Hivi karibuni kwenye gazeti hili tuliandika habari iliyohusu mtandao wa matapeli wa madini unaowahusisha polisi kadhaa jijini Dar es Salaam.

Tukaeleza kwa kina namna polisi hao wanavyoshirikiana na matapeli wa madini kuwaibia wenyeji na raia wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Tukaenda mbali zaidi kwa kuweka hata majina ya polisi hao na mahali walipo.

Katika nchi zenye kujali maadili, habari ile isingepita hivi hivi bila hatua za kinidhamu na kisheria kuchukuliwa. Au hata kama kuna mpango wa kuchukua hatua, basi umma ungeelezwa ni hatua za aina gani zinachukuliwa dhidi ya polisi hao. 

Lakini kama ilivyotarajiwa, hakuna kauli yoyote iliyotolewa na Jeshi la Polisi kuhusu tukio hilo licha ya Naibu Kamishina wa Jeshi la Polisi nchini kuuliwa na kuonesha kutojali!

Ukimya wa viongozi wa Jeshi la Polisi na ule wa viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, unathibitisha jambo moja muhimu, nalo ni kilio cha siku nyingi cha wananchi cha kuona Jeshi hili likivunjwa na kusukwa upya.

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni matokeo ya kusukwa upya kwa jeshi letu kutoka jeshi tulilorithi kutoka kwa wakoloni. Jeshi la kikoloni lilikuwa na vimelea vya kikoloni. Hilo lilithibitika kwa kile kilichofanywa na askari wa jeshi hilo mwaka 1964. 

Baada ya tukio hilo, uongozi shupavu wa juu wa nchi yetu ukaona hakuna namna, isipokuwa kuunda upya jeshi la kizalendo lenye kuzingatia weledi na mahitaji ya nchi na wananchi wake. Tangu wakati huo tumekuwa na Jeshi la kupigiwa mfano ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu. JWTZ limebaki kuwa Jeshi lenye faraja kwa Watanzania. Ile dhana au tafsiri halisi ya Jeshi la ‘Wananchi’ inaonekana bayana.

Bahati mbaya, kwa upande wa Jeshi la Polisi, mambo mengi ndani ya Jeshi hili bado yana vimelea vilevile tulivyorithi kutoka kwa polisi wa kikoloni na ndiyo maana watu wanaoitakia mema nchi yetu hawasiti kuiomba mamlaka inayohusika ilifumue jeshi hili ili kulipa muundo wenye kukidhi mahitaji ya Watanzania.

Polisi wetu bado wanaamini ili waonekane ni polisi kweli, basi sharti wawe wababe, wenye majibu ya jeuri, watesaji na watu walio juu ya haki za msingi za binadamu wengine.

Nitatoa mifano miwili kuthibitisha haya. Juzi, nikiwa naendesha gari eneo la Korogwe, Ubungo jijini Dar es Salaam, nilisimamishwa na polisi kwa ukaguzi wa gari. Kila kilichotakiwa – kuanzia leseni, vibali, tairi na mambo mengine yote – vilikutwa vikiwa barabara. Kuona vile, polisi akanirejeshea leseni na kuniamuru niondoke. 

Usoni alionekana kwenye ghadhabu. Nikamweleza kuwa polisi anatakiwa baada ya ukaguzi wote huo na kubaini sina dosari mimi na gari, anishukuru na pengine ‘anisifu’ na anitakie safari njema maana nimekamilisha kile kinachotakiwa kisheria. 

Yule polisi akaona kama nimemdharau kwa ‘kumfundisha kazi’. Akanitazama kwa jeuri na kusema: “Wewe ndiye unayepaswa kunishukuru kwa kukuachia uendelee na safari yako!’ Kwa hilo jibu pekee, nikajua hiki chombo kinahitaji muundo mpya utakaotokana na mitaala mipya vyuoni!

Hili la usalama barabara linaweza kuwa dogo, lakini tujiulize hii ‘furaha’ wanayoipata baadhi ya wananchi wanaposikia polisi wameuawa kwenye matukio ya ujambazi au ajali!

Ndugu zangu, ‘furaha’ hii ya wananchi imeficha jambo kubwa ambalo wetu wetu, hasa viongozi wanataka kujifaragua kuwa hawalijui. Wanalijua sana lakini nafsi zinawasuta kusimama hadharani kueleza chanzo cha ‘furaha’ hiyo ya wananchi.

Huhitajiki utafiti wa ‘Tweweza’ kutambua kuwa wananchi wengi wanawachukia polisi. Wala hatuhitaji wataalamu kutoka nje kutueleza ni mambo gani yanayowafanya wananchi wawachukie polisi.

Polisi wetu wamekuwa ni watumishi wa kuwaonea wananchi. Sisi tulio kwenye vyombo vya habari kila leo tunapata matukio mengi ya polisi wanaowaonea wananchi.

Naomba nitoe mfano wa tukio moja kati ya manane ya uonevu unaofanywa na polisi niliyopokea kwa miezi miwili tu! 

Kijana mmoja alikamatwa na polisi wa kituo cha Wazo Hill Dar es Salaam akituhumiwa kujihusisha na ujambazi wa kutumia silaha. Ni kijana mdogo ambaye muuza duka maskini. Akawekwa rumande kwa masharti ya kuachiwa baada ya kuwapa polisi Sh milioni 1.5. Amekaa siku tatu fedha hazijapatikana. Rafiki zake wanaona mwenzao anafia rumande. Siku ya nne wakawa wamechangishana na kupata Sh 800,000. Wakazipeleka. Polisi wakagawana. Akaachiwa huru kwa masharti ya kumaliza kulipa deni la Sh 700,000.

Nilipopata taarifa nikawasiliana na viongozi wa Polisi Wazo Hill na hao polisi ‘wahuni’. Nikawasiliana na uongozi wa juu Kanda Maalumu ya Dar es Salaam. Wale polisi wakaona mambo yameshaharibika. Siku iliyofuata wakafanya walichoweza, zile fedha zikarejeshwa. Hawakuridhika, bado wakaahidi kumshughulikia kijana huyo kwa kuhakikisha anabambikiwa kesi nyingine. 

Nami nimelifikisha suala hili kwenye uongozi ngazi za juu na nimeapa kuhakikisha huyu kijana haonewi. Polisi hao wapo. Hawana wasiwasi pengine kwa kutambua kuwa kwa muundo huu wa Jeshi lao, hawawezi kufanywa kitu.

Polisi kadhaa si rafiki wa raia. Wamegeuka kuwa waonezi wakuu wa wananchi, hasa wanyonge. Wakiwakamata watuhumiwa huwapiga hata kama anayekamatwa haoneshi namna yoyote ya ukinzani. Sare za polisi, kwa wananchi kadhaa sasa ni alama ya dhuluma, uonevu, matusi, udhalilishaji, wizi, ujambazi, utapeli na matukio mengine mabaya.

Polisi hawatendi wajibu wao kwa haki. Kesi nyingi, hasa za makabwela zinavurugwa kuanzia ngazi ya polisi. Hivi juzi mwananchi mmoja mfugaji, mkazi wa Mkoa wa Pwani, alivamiwa. Akaporwa ng’ombe zaidi ya 50; fedha taslimu Sh milioni 48; mkewe akatekwa na kwenda kubakwa kwa miezi kadhaa. Wahusika wanajulikana, lakini polisi walipofungua mashitaka, wakaona mbinu nzuri ni kumwepusha mhusika mkuu kwenye tukio hilo. Maskini huyo ambaye hata kusoma hajui, kesi yake imetupwa kwa sababu tu ya ‘makosa’ yaliyofanywa na polisi kwenye mashitaka.

Katika hali ya kawaida ilikuwa polisi wanaofikwa na matatizo, wananchi waungane kuwasaidia. Polisi wanaojeruhiwa au kuuawa, ilipaswa wananchi watokwe machozi ya huzuni, na si kufurahia kama ilivyo sasa. Polisi wamebaki kuliliwa na ndugu zao pekee.

Hili jambo, hata kama tutajifanya hamnazo kwa kudhani halijulikani sababu zake, ukweli ni kwamba linajulikana. Wananchi wamepoteza imani kwa baadhi ya polisi. Wananchi wanao miongoni mwa polisi wamo wahuni ambao wanachojua ni kuchuma tu fedha.

Haya yanapofanywa, lakini yakatazamwa na wakuu wa Jeshi hilo pamoja na viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, yanachochea hasira za wananchi kwa walinzi hawa wa amani.

Wananchi wanapoona polisi wanakuwa wa kwanza kuiba au kunyofoa mali wakati wa ajali za magari au moto, wanazidi kuwachukia.

Wananchi wanapohudumiwa kwa matusi, kejeli au kudhalilishwa, hawawezi kutoa ushirikiano wowote pindi polisi wanapofikwa na mambo mabaya.

Polisi wanaposhiriki utapeli-wanapowasaidia matapeli kuwatapeli wageni wanaokuja nchini, wanaeneza sifa mbaya ya nchi yetu. Wanapolia ugumu wa maisha, nani kawambia makabwela ndio wa kumaliza shida zao?

Ukiyatafakari haya na mengine mengi, unaona hakuna namna nyingine, isipokuwa kuvunjwa na kuundwa upya kwa Jeshi la Polisi ni jambo lisilohitaji mjadala mrefu.

By Jamhuri