu wa kuwasikiliza wananchi, pia alishirikiana na viongozi wenzake katika shughuli mbalimbali za kuwaletea maendeleo Watanzania.

Naye Augustine Mrema, akichangia mada katika kongamano hilo, Amesema amefuata nyayo za Mwalimu Nyerere kwani hakujilimbikizia mali alipokuwa Naibu Waziri Mkuu na ameishi maisha ya kawaida.

By Jamhuri