Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) linalojumuisha Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekosti Tanzania (PCT) na Kanisa la Waadventisti Wasabato (SDA), limenishangaza. Limenishangaza kwa lililolitoa hivi, kufuatia mkutano wake wa dharura uliofanyika Kurasini, Dar es Salaam, Machi 8 mwaka huu, ukiwahusisha maaskofu 117 wa makanisa mbalimbali nchini.

Wamenishangaza kwani katika tamko lao walianza vizuri wakisema vitendo vya kikatili vinavyofanywa dhidi ya makanisa,  vitisho na mauaji kwa viongozi wa Kanisa si kwamba vinafanywa na Waislamu wote, bali wachache. Wema wa kauli hiyo wameutia doa kwa hatua waliyofikia wakati wakizungumzia mgogoro wa nani anastahili kuchinja wanyama kati ya Waislamu na Wakristo, waliposema katika tamko lao la pamoja, “Wakristo wanaitaka Serikali iweke utaratibu wa kugawana machinjio na mabucha kati ya Wakristo na Waislamu ili kila Mtanzania awe huru kujinunulia kitoweo mahali anapotaka.”

 

Hapa ndipo waliponishangaza hata kuyakumbuka maneno aliyowahi kusema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipokemea ubaguzi miongoni mwa jamii, akisema ni dhambi mbaya sawa na kula nyama ya mtu ambapo mtu akishaila, anaizoea kiasi kwamba haiachi. Wakristo ni miongoni mwa waumini ambao ninaamini umakini wao, hivyo, pendekezo lao limekinzana na matarajio yangu kwao kwani nilitarajia waendelee kusisitiza jamii idumu katika upendo, bila kulipiza visasi na ikemee kwa dhati chuki na ubaguzi.

 

Sikutarajia kuwasikia wakipendekeza na kubariki dhambi ya ubaguzi na utengano miongoni mwa jamii. Kwamba Waislamu wawe na bucha na machinjio yao na Wakristo nao wawe na bucha na machinjio yao. Hilo sikutarajia litokee katika vinywa na vichwa vya maaskofu. Hapa nadhani nao wana maslahi binafsi.


Tamko hilo lililosomwa kwa kupokezana kwa wawakilishi wa taasisi hizo; Mwenyekiti wa CCT, Askofu Peter Kitula, Rais wa TEC, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Askofu Batholomeo Sheggah (PCT) kwa niaba ya Mwenyekiti wa PCT, Askofu David Batenzi, maaskofu walisahau kuwa kwa kubariki ubaguzi katika mabucha, linakuja tatizo la ubaguzi katika huduma mbalimbali za kijamii.


Huduma ni pamoja na shule, hospitali, barabara, maji, maduka na hata vyombo vya usafiri. Nimeshangaa maana maumivu ya kichwa huanza polepole. Kwamba tukianzia kwenye mabucha, tunaenda katika hatari ya jamii sasa kutaka Waislamu wawe na shule zao, vivyo hivyo kwa Wakristo.

 

Wakristo daladala zao, na Waislamu wawe na zao. Waislamu wawe na barabara zao na Wakristo nao barabara zao na kadhalika; hata visima vya maji. Ipo hatari tutake Waislamu wawe na vyao na Wakristo visima vyao. Ndiyo maana ninasema kwa hili, nimeshangaa maaskofu kutaka libarikiwe.

 

Hili sikulitarajia litoke kwa maaskofu kwani kama alivyosema Mwalimu Nyerere, dhambi hiyo ikibarikiwa miongoni mwa Waislamu na Wakristo kisha ikafanikiwa, itahamia ndani ya Uislamu na Ukristo wenyewe.

 

Nao Walutheri watatakiwa kuwa na bucha zao, daladala zao, vijijini vyao na shule na hospitali zao. Wakatoliki nao, Wasabato, Waanglikana na Wapentekosti nao hivyo hivyo. Kwa mwendo huo, tunakwenda wapi kama si kujichimbia kaburi ili kufurahisha watazamaji wa nje?

 

Tunakwenda wapi kama Waislamu nao watatafunwa na dhambi hiyo wakabaguana namna hiyo ndani yao wenyewe? Si siri tumekwisha. Ndiyo maana ninasema nimewashangaa maaskofu maana katu sikutarajia hilo litoke kwao. Wamenishangaza.

 

Hata hivyo, ninaungana nao kuhusu umuhimu wa jamii nchini kushirikiana kwa dhati na Serikali, kudumisha amani na upendo wa dhati watu waishi kwa amani bila hofu, chuki wala visasi.

 

Suala kwamba Serikali itamke Waislamu wawe na bucha zao, Wakristo bucha zao na hata wapagani au watu wa dini nyingine bucha zao, hakika sikubaliani nao na ndiyo maana ninasisitiza kwamba kwa hili, maaskofu kupitia Jukwaa la Wakristo wamenishangaza!


1360 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!