Mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga, January Makamba, ametangaza kuwa amejipanga kuongeza kasi ya maendeleo ya elimu katika jimbo hilo, kazi itakayofanyika kwa kupitia Shirika la Maendeleo Bumbuli (BDC) kuanzia mwaka huu.

 

Programu hiyo itagharimu Sh. milioni 40 ikijumuisha vivutio kwa walimu na wanafunzi wa shule za sekondari; yote ikilenga kuongeza tija na umakini wa kujifunza na kusaidia juhudi zinazofanywa na serikali katika elimu.

Katika hatua yake ya kwanza, programu hiyo inayoanza kwa majaribio itakuwa ni ya miaka mitatu na imelenga kuanza na sekondari 17 za kata, zile ambazo mwaka jana hakuna iliyotoa mwanafunzi hata mmoja aliyepata daraja la kwanza kwenye mitihani ya kuhitimu kidato cha nne.

 

Kwa mujibu wa January, wanafunzi waliohitimu ngazi hiyo ya elimu mwaka 2011 walikuwa 1,274 lakini kati yao, wanne walipata daraja la pili na 39 daraja la tatu, matokeo ambayo ni mabaya kupindukia katika ushindani wa dunia ya sasa inayohitaji kwa kiasi kikubwa kabisa maendeleo ya elimu.

 

Ili kufanikisha mpango huo, kila mwanafunzi atakayepata daraja la kwanza hadi la nne atazawadiwa Sh. 50,500 huku walimu wakijinyakulia Sh. 60,400 wakati shule, kama taasisi zitapewa Sh. 31,600 na Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ambako ndiko liliko jimbo hilo, itakuwa inapata Sh. 15,800 kwa kila mwanafunzi anayefaulu kwa ngazi hizo.

 

“Fedha zinazokwenda shuleni si za kugawana Wajumbe wa Bodi, tunataka ziendelee kuinua ufaulu ikiwamo kununulia vitabu”, anasema January na kuendelea: “Tunataka ufaulu wa mwaka huu (wa 2012) uongeze chachu ya ufaulu mwaka ujao”.

 

Hivyo ndivyo amejipanga mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia. Anataka kuliinua jimbo lake kielimu, sekta ambayo ndiyo msingi wa maendeleo yote duniani. Kwa jinsi ninavyomfahamu kuwa ni kiongozi mbunifu, anayefanya kila jambo kwa kushirikisha wenzake na ambaye siku zote kiu yake ni kusonga mbele, sina mashaka kwamba atafikia lengo hilo.

 

Nasema hivyo si kwa sababu ninataka kumpamba, kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa au kumpa sifa asizokuwa nazo. Nasema hayo kwa vile naujua uongozi wake, utendaji wake, ushirikishaji wenzake, ubunifu wake, ari yake ya kazi, kasi yake, imani yake na ushirikiano wa hali na mali alionao kwa kila mtu anayekuwa naye katika utekelezaji wa majukumu yanayokuwa mbele yake.

 

Mimi si afisa wala mfanyakazi wa ngazi yoyote wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, na pia sifanyi kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto wala si mtumishi wa umma au wa sekta binafsi mahali popote kule Bumbuli.

 

Namfahamu January kutokana na sababu moja tu; yeye ndiye Mkuu wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ile ambayo mimi ni mmoja wa maafisa wake waandamizi, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu, Lumumba jijini Dar es Salaam .

 

Pamoja na kuwa umri wake bado ni mdogo wa miaka 38 tu hivi sasa, mbunge huyo ni mfano wa viongozi ambao siku zote, wakati wowote na mahali popote wanaweka mbele maslahi ya umma kwa kutumia mazingira yanayokuwapo, fursa zinazokuwepo na mwelekeo wa jambo linalohitaji kutekelezwa kwa faida ya wote.

 

Kama bosi wangu mkuu wa idara ninayofanya kazi, January amekuwa akitushirikisha wote katika utekelezaji wa majukumu yetu kwa jambo lolote na hatua zote huku akitupa uhuru wa kutosha ukiwamo wa kumuona, kumshauri au kuomba ushauri wake na ajabu zaidi, Naibu Waziri huyo anakuwa radhi na tayari kukosolewa kwa jambo lolote na kujirekebisha endapo litakuwa na tija kwa wote.

 

Licha ya madaraka ya juu aliyonayo katika chama kinachotawala, serikali yake na Jimbo la Bumbuli, January ni kiongozi asiye na makuu au asiyetaka kujikweza ama kutukuzwa, lakini katika orodha ya wachapakazi hodari na makini jina lake haliwezi kuwa chini isipokuwa juu.

 

Ni katika hali hiyo ama vinginevyo, hakika ninaamini kwa asilimia 100 kuwa mkakati wake wa kuliletea maendeleo ya elimu jimbo hilo la Bumbuli utakuwa na matunda chanya. Kitu pekee anachopaswa kupewa ni ushirikiano wa hali na mali kutoka kwa kila mdau ili pamoja na mambo mengine, miaka mitatu iliyotengwa kwa majaribio itumike kuhakikisha kwamba lengo hilo linafanikiwa na kuvukwa.

 

Wakati mkakati huu mzuri na bora ukibuniwa na kuanzishwa na January Makamba katika Jimbo hilo la Bumbuli, kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi hasa wa kidato cha nne nchini kinazidi kushuka kwa kasi.

 

Matokeo ya mitihani ya kuhitimu kiwango hicho cha elimu yanaonyesha janga kubwa la taaluma huko mbele ya safari, hatari inayoweza kuifanya Tanzania kuwa ya watu wanaosoma hadi shahada za taaluma mbalimbali, lakini ufahamu wao unakuwa kama wa wanafunzi wanaohitimu kidato cha sita au chini zaidi kutoka mataifa mengine duniani.

 

Nilipokuwa nasoma shule ya msingi, kipindi hicho enzi za Serikali ya Awamu ya Kwanza na kuendelea hadi wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Pili, kila darasa lilikuwa halizidishi wanafunzi 45 na 36 kuanzia kidato cha kwanza.

 

Aidha, kila wanafunzi watatu katika shule za msingi walikuwa wakikaa dawati moja na kushirikiana kitabu kimoja kwa kila somo na vyote vilikuwapo. Wale waliobahatika kwenda sekondari; kila mwanafunzi alikuwa na kiti chake mwenyewe, meza yake na vitabu vya peke yake.

 

Kana kwamba haitoshi, kila mwalimu kwa somo lake darasani alihakikisha kuwa anajitahidi  kufundisha kwa juhudi na maarifa yake yote, bidii zake zote, ujuzi wake wote na upendo wa hali ya juu kwa kila mwanafunzi, mambo waliokuwa kielezwa wanafunzi wa ngazi hizo za elimu wa siku yanaonekana kuwa hadithi ya kutunga.

 

Leo wanajazwa hadi 100 kwenye chumba kimoja cha darasa huku pengine nusu yao au zaidi wakiwa wameketi katika sakafu. Wanakuwa idadi hiyo huku wakiwa hawana vitabu vya kiada, badala yake kila mmoja anatakiwa akajinunulie mwenyewe na mtoto wa masikini inakuwa “shauri yake”.

 

Tofauti na miaka hiyo inayosemekana kuwa iliishia katika kizazi chetu shuleni, leo hakuna mwalimu kuanzia wa chekechea, shule ya msingi, sekondari hadi vyuo vikuu anayefundisha kwa moyo wake wote, juhudi zake zote wala upendo kwa wanafunzi wa darasa au wa somo lake. Sasa wanataka wanafunzi wakitoka kwenye vipindi vya kawaida wabaki ili wafundishe tuisheni kwa malipo.

 

Kila mwalimu anafundisha chini ya kiwango kwa muda wa kawaida, lakini anaongeza bidii pale anapobaki na wanafunzi wa tuisheni ili kuvutia wengi. Hii imesababisha wale wasioweza kulipia masomo hayo ya ziada kuwa nyuma kwa kila kitu.

 

Hapo ndipo yanapotokea mashindano ya kufeli badala ya kufaulu kama ilivyokuwa zamani. Hapo ndipo wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne au cha sita wanaposhindana kupata daraja sufuri, la nne na wachache sana, tena katika shule chache wanaambulia angalau daraja la tatu huku la pili na la kwanza wakihesabika.

 

Hapo ndipo ninapoupongeza mkakati wa Makamba wa kuanzisha mashindano ya ufaulu katika jimbo lake. Hakika jambo hili linapaswa liigwe na wabunge wote, lengo likiwa ni kuifanya Tanzania ya sasa na ijayo iwe kinara kwa elimu katika Afrika Mashariki na Kati.

 

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244

 

By Jamhuri