Wiki iliyopita tulikuletea sehemu ya tatu ya makala haya. Leo tunakuletea sehemu ya nne. Endelea…

Moja ya madai ya Waislamu ni kwamba wao mbali ya kumwelekeza Qibla mnyama anayechinjwa, lakini pia ni lazima atajiwe jina la Mwenyezi Mungu.

Hoja hiyo inakuwa na utata kwa sababu vitabu vingine vya hadithi sahihi za Kiislamu, vinasema Mwislamu anaweza kumchinja mnyama hata kwa kutaja jina lake tu maadam ni Mwislamu.

 

Moja ya vitabu hivyo kinaitwa “Mkweli Mwaminifu”  na  kimeandikwa na Sheikh Said Moosa Mohammed al-Kindy wa Muscat, Oman.

 

Juzuu 3-4, Uk.13 Hadith Na. 727 inasomeka hivi: Mwislamu inamtosheleza jina lake, basi akisahau kusema jina (la Mwenyezi Mungu) wakati anapochinja, basi aseme (anapokumbuka) asha ale”.

 

Kwa mujibu wa hadithi hii, Mwislamu anaweza kutaja hata jina lake tu la Uislamu wakati wa kuchinja mnyama. Je, wasio Waislamu walitegemee jina hilo la Mwislamu kuwa limekamilisha ibada ya uchinjaji? Je, yeye ndiye Mungu?

 

Suala la kuelekeza wanyama Qibla wakati wa kuchinja limeelezwa vizuri ndani ya Qur’an katika Suratul Al-Maidah, 5:4. “Wanakuuliza wamehalalishiwa nini? Sema mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri na mlichowafunza wanyama (kuwinda) na ndege wa mawindo (kuwinda).

 

Mnawafunza alichokufunzeni Mwenyezi Mungu. Basi kuleni walichokukamatieni na mkisomee jina la Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhesabu”.

 

Ufafanuzi wa aya hiyo kwenye sharti la kuchinja uliyomo ndani ya Qur’an unasema: “Na sharti ya kuchinja kwa madhehebu ya Kishafi ni moja tu – kumkata kwa upesi njia ya kupitia chakula na njia ya kupitia pumzi.

 

Mengine yote yaliyosalia ni Sunna kama (a) Kumuelekeza Qibla (b) Kusema Bismillah (c) Kisu kuwa kikali. Ama kusema kuwa (a) Mwanamke hawezi kuchinja sharti atahiriwe na (b) Kisu sharti kiwe kikali, haya ni maneno ya upuuzi. Mwislamu yeyote anayejua kuchinja, akichinja kinachojuzu kuliwa kitaliwa.

 

Sunna maana yake ni kitu au jambo ambalo ukiacha kulifanya si dhambi na wala ukilifanya halikuongezei thawabu yoyote. Hivyo, kuelekeza mnyama Qibla ni sunna tu, kinyume na baadhi ya Waislamu wanavyofikiri, pia kutamka Bismillah ni sunna tu wala si faradhi yaani (jambo la lazima).

 

Kwa ufafanuzi huu unaotokana na vitabu vya Kiislamu, kumbe mtu yeyote anaweza kuchinja na kikaliwa. Je, leo ndivyo ilivyo?

 

Katika kitabu kiitwacho “Halal na Haram Katika Uislamu”, kilichoandikwa na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Ustadh Yusuf al-Qaradhawi, na kuchapishwa na Afroplus Industries Limited Dar es Salaam, pamoja na maelezo mengine, amefafanua vyakula vya kuchinjwa ambavyo ni halali kwa Waislamu.

 

Katika ukurasa wa 66, 68 wa kitabu hicho ninamnukuu: “Dhabihu wa Watu wa Kitabu- Ahlul Kitaab (Vichinjwavyo na Mayahudi na Manasara (Wakristo)” anasema:

 

“Tumeona vipi Uislamu umetia tashdidi na mkazo katika mambo ya kuchinja na namna gani umelishughulikia jambo hili, kwani washirikina wa Kiarabu na wengineo wanaofuata mila nyinginezo, wamejaaliya dhabihu (wanyama wachinjwao) kuwa ni katika mambo ya ibada na kuchukulia kuwa ni mambo yanayohusu itikadi na asili ya dini, wakawa wanaabudu kwa kuchinja dhabihu kwa miungu yao kwenye masanamu au kwa kutaja majina ya miungu yao wakati wa kuchinja.

 

Uislamu ulipokuja na kuona mambo haya, uliyabatilisha na kuyafanya hayafai na ukalazimisha lisitajwe jina lolote wakati wa kuchinja ila la Mwenyezi Mungu, na ukaharamisha vinavyochinjwa kwenye masanamu na mizimu na kila kinachochinjwa si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

 

Lakini Uislamu ulipokuja uliwakuta Watu wa Kitabu wanafanya kama yale wafanyavyo washirikina, na kwa kuwa wao asili yao ni Watu wa Tawhidi (yaani wenye kuabudu Mungu Mmoja tu) na ikadhaniwa kuwa baadhi ya Waislamu watawachukulia Mayahudi na Manasara kama wenye kuabudu masanamu na mizimu.

 

Mwenyezi Mungu alitoa ruhusa ya kula chakula chao na kuoa wanawake wao ili kuwa tafauti kuwatafautisha na washirikina, na akasema Mola Mtukufu; “Na chakula cha wale waliopewa Kitabu (Mayahudi na Manasara) ni halali kwenu” (Al- Maida, 5:5).

 

Kwa jumla, aya hii ina maana kuwa leo mumehalalishiwa vizuri basi msiharamishe Bahira wala Saiba wala Wasila wala Hami (wanyama waliokuwa Waarabu wakijiharimisha nao zama za Ujahili kama tulivyokwishaeleza nyuma), na mumehalalishiwa vile vile chakula cha wale waliopewa Kitabu kabla yenu katika Mayahudi na Manasara kwa mujibu wa asili ya  mambo ilivyokuwa.

 

Wala Mwenyezi Mungu hakukuharamishieni kabisa, na kadhalika chakula chenu ni halali kwao, basi na mle katika wanyama wanaowachinja au wanaowawinda na mna ruhusa kuwapa katika mnavyochinja na kuwinda.

 

Neno “chakula cha waliopewa Kitabu”ni neno lililokusanya jamii ya vyakula vyao – vya kuchinja (dhabihu) na vya punje punje (nafaka) an vinginevyo.

 

Vyote hivi ni halali maadamu hicho chakula chenyewe si haramu kwa Waislamu kama mfu, na damu ya kutiririka na nyama ya nguruwe, kwani hivi havijuzu kuliwa kwa itifaki ya wanazuoni wote ikiwa ni chakula cha watu wa Kitabu au cha Waislamu.

 

Sasa hapa kumebakia baadhi ya mas-ala ambayo yana umuhimu kwa Mwislamu kuyajua.

 

Je, unajua hatua inayofuata? Usikose toleo la wiki ijayo.

Daniel anapatikana kwa namba 0687 931313.

 

By Jamhuri