simbachawene-georgetopWiki iliyopita, Serikali ilisitisha kufanyika kwa mashindano ya vijana ya Umoja wa Michezo ya Shule za Msingi (Umitashumta) na ule wa shule za sekondari (Umisseta).

Waziri wa Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simbachawene, alitoa kauli hiyo kusitisha rasmi baada ya kuzagaa uvumi kwa siku mbili.

Mwaka huu michezo hiyo ya Umisseta ilipangwa kufanyika kuanzia Juni 13 hadi Juni 22 jijini Mwanza, ambayo ingechukua siku tisa wakati Umitashumta ilitarajiwa kuanza kufanyika Juni 25 hadi Julai 5 mwaka huu na ingechukua siku 10.

Simbachawene alisema wameamua kusitisha michuano hiyo ili kuweza kusimamia kwa ukamilifu utekelezaji wa agizo la Rais John Pombe Magufuli kuhusiana na suala la madawati mashuleni.

Alisema kuwa haiwezekani kufanyika kwa michezo hiyo ambayo ingegharimu fedha nyingi wakati wanafunzi wanakaa chini kwa uhaba wa madawati.

Hivyo basi, wanataka kutekeleza kwa wakati agizo lake la kila

mwanafunzi kuwa ameketi kwenye dawati ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Kusimamishwa kwa michezo hii, wanamichezo kwa ujumla wanakumbuka enzi za Waziri wa Elimu, Joseph Mungai, ambaye aliwahi kuyasimamisha bila sababu za msingi na kusababisha kutoweka kwa vipaji vya vijana.

Lakini ilikuja kutoa ahueni kwa Serikali ya Awamu ya Nne iliyofahamu kosa lililofanyika katika awamu ya tatu, ikarejesha michezo hii mashuleni.

Kufuta michezo hii bila shaka ni kufuta ndoto za vijana wengi waliokuwa wameanza kuonesha njia katika sekta ya michezo.

Michezo ni moja ya sekta ambazo zimeweza kutoa ajira nyingi kwa vijana hapa Tanzania na duniani kwa ujumla.

Zaidi ya wanamichezo 4,000 wameajiriwa katika sekta ya michezo, sasa kwanini Serikali isithamini michezo? Haioni mzigo huu ambao wamepunguziwa hadi leo waifute?

Michezo hii ya mashuleni ndiyo iliyoibua vipaji vya wachezaji lukuki ambao wamevuma katika ulimwengu wa soka na kuliletea Taifa heshima.

Kwa hili, tunaona kabisa Serikali imezika rasmi michezo, hivyo basi hata wizara yake haina mantiki kwa sasa kutokana na haijaliwi.

Kumbukumbu zangu zinaonesha nyota waliotoka katika michuano hiyo ni pamoja na Dua Said aliyeng’ara Simba, na leo amejiajiri kwa kufanya biashara zake kutokana na fedha alizopata kupitia mpira.

Tunawajua wachezaji wengi Watanzania ambao wana ajira zao kwa sasa, wanalipwa mishahara ya Sh milioni moja na zaidi kwa mwezi na Serikali inaingiza kodi, lakini walianzia kwenye mashindano hayo ya mashule.

Nyota wa Taifa hili, mfano Edibily Lunyamila, Nteze John Lungu, aliyeng’ara baadaye Pamba na Yanga na Simba; kwenye kikapu Ramadhani Dullah, hawa wote ni zao la Umisseta na Serikali haifahamu jambo hili na kufikia uamuzi huo?

Achana na hao, kuna Jacob Masawe anayevuma na Stand United ya Shinyanga, lakini amepitia Toto African ya Mwanza, Ndanda FC ya Mtwara na African Lyon ya Dar es Salaam na aliweza kujisomesha kupitia soka ila naye alionekana katika michuano hii.

Lakini waliotoka katika mashindano haya ni Filbert Bayi, Selemani Nyambui, Salehe Zonga, Salumu Telela, Juma Kaseja na wengine wengi walioliletea Taifa heshima.

Si kama nabeza tatizo la madawati mashuleni, ila lingeangaliwa aina ya kutatua tatizo hili, na sina imani kama tutamaliza tatizo hilo kwa wakati ama hadi Januari litakuwa limeisha.

Najua michezo ni michezo kwa ajili ya kucheza. Lakini ni ajira na chanzo kikubwa cha ajira, ndiyo maana wachezaji ambao hawajafika chuo kikuu hapa nyumbani na nje ya nchi, wanalipwa fedha nyingi kuliko wafanyakazi waliohitimu vyuo vikuu.

Acha na habari zote, kwa sasa Serikali inafaidika na kodi kupitia

sekta ya michezo kupitia mishahara ya wachezaji, kwanini isithamini kitu ambacho kinaiingizia fedha?

Angalia kwa wachezaji wa nje na wa hapa nyumbani wanalipa VAT kila mwezi kwa kila mmoja, na wanaingiza zaidi ya mamilioni kwa mwezi kupitia soka.

Kama imesitishwa kwa mwaka mmoja basi iwe kweli na mwakani irudi huku ikiwa na taswira mpya kwa vijana hawa Taifa la kesho watakaokuja kuleta heshima kubwa hapo baadaye.

Kwa hili, hakuna aliyependezewa nalo maana tunashindwa kuelewa wapi tunaelekea katika mustakabali wa tasnia hii ya michezo, maana maendeleo yanakuja katika nyanja nyingi.

Nchi kama Brazil, Argentina na Hispania zinafahamika kupitia michezo na hata uchumi wao upo juu…ni wachezaji ambao wamesababisha kukuza sekta hiyo.

Inashangaza kuona wizara husika kusema kuwa Serikali ina nia ya kuendeleza michezo, sasa kwa aina hii? Unajenga vituo vya michezo wakati mashuleni wanakosoma hawapewi kipaumbele hiyo michezo? 

Ni wakati wa kujitafakari mara mbili ili kurejesha heshima ya michezo. Wengi wanasema yote ni kutokana na mambo ya kisiasa, ila mimi sitaki kuamini hilo kuwa ni siasa, cha msingi kufikiria tena uamuzi huo na mwakani vijana wacheze kama tuna nia ya dhati kukuza michezo nchini.

By Jamhuri