2 Rais Kikwete akiongea na Viongozi wa CCM Mkoa Dsm Leo jijiniImenichukua takribani wiki mbili kutafakari kauli ya Mwenyekiti wa NLD, Dk. Emmanuel Makaidi, ambaye ni miongoni mwa wenyekiti wenza wa vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
  Katika mkutano na waandishi wa habari, Dk Makaidi akiwa na wenzake, alidai kwamba “Oooh kuna mipango ya kumfanya Rais Kikwete akae madarakani mpaka mwaka 2017.”


Kwa umri wake, Dk. Makaidi na ukilinganisha na usomi akiongozana na wenyeviti wenza wenzake, Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi), akadiriki kusema hayo mwishoni mwa mwezi na kuonekana kama anampakazia Rais Kikwete.
Lakini kwa uungwana na kuonesha ukomavu katika uongozi na kidemokrasia, Rais Jakaya Kikwete amefikia mahali amesema ikifika kipindi chake cha ukomo wa urais wake Oktoba, mwaka huu, “Nitaondoka.”


Kiko wapi? Kauli ya Rais Kikwete maarufu kama JK aliitoa Ijumaa ya Mei Mosi mbele ya maelfu ya wananchi waliohudhuria Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani, iliyofanyika kitaifa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, mkoani Mwanza.
Mbali ya maelfu hayo ya wafanyakazi, ikumbukwe tu kwamba pale jukwaani JK alizungukwa na vigogo mbalimbali wa Serikali yake, walikuwako pia wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)-chama tawala.


Unadhani walikuwa hao tu? Hapana, walikuwa majaji na mabalozi wa mataifa mbalimbali na Rais kwa mbwembwe akawataja wazee wenzake ambao walikaa kwenye mkutano mmoja na waandishi wa habari na kudai ‘eti JK anatengeneza mbinu za kmuendelea kuongoza.”
Ngoja nikupe nukuu ya JK aliyoitoa siku hiyo, “Jana niliwaona wazee fulani (hakuwataja majina), hivi sijui wamepagawa na nini? Wanasema ooh Rais ana mpango wa kujiongezea muda madarakani. Mimi nasema uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani utafanyika Oktoba, mwaka huu.”
Bila shaka Rais Kikwete alikuwa anakata mzizi wa fitina uliotangazwa na viongozi wa Ukawa, ambayo wamekuwa wakiyatoa kwa nyakati tofauti. Aah jamani!


Lakini, nimwambie tu Rais JK madai hayo ya Ukawa hayako akilini mwao tu, pia yapo kwa wananchi wanaofuatilia masuala mbalimbali ya nchi ambayo sasa yametokea kuteka akili za watu wengi.
Unajua kwanini Rais JK hawa jamaa walifikia kusema hayo? Ni kwa sababu wanaona kuwa chama unachoongoza, chenye mtandao mkubwa wa wananchi mpaka leo, hakijatangaza ratiba ya kupata wagombea na hasa nafasi ya mrithi wako?
Hawaendi mbali, wanarejea uteuzi wako wewe uliofanyika Mei 4, 2005. Kwamba ikiwa leo Mei 12, 2005 hata dalili za kufanyika vikao vya wazi kama vile vya NEC havisikiki, ndiyo maana wanahisi hivyo kwamba eti unataka kuendelea kukalia kiti hicho.


Pia wanarejea kasi ya Tume ya Uchaguzi (NEC) kuandikisha daftari jipya la wapiga kura katika mikoa 30 ya Tanzania.
Unajua Rais ulifanya kazi kubwa kuongeza mikoa minne, hivyo kufikia idadi ya mikoa 30. Huku Tanzania Bara uliongeza mikoa ya Simiyu, Njombe, Katavi na Geita wakati mtangulizi wako, Benjamin Mkapa, yeye kwenye utawala wake aliongeza mmoja tu wa Manyara.
Sasa kama mpaka sasa mikoa mitano NEC haijamaliza kusajili wapigakura, itakuwaje safari ya kumaliza mikoa 25 ikiwamo mitano ya Tanzania Visiwani? Ndiyo maana wanaona kwamba muda wa Uchaguzi Mkuu utafika, na wenye haki ya kupiga kura hawajasajiliwa.


Sasa ushauri wangu kwa Rais Kikwete ni mmoja tu, ili kukata vilimilimi vya Ukawa na wananchi ambao wanakupakazia huku mtaani kwamba eti unataka kuongoza muda, ni kuiwezesha NEC ya Jaji mstaafu Damian Lubuva isajili Watanzania wenye sifa za kupiga kura.
Wakimaliza na kupiga kura, bila shaka utakuwa na amani na kuonesha ukomavu wa kuongoza nchi badala ya watu kuanza kufikiria kama yale yanayofanywa na baadhi ya viongozi wa nchi jirani.
Rais JK usikubali hilo hata kidogo. Usiwasikilize Ukawa, ikifika Oktoba jiendee zako kijiji Msoga, Bagamoyo mkoani Pwani ukatafakari kazi zako unazoota kama vile kufuga na kufundisha kama ulivyopata kusema huko nyuma.

By Jamhuri