Nimefurahishwa sana na tamko la Mkuu mpya wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Raphael Muhuga, alilolitoa Ikulu Septemba 26, mwaka huu, mara tu baada ya kuapishwa kwake kushika wadhifa huo.

Napenda nimnukuu “…Tunataka vijana waoneshe UZALENDO wa nchi na wawe walinzi wazuri wa mali za umma”. Huku ni kuonesha uchungu wa hali mbaya ya vijana katika nchi. Hakuna uzalendo na wala hakuna uchungu kwa kulinda mali ya umma katika Taifa hili wakati huu. Neno hili UZALENDO kwa Kiingereza ni “PATRIOTISM” na lina asili ya Kigiriki “patriotes” (wa nchi moja nawe). Sikuweza kutafsiri sawa sawa hicho Kigiriki.


Lakini kwa ujumla wake ni moyo au hali ya utayari kufia nchi yako – iwe Warusi, iwe Wamarekani hata akiwa mweusi (kama mimi Mngoni wa Litapwasi kule Songea), iwe Mjapani, na kadhalika wao kwa umoja thabiti wamejengeka kiuzalendo. Uzalendo hauna nafasi yoyote ya dini wala ya rangi. Cha muhimu ni wa nchi moja ile ile. Kwao la msingi ni kufia nchi yao (motherland), na si vinginevyo.


Walifikiaje hatua namna hiyo ya kujitambua ni wa nchi moja, wa Taifa moja na wa uraia mmoja? Si jambo la kulala Mtanzania, kuamka mzalendo, la hasha!. Uzalendo unajengeka pole pole tokea katika familia hadikufikia katika utaifa.

 

Uingereza kwa mfano, si wote wale ni wa asili ya Celtic au Anglo-Saxons, bali wapo wenye asili ya Scotland, Wales, Ireland na wazaliwa wa Warumi walio watawala na Wafaransa; ndiyo sababu ukiwa kule utagundua wenyewe wakijisema huyu wa Kaskazini, Yorkshire; huyu wa Sussex; huyu wa Midlands au huyu wa Kusini, Southampton.

Tofauti zao zinatokana na lafudhi (accent). Ujerumani utakuta wa Bavaria-Kusini na wa Prussia-Kaskazini, na kadhalika.


Ubelgiji utakula wa kusini huongea lugha ya Kifaransa; wale wa kaskazini huongea Kiflemish (Kiholanzi). Marekani ndiyo mchanganyiko tunaouita mseto wa kimataifa –

Waingereza, Wafaransa, Wahispania, Wabantu, Wajerumani, Wahindi Wekundu na kadhalika.

 

Lakini mwote humo wananchi wao wana kitu kimoja (common denominator) na hicho ndiyo UZALENDO kwa nchi yao. Rangi kwao si kitu, asili (origin) ya walikotoka au wa dini gani siyo la maana. Kwao ni uzalendo ndiyo unaowatambulisha kuwa wa nchi hii au ile; wa taifa hili au lile.


Basi, Meja Jenerali Muhuga aliposema anataka JKT iwajengee vijana uzalendo wa nchi yao amelenga kuunda hali mpya kabisa katika mawazo ya vijana wa Taifa hili. Huko nyuma si kwamba hatukuwa na azma hiyo, la hasha! Tulikuwa nayo, bali kutokana na hali ya nchi inavyoenda siku hizi ndiyo ipo haja kubwa sana ya kujenga uzalendo miongoni mwa vijana ambao ni taifa la kesho.


Napenda kukumbusha hapa kuwa JKT tangu kuasisiwa kwake mwaka 1963 ilikuwa na dhana hiyo ya kujenga Taifa jipya lenye mwelekeo wa kuthamini na kupenda NCHI YA TANGANYIKA. Na kwa sababu hiyo liliitwa JESHI LA KUJENGA TAIFA! Chama cha Tanganyika Africana National Union (TANU) na Serikali yake viliona mbali sana, ndipo vikaamua kuanzisha JKT. Mbona wangeweza kuita jina jingine lolote lile? Kwa nini wakaita Jeshi la Kujenga Taifa?


Napenda kuwakumbusha wasomaji wangu maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere juu ya JKT alivyotamka pale Kambi la Mgulani Machi 31, 1964. Mwalimu akiwa Rais wa Tanganyika alifuatana na Mzee Abeid Amani Karume akiwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Walifika Kambi ya JKT Mgulani.

 

Pale Mwalimu alianza kwa kusema, namnukuu; “…Bwana President Karume …nadhani kwanza ningewaambieni kwamba tunaye ndugu yetu hapa President Karume na nilifikiri nitumie nafasi hii nije naye hapa kabla hajaondoka ili kusudi awaone na nyinyi vijana mpate nafasi ya kumwona. Nadhani kwanza Bwana President ungesimama vijana wako wakakuamkia”.

 

Baada ya utangulizi huo Mwalimu alisema, “Vijana, nadhani mnaelewa kwa nini mko hapa… mko hapa kwa ajili ya KUJIFUNZA KULITUMIKIA TAIFA LENU. Sisi, hasa watu ambao tumezaliwa na kukulia katika ukoloni tunalo zoea moja kubwa ambalo tuliambukizwa na wakoloni – tunajua sana kunung’unika ndiyo ilivyokuwa zamani, mambo yakienda vibaya tunamlaumu mkoloni, wengi sana tunayo mazoea yale ya kulaumu.


“Wakoloni wametufundisha jambo jingine baya – wamezitenga KAZI za nchi. Ziko kazi za kuvaa tai tu (white coloured jobs) na wavaa tai. Ziko kazi fulani wanazidharau. Na ziko kazi za watu wa kawaida za mikono, kulima, udobi, kusafisha viatu, hizi za watu wasiovaa tai.

“Sasa vijana nasema tumo katika jitihada kubadili upuuzi huu katika nchi yetu.

 

Na tumeunda kundi hili la kujenga Taifa. Kazi yako ya kwanza ni kujifunza kulitumikia Taifa lako. Ni nia ya Serikali kwamba hapa watapita watu wa aina zote hapa kesho na keshokutwa ndiyo mlango mkuu. Kama hakupita mlango huu hapa huingii mahali pengine sharti upitie kwanza mlango huu hapa…”


Nimetumia nafasi ndefu kunukuu yaliyosemwa na Baba wa Taifa Machi 31, 1964 kuonesha uzito alioupa Baba wa Taifa utaratibu mzima wa kulitumikia Taifa hili, akitaka sana mkazo uwekwe kwenye kuwajengea vijana moyo wa uzalendo. Vijana waache kunung’unika na waache kuchagua kazi. Ili kujenga chombo hiki kiutaratibu na kisheria, wakaazimwa wasomi wenye ujuzi kutoka wizara mbalimbali ili kujenga msingi wa chombo hiki kipya.

 

Mambo ya ndani aliazimwa polisi wenye vyeo vya Assistant Kamishna (ACP), Bwana David Nkulila kuja kuleta Utawala wa Sheria. Waliazimwa na Senior Superintendents wa Polisi (SSP) kama Bwana Saidi Magambo kuangalia ghala kuu (Q Master), Bwana Gladston Mwamlima kuwa Mkuu wa Shule (School Leader), mabwana waratibu wasaidizi wa Polisi (ASP) kuwa watawala kama mabwana Laurent Mtazama Gama, Nelson Levi Mkisi, na Eliyawinyo P. Njau.


Kutoka Wizara ya Elimu aliazimwa Mwalimu wa Sekondari wa Kuendeleza Elimu ya Kawaida (Education Officer) Bwana Francis Xavier Mbenna, kutoka Kilimo waliazimwa mabwana S. Kalinga (Agriculture Officer) na Bwana Lewis (Field Officer) kwa shughuli za ugani.

 

Kutoka Afya waliazimwa Dk. Jastin Omari na baadaye Dk. Hussein Lueno kwa tiba, kutoka Tawala za Mikoa waliazimwa mabwana Mathew Mhuto (PAS) na Ahmed Mohamed Massenga (OS) kusimamia fedha na rekodi za ofisi. Kutoka Ulinzi waliazimwa maafisa na MaNCO kadhaa kwa shughuli za ukufunzi kijeshi.

 

Mwanzo namna hii kwa miaka ile ya mwanzo wa JKT ilikuwa kuandaa msingi wa kiutawala katika chombo hiki muhimu kwa Taifa.Wakati shughuli za mafunzo zikiendelea, ikatungwa Sheria Na. 16 ya mwaka 1964 kuhalalisha uwepo wa chombo hiki katika nchi hii.

 

Vijana wa Jamhuri ya Tanganyika kwa mujibu wa sheria hiyo waliweza kuingia JKT kwa kujitolea na pia waliweza kuajiriwa kama watumishi wa kudumu. Ajira za watumishi wa kudumu zilianza kutolewa Julai 1964 kwa vyeo namna hii; askari wa kawaida walioitwa cadet guide viongozi walianzia cheo cha “Assistant Guides, Deputy Guides, Senior Guides na kukomea Chief Guides. Maafisa walianzia cheo cha Assistant Masters, Masters, Seniors Masters, Assistant Director na kileleni ni cheo cha Director.


Vyeo hivi viliigwa kutoka Jeshi la wataalamu Wayahudi, lakini kima cha mishahara (salary scales) kilifuatwa kile cha Jeshi la Polisi chenye alama za PG.


Tukiachia mbali mwanzo huo kiutawala, Sheria Na. 16 ya 1964 iliainisha wazi masharti ya kuingia katika JKT. Sifa zilizotolewa zilisema kijana yeyote anaweza kujiunga JKT alimradi awe na umri wa miaka 18 na asizidi miaka 25. Awe na afya timamu, awe mwanachama wa

Tanu Youth League (TYL) au ASP Youth League awe amemaliza elimu ya msingi. Kambi pekee iliyotoa mafunzo ya awali ya JKT ilikuwa Mgulani. Baadaye ilifunguliwa Kambi ya Ruvu kwa shughuli za kilimo na mifugo mwaka huo wa 1964.


Lakini kutokana na mushkeli wa maasi ya askari wa King African Rifles (KAR) Januari 20, 1964, basi azma ya kwanza ya JKT ilikuwa kuandaa vijana wengi kwa haraka ili wakajenge upya Jeshi la Ulinzi.


Kwa mtazamo huo, Machi 1964 vijana aliowatembelea Mwalimu pale Mgulani walikuwa wanaandaliwa kwenda kwenye ulinzi wa nchi. Mkupuo ule wa kwanza (1st intake) uliitwa Operation One Thousand, mkupuo wa pili uliingia Mgulani mwezi  Agosti, hawa waliitwa Operation Kujenga na mwezi Septemba mkupuo wa tatu waliitwa Operation Seven Hundred”.


Hawa wote baada ya kuhitimu walikwenda kujaza nafasi katika Jeshi la Ulinzi ambao wakati linaundwa walijulikana kama TR (yaani Tanzania Rifles – Bunduki za Tanzania), hatimaye Jeshi lile la ulinzi liliitwa rasmi Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanzia Septemba Mosi, 1964.

Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).


2026 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!