pg 1Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeingia kazini rasmi na kuahidi kushughulika na vitendo vyovyote vya kikatili vinavyoendelea hapa nchini, hasa mauaji yaliyotokea Mwanza na Tanga hivi karibuni.

JWTZ wameamua kuimarisha ulinzi nchini kote kutokana na matukio ya mauaji hayo, ambapo operesheni itaendela bila kukoma kuhakikisha watanzania wanabaki salama na kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali bila wasiwasi.

JAMHURI limezungumza na mmoja wa viongozi wa juu wa JWTZ, ambaye hakupenda kutajwa gazetini, anasema jeshi la wananchi limeingia katika operesheni maalum kuhakikisha Watanzania wanabaki salama na kwamba mauaji hayatokei.

“Tumeimarisha ulinzi katika maeneo ambayo matukio hayo ya kinyama yametokea, lakini pia katika mikoa yote tumejizatiti kuimarisha ulinzi zaidi. Tuko kazini muda wote, tutahakikisha kwamba wale wote waliohusika wanasakwa na kukamatwa,” anasema.

Chanzo kingine kutoka JWTZ kimesema wanaendelea kuchunguza taarifa za kiintelijensia na tayari wanazo taarifa za kutosha wasizoweza kuzichapisha gazetini ila mwisho wa hao wanaotenda maovu hayo umewadia.

“Tunajua hawa wanajaribu kupima ubavu wa jeshi letu, ila nakuhakikishia tuko imara. Tutawasafisha wote. Yaliyowakuta M23 kule DRC kwa uongozi wa jeshi mahiri la JWTZ yatawakuta hao wanaojaribu kuchezea amani ya Tanzania.

“Tumejiandaa vilivyo, tutatumia kila mbinu za kijeshi kuhakikisha tunawanasa. Kama wamejificha katika hayo yanayoitwa mapango ya Amboni, tutawafukizia hadi moshi kuhakikisha wanatunawapata. Haiwezekani, haiwezekani, haiwezekani… hawa sasa wamefika mwisho wao,” kilisema chanzo chetu.

JWTZ kwa kushirikiana na polisi wamepewa vifaa vya kisasa, ikiwamo vyombo vya usafiri na viona mbali vinavyobaini mtu alipo hata kama ni giza, kisema chanzo chetu na kusema kuwa wamechokoza sasa watakiona cha moto.

Mmoja wa majenerali anasema wataalam wa JWTZ wameamua kupambana na adui kwa mbinu za kivita kuhakikisha wanaondoa mzizi wa fitina. Anasema maelekezo yametolewa katika kambi zote za JWTZ nchini kuhakikisha ulinzi unaimarishwa.

“Kazi kubwa ya JWTZ ni kulinda mipaka yetu, ila sasa kama kumeanza kuwa na hayo matatizo yanayoanza kujitokeza, hatuna budi kuhakikisha kwamba ulinzi umeimarishwa zaidi, maana ni haki ya Watanzania kulindwa na jeshi lao. Kazi hiyo tumekuwa tunaifanya na tutaendelea kuifanya kwa nguvu zaidi,” anasema.

Afisa mwingine mwandamizi anasema katika kuhakikisha watuhumiwa wote wanakamatwa umewekwa mtandao nchi nzima, utakaowawezesha kudhibiti uhalifu huo na kuwakamata watuhumiwa wa mauaji ya Tanga na Mwanza na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Tarifa zaidi kutoka kwenye vyanzo vyetu ndani ya vyombo vya dola, zinasema suala la kuimarisha ulinzi, kwa sasa linaongozwa na JWTZ kwa kushirikiana na kikosi maalum cha kuzuia ugaidi.

Katika kipindi cha mwezi mmoja, yametokea matukio makubwa mawili ambayo yamehusisha mauaji ya Watanzania katika mikoa ya Tanga na Mwanza.

Matukio haya yamekuja takribani miezi 15 tangu litokee tukio ambalo lilihusishwa na ugaidi katika Mkoa wa Tanga.

Tukio lililotokea mkoani Tanga wiki iliyopita liliishitua nchini. Kutokana na tukio hilo katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu, pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi, Hamad Masauni walikutana katika uwanja wa mapambano Tanga.

“Ndugu zangu nawapeni pole kutokana na kuondokewa na wapendwa wetu… naomba kuwahakikisha sisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola tutahakikisha tunawatia nguvuni watu wote waliohusika na mauaji haya,”anasema Jenerali Mwamunyange.

“Tanzania inasifika kuwa na amani duniani kote, lazima hatua za kiusalama zichukuliwe haraka ili kunusuru amani yetu isichezewe…ni tukio la ajabu ambalo limegusa watu wengi wasio na hatia, tutasaidiana na wenzetu kuhakikisha wahalifu hawa wanapatikana,” anasema Jenerali Mwamunyange.

Kumekuwa na kasi kubwa ya watu kuchinjwa, ambapo watu takribani 20 wameuawa katika kipindi kifupi nchini. Watu wanane wakiripotiwa kuuwawa kwa kuchinjwa katika Kitongoji cha Mabatini, Kata ya Mzizima mkoani Tanga, huku tukio jingine likitokea Mei 10 katika Kijiji cha Sima, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza ambapo watu saba wa familia moja waliuawa.

Kitendo cha wajumbe wazito wa kamati ya ulinzi na usalama kuzuru Tanga wiki iliyopita, kilidhirisha uzito mkubwa ambao sasa suala la ulinzi limepewa na hasa katika kuwakamata wote waliohusika na matukio hayo.

By Jamhuri