Waswahili wanasema kwamba ukimwona mwenzio ananyolewa, usilete maneno isipokuwa anza kutia maji kwenye nywele zako na kukaa mkao wa kunyolewa.

Hayo ndiyo yaliyojiri Ijumaa ya Machi 4, mwaka huu kwa Balozi Ombeni Yohana Sefue, aliyekuwa akishangilia wakati wenzake wakinyolewa, naye kunyolewa.

 Nikumbushe kwamba wiki mbili zilizopita niliandika makala nikimshukuru na kumtia moyo Rais Magufuli kwa kutumia usemi wa Kihaya wa ‘kwatilaho’ wenye maana ya ‘endelea na msimamo huohuo’ katika jukumu au mtindo, wa kuifanya kazi yake ya ukuu wa nchi, mtindo wa kutumbua majipu.

 Nilisema kwamba Rais Magufuli anafanya kazi hiyo bila kuonesha unafiki, hajali kwamba fulani anamfahamu na hivyo kumwacha aendelee na uchafu anaoweza kuwa nao ndani ya jamii, wala kujali mtu anayejipendekeza kwake hata kama mtu huyo anafanya mambo yaliyo machafu kwa jamii.  Kwake Magufuli jipu ni jipu hata kama limekaa mguuni kwake, ni lazima litumbuliwe tu.

Moyo wa aina hiyo wanao watu wachache, walio wengi wanataka uchafu uonekane kwa wengine walio mbali na wao, lakini uchafu ulio karibu unalazimishwa kuonekana ni usafi au kufumbiwa macho na kufanywa hauonekani.

Tabia hiyo ya kinafiki ndiyo iliyoidumaza nchi yetu kwa kuifanya iwe na mambo mengi machafu yaliyo kama spidi gavana katika kasi ya maendeleo yake. Kwa hiyo, Magufuli alichoamua kukifanya ni kuichomoa hiyo spidi gavana ili kuangalia kama kasi ya maendeleo ya nchi inaweza kuwa katika hali yake inayotakiwa.

Balozi Ombeni Yohana Sefue, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, alikuwa mtu aliyeanza kuuona mtindo wa Rais Magufuli wa kutumbua majipu kama sehemu ya wajibu wake, hiyo maana yake ni kwamba utumbuaji majipu usingeweza kumgusa yeye kwa vile si rahisi mtu kujitumbua.

Kazi aliyoamini kwamba atabaki na kuendelea nayo ni ya kuutangazia umma wa Watanzania ni majipu gani yametumbuliwa, kazi aliyokuwa akiifanya kwa mbwembwe nyingi na kujiamini kulikopitiliza. Kweli Sefue aliusahau usemi wa Baba wa Taifa wa kwamba cheo ni dhamana.

Wapo wanaodhani kwamba Balozi Sefue hakutumbuliwa jipu ila Rais kafanya utaratibu wa kawaida wa kuwabadilisha nafasi za kazi wasaidizi wake. Hilo ni wazo ambalo linashindwa kuingia kichwani mwangu. Kweli, Rais anaweza kufanya mabadiliko ya nafasi za kazi kwa wasaidizi wake, lakini hafanyi hivyo bila sababu.

Kawaida ni kwamba mabadiliko yoyote yanayoweza kufanyika kwa utaratibu huo yote yanalenga katika ufanisi, kuleta au kuboresha ufanisi. Kwa maana hiyo, yanapofanyika mabadiliko ya aina hiyo ni lazima ieleweke kwamba kuna mahali ambako mambo yamesuasua. Kwa hiyo hali hiyo ya kusuasua yenyewe tu ni jipu tayari.

Rais anaweza kufanya mabadiliko ya nafasi za kazi kwa wasaidizi wake kama njia ya kuondoa jipu au kuzuia jipu lisijitokeze katika nafasi hizo anazozifanyia mabadiliko. Kwa hiyo, mtu hawezi kujisifu kwamba kaondolewa kwenye nafasi ya kazi kama njia ya kuonesha uwajibikaji wake uliotukuka, labda itokee kwamba yeye anaomba kupumzika.

Lakini kuondolewa kwenye nafasi ya juu na kushushwa kwenye nafasi ya chini au kuambiwa kwamba asubiri kupangiwa nafasi nyingine, huko ni kuonekana kwamba nafasi aliyokuwa nayo hakuitendea haki, kwa ufupi huko ndiko kutumbuliwa jipu.

Haiwezekani jipu likatumbuliwa na kuanza kujitapa kwamba limetumbuliwa kwa vile linapendwa sana, jipu linatumbuliwa kwa vile halitakiwi, jipu ni uchafu katika mwili wa binadamu. Jipu linaufanya mwili uwe katika hali mbaya kiafya, kwa hiyo kuondolewa kwake ni nafuu katika mwili.

Kwa maana hiyo, Rais Magufuli ni lazima kaona kwamba kasi anayoitaka kwa kiasi fulani ilikwamishwa na aliyekuwa kiranja namba moja katika Ikulu yake, na hivyo kuona hakuna njia nyingine isipokuwa kumwondoa mtu huyo kwenye nafasi hiyo. Kwa ufupi ni kwamba Sefue alikuwa jipu lililomkwaza Magufuli.

Kama ilivyozoeleka, tukimwona Balozi Sefue akijitokeza kwenye vyombo vya habari na kutangaza kwa madaha kwamba watu fulani wametumbuliwa, yalikuwa majipu, basi nilidhani kwamba hata hilo la kutumbuliwa yeye angelitangaza vilevile na kwa njia ileile, lakini badala yake nilimwona JPM mwenyewe akilisema hilo kwa kutueleza kwa njia nyingine kwamba huo ndiyo uliokuwa mwisho wa Sefue kujionesha kwenye vyombo vya habari akiushadidia utaratibu wa kutumbua majipu.

Niliona Rais Magufuli akijaribu kumpaka mafuta Sefue kwa mgongo wa chupa wakati akitangaza kumtumbua, kwamba Sefue alikuwa mchapakazi mzuri; kweli kamstahi. Hapo yapo mambo mawili yanayopaswa kuangaliwa. Iweje mchapa kazi hodari aondolewe kwenye nafasi ya uchapazi na kuwekwa mtu mwingine wa kujaribu ambaye ndiyo kwanza anajifunza kazi hiyo?

La pili ni kwamba mchapakazi anaweza kupandishwa na siyo kuteremshwa, tena linapotokea hilo ni kwamba apoondolewa tayari anakuwa amepangiwa nafasi nyingine ya kiutendaji anayopewa mara moja siyo kusema atasubiri kupangiwa.

Hapa tutaona kwamba kazi iliyobaki ambayo Sefue angeweza kupangiwa, kama kweli Magufuli angekuwa amefurahishwa na uchapazi wake, ni ya umakamu wa rais au uwaziri mkuu. Nje ya nafasi hizo mbili kazi yoyote atakayopewa Sefue, kama ipo, ni ya kushushwa ngazi na siyo kupandishwa.

Tangu lini uchapakazi mzuri ukamfanya mtu ashushwe ngazi? Lile la kwamba yeye Sefue alikuwa kwenye nafasi hiyo kwa awamu iliyopita, kwa maana ya kwamba Magufuli alipaswa kuingia Ikulu na safu mpya ya watumishi kuanzia kwenye nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi, siamini kama lina ukweli. Ni kwamba hii ni awamu mpya lakini inayoendeleza Serikali ileile ya awamu zote.

Ingekuwa kwamba inaingia Serikali nyingine, kama ilivyo katika baadhi ya nchi, kwa maana ya chama kingine mbali na CCM kuchukua madaraka ya kuongoz nchi, hapo ningelielewa jambo hilo. Lakini katika Serikali ileile ya chama kilekile bado siuoni umuhimu wa rais anayeingia madarakani kufanya mabadiliko makubwa, ila anaweza kufanya mabadiliko mahali anapouona udhaifu katika uwajibikaji. Hilo ndilo lililofanyika.

Ila kitu ambacho naweza kumshauri Rais Magufuli ni kwamba mahali anapoona udhaifu na kulazimika kupafanyia mabadiliko, kwa maana ya kutumbua jipu, hana ulazima wa kujisumbua kupasemea, ni kuchukua mtu mwingine na kujaza nafasi basi. Nchi hii inao watu wanaokaribia milioni 50, ni idadi kubwa sana ya watu, hakuna mtu mwenye nafasi ya kudumu. Huu siyo ufalme.

 

[email protected]

0784 989 512

By Jamhuri