Wiki iliyopita nimehitimisha makala iliyokuwa ikiwasihi Rais John Magufuli na Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, kujenga wafanyabiashara nchini. Nimeandika makala hii katika matoleo matano yaliyopita, na nashukuru tayari maandishi yangu yamezaa matunda. Nilianza kuandika makala hizi baada ya Rais Magufuli kuwazuia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wasiwakadirie kodi kubwa isiyolipika wafanyabiashara.

Dk. Mpango naye amewazuia TRA kufunga biashara ya mtu yeyote isipokuwa kwa amri maalumu ya Kamishna wa TRA na biashara itafungwa kwa wakwepa kodi sugu pekee. Historia ya nchi hii katika biashara ni ya kusikitisha. Ni kwamba tangu tunapata uhuru, nchi yetu ilitangazwa rasmi kuwa ni ya wakulima na wafanyakazi. Kwa hiyo, wafanyabiashara wakawa raia daraja la pili.

Sitanii, ni kwa bahati mbaya hata mwaka 1987 Tanzania ilipoingia katika Mpango wa Kurekebisha Uchumi wa Benki ya Dunia (WB) uliojulikana kama Structural Adjustment Programs (SAPs) mpango huu ulishughulikia zaidi kupunguza wafanyakazi serikalini, lakini si biashara. Wawekezaji wa kutoka nje wameanzishiwa Kituo cha Uwekezaji (TIC), ila wazawa hadi wiki iliyopita hawakuwa na chombo chochote cha kuwashauri kibiashara.

Nafahamu na nimeguswa na uamuzi wa TRA baada ya kuandika makala kwa wiki tano mfululizo juu ya uanzishaji na uendeshaji wa biashara hapa nchini, kuna jambo limefanyika. TRA wiki iliyopita imeanzisha Kituo cha Ushauri kwa Walipakodi Dar es Salaam. Ni kituo cha kwanza tangu nchi hii ipate Uhuru, mwaka 1961.

Kuna mpango wa kufungua vituo kama hivyo Dodoma, Mwanza, Arusha na Mbeya. Naamini uamuzi huu ni wa busara na hii imeimarisha nia yangu ya kuandika masuala yanayohusiana na uanzishaji na uendeshaji wa biashara nchini.

Wiki iliyopita nilieleza nia ya kuandika kitabu kuhusu ‘Jinsi ya Kuanzisha Biashara Tanzania.’ Nimepata simu nyingi. Leo naomba nianze na mada ya kwanza juu ya uanzishaji na uendeshaji wa biashara nchini Tanzania. Ni kwa bahati mbaya kuwa elimu ya biashara hapa nchini iko kwa kiwango cha chini mno.

Sitanii, ingawa shule nyingi zilikuwa na mchepuo wa biashara miaka ya nyuma (Book Keeping and Commerce), bado wahitimu wa masomo hayo hawakupata fursa ya kufanya biashara. Hawakufanya biashara si kwa kupenda, bali kutokana na mazingira yaliyokuwapo hapa nchini. Ni bahati mbaya kuwa nchi hii kila anayeamka asubuhi anafikiri anaweza kuanzisha biashara.

Kuna msemo wa ‘ku-copy na ku-paste’. Biashara nyingi zinafanyika kwa Watanzania kuangalia nani anauza na kupata nini. Ukianzisha kibanda cha kuuza maji, siku mbili zijazo unakuta watu watano wengine pembeni mwako wanauza maji. Ukikaanga vitumbua, kesho wote wanakaanga. Angalia sasa mradi wa bodaboda. Kila mwalimu anataka kununua bodaboda.

Leo nataka kuanza na wazo la msingi. Ukitaka kuanzisha biashara unapaswa usiingie kichwa kichwa. Kuanzisha biashara ni sawa na kujenga nyumba. Inapaswa kama una nia ya kuanzisha biashara kuanzia hatua ya kwanza ambayo ni KUPATA WAZO. Unapaswa kupata wazo la biashara unayopaswa kufanya. Kwa mfano ukasema nataka kuuza saruji.

Ukipata wazo la kuuza saruji, ni lazima ujiulize maswali yafuatayo:- Saruji utaiuzia wapi? Eneo gani lina biashara ya saruji? Muda gani mzuri wa kufungua duka la saruji? Utajenga duka lako au utakodisha? Kodi ya pango ni kiasi gani? Saruji yenyewe inauzwa wapi? Washindani wanaouza saruji tayari na watarajiwa ni wangapi? Wanauza shilingi ngapi? Inauzwa kupitia kwa wakala au moja kwa moja kutoka kiwandani? Bei ya jumla ni shilingi ngapi? Bei ya rejareja ni kiasi gani?

Kuuza saruji unahitaji leseni ya aina gani? Unahitaji kufanya biashara kama mtu binafsi, kampuni au jina la biashara? TRA biashara ya aina hiyo unayotaka kuifanya inaitoza kodi kiasi gani? Ni vibali vipi vingine unavyopaswa kuwa navyo? Kuna malipo utadaiwa na serikali za mitaa au kijiji? Una mtaji kiasi gani? Unahitajika mtaji kiasi gani? Una akaunti ya benki? Usafiri upi unatumika kusafirisha mzigo na unapatikana wapi? Ulinzi wa duka lako utakuwaje? Huduma ya chakula, maji na choo katika sehemu unayoanzisha biashara ipo? Ni muda gani unapaswa kwenda TRA kuomba kukadiriwa kodi? Maswali haya na mengine kwa lugha ya kawaida unaweza kuyaita Mpango wa Biashara (Business Plan).

Kuanzisha biashara ni sawa na kujenga nyumba. Maswali hayo na mengine, ni sawa na ramani ya nyumba. Ni kwa mantiki hiyo nasema kila biashara inaanza na wazo, ambalo linafanyiwa kazi sawa na ramani ya kujenga nyumba. Je, unafahamu kinachofuata baada ya hapo? Usikose nakala ya JAMHURI wiki ijayo.

By Jamhuri