Chakula cha nyama, ni moja ya hitaji  katika  mlo. Hutumika  kama kitoweo sehemu mbalimbali kuanzia kwenye milo ya nyumbani, sherehe mbalimbali hadi sehemu kunakouzwa vyakula.Hata hivyo,suala  linalohusiana na uchinjaji wa wanyama kwa ajili ya chakula, limekuwa likileta matatizo na misuguano isiyo ya lazima katika jamii yetu Watanzania, na hivyo kusababisha  kero kwa watu wengine.

Mara kwa mara tunasikia migogoro ikiibuka sehemu mbali mbali za nchi yetu, pale inapotokea  mnyama amechinjwa kwa ajili ya chakula, na mtu ambaye kwa mtazamo wa baadhi ya watu  wasingetegemea kusikia amemchinja mnyama kwa matumizi ya chakula.


Kundi la kwanza la watu wa aina hiyo ni wafuasi wa dini ya Kiislamu, ambao, hudai kwamba wao ndiyo walioruhusiwa  na Serikali kuchinja wanyama kwa matumizi ya chakula cha watu wote. Dhana hii imekuwa fimbo ya kuwaadhibia watu wengine wasiokuwa Waislamu, wasio na fursa ya kujua au  kutafuta ukweli wa  jambo hilo, na hivyo kuwa sababu ya kundi  hilo kunyanyaswa na kukandamizwa kwa kutojua haki zao.


Kwa upande mwingine huzusha migogoro isiyo ya lazima katika jamii, pale jamii moja inapong’amua kwamba inanyang’anywa haki yake ya msingi na kundi ambalo limejipa haki hiyo kinyume na Katiba, sheria, kanuni na taratibu za nchi yetu yenye mchanganyiko wa imani kama Tanzania (Tanzania is a pluralism state). Binafsi, nimewahi kushuhudia migogoro ya aina hiyo huko Katoro, wilaya ya Geita Mwanza, ambako Mchungaji Ikiri wa Kanisa la TAG Katoro, alikwenda kwenye machinjio ya Serikali kwa ajili ya kuchinja  mbuzi kwa matumizi ya chakula akitaraji ndiko anakopatikana Afisa Mifugo ambaye angeweza kumkagua mnyama yule kama anafaa kwa chakula au la, yakamkuta.


Jambo hilo lilileta mtafaruku, kwa sababu Waislamu walitaka kuleta vurugu katika eneo hilo kwa madai kwamba kwa nini mtu mwingine asiye Mwislamu anachinja.


Sakata hilo lilimalizwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Katoro wa wakati huo kuwataka Waislamu wasijichukulie sheria mkononi, kama walivyotaka kwa sababu hakuna sheria yoyote katika nchi yetu,inayotamka rasmi kuwa Waislamu peke  yao ndiyo wanaoruhusiwa kuchinja.


Sehemu nyingine ni Isaka katika Wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga, ambako mgogoro uliibuka pale Waislamu walipotaka kupandisha kodi ya uchinjaji wa wanyama kwenye machinjio ya Serikali. Lakini wauzaji hawakukubaliana na ongezeko hilo na jambo hilo lilitaka kusababisha kitoweo cha nyama kukosekana.


BAKWATA-Isaka hutoa risiti  zenye muhuri wa Bakwata-Isaka kwa watu wanaochinjiwa wanyama na Waislamu,  baada ya kutoa pesa Tsh.1,000/= kama kodi ya uchinjaji  kama ambavyo Waislamu hao  wamepanga.Nakala za risiti za aina hiyo ziliwahi kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Wilaya Kahama, ambaye ndiye mwajiri wa Afisa Mifugo kwa utatuzi zaidi.


Katika Wilaya ya Misungwi, mkoa wa Mwanza, Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) lilitoa waraka uliokuwa umesambazwa katika sehemu mbali mbali za biashara,kwa wafanya biashara, Mahoteli, Biashara ndogo ndogo (Mama Lishe), Wakaanga Chips kwenye Baa, mjini Misungwi,  likionya mtu mwingine asiye kuwa Mwislamu kutoruhusiwa kuchinja wanyama.


Waraka huo wa tarehe 28 Machi, 2005, wenye kumb. Na BKT/MT/02/MSS,  uliosainiwa na Katibu wa Bakwata, Mtaa wa Misungwi, na nakala zake kupelekwa Kituo cha Polisi, Ofisi ya Afya Misungwi, Mtendaji wa Kijiji, Sungusungu na kwa Mwenyekiti wa Kitongoji  ambao una kichwa cha habari, ninakinukuu “UCHINJAJI HOLELA KWENYE SEHEMU ZENU ZA BIASHARA”, ulisomeka hivi:


“Husika na kichwa cha habari hapo juu. Baada ya ukaguzi uliofanywa na Baraza Kuu la Waislamu Mtaa wa Misungwi, umebaini kuwa katika sehemu zenu za biashara mmekuwa mkiendesha shughuli ya uchinjaji wa mbuzi, kuku, bila kufuata taratibu zilizowekwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania.


“Mmekuwa mkichinjiwa na watu ambao siyo wahusika na hata mmefikia hatua  kuuzia watu vitoweo ambavyo vimekufa yaani (mizoga),” inasomeka sehemu ya waraka huo.


“Kwa hiyo Baraza linapenda kuwataarifu wahusika ambao watakuwa wanahusika na uchinjaji katika maeneo yote yanayohusika. Wahusika hao watakuwa wanatoa stakabadhi kwa kila mtu watakayemchinjia. Na stakabadhi hizo zitakuwa na mhuri wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania.


“Pia patakuwa na watu ambao watakuwa wakipita kukagua maeneo yote yanayohusika. Utakapokutwa umejichinjia kiholela na huna stakabadhi, basi hatua kali zitachukuliwa dhidi yako” unaonya waraka huo.


Pamoj na onyo hilo katika waraka huo imetolewa orodha ya majina ya Waislamu waliokuwa wanatakiwa kuchinja maeneo yote. Lakini ukiyachunguza kwa makini majina hayo, utagundua kuwa yote ni ya  watu wanaoaminika  kuwa ni wafuasi wa dini ya Kiislamu tu.


Swali ambalo mtu yeyote angeweza kujiuliza ni kwamba kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu pombe ni dhambi. Ni kwa vipi uchinjaji huo Waislamu wanataka ukafanyike kwa misingi ya dini yao hata kwenye mabaa ambako vinauzwa vitu vya haramu kwa misingi ya dini hiyo? Wanataka kutwambia wanakwenda na kwenye baa? Kuna haramu wanazotumia siku hizi?


Hapa ndipo inapojitokeza hoja kuu  ya ni nani aliyeagiza kuwa ni Waislamu tu ndiyo wanaoruhusiwa kuchinja wanyama kwa ajili ya watu wote?


Je, ni Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama baadhi ya Waislamu wanavyosema? Je, kodi wanazozikusanya kwa ajili ya uchinjaji kwenye machinjio ya Serikali yaliyojengwa kwa kodi za Watanzania wote huku wakitoa risiti za Bakwata zinakwenda wapi?


Ni nani aliye bora zaidi ya mwingine katika nchi yetu? Je, kabla ya Uislamu kuja Wakristo walikuwa hawali nyama? Haya na mengine mengi ni baadhi ya maswali ya msingi ambayo mtu yeyote aliyekutana na manyanyaso yanayohusiana na uchinjaji wa wanyama angejiuliza. Je, unajua suluhisho la mgogoro huu? Soma JAMHURI katika toleo la Jumanne ijayo.

By Jamhuri