Baada ya ushindi dhidi ya Waasi wa March 23 (M23), Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na Majeshi ya Umoja wa Mataifa (MUNUSCO) limesema hakuna kikwazo chochote cha  kuwaondoa waasi wa ADF- NALU  na FDRL.

Akizungumuza na JAMHURI mwishoni mwa wiki, Msemaji wa JWTZ, Luteni Kanali Eric Komba, alisema kikosi hicho kilipewa jukumu la kuungana na Jeshi Congo mjini Beni na tayari limefanya hivyo.

“Vikundi vyetu viko katika hali nzuri na vinaendelea kujipanga kutokana na maagizo kutoka kwa viongozi wao mjini Beni pia Jeshi letu la JWTZ linaendelea kupeperusha vizuri bendera yetu.

“Vikosi vyetu vyote vya Chapter 6 na Chapter 7 vinafanya kazi kwa umakini mkubwa na uadilifu uliotukuka na vimejipanga vya kutosha, kwa hiyo hakuna wa kuwazuia, hakuna kikwazo chochote kitakachosababisha washindwe kuwanyanganya silaha na kuwaondoa waasi wote nchini Congo,” amesema Luteni Kanali Komba.

Amesema hata Brigedi Maalum (FIB) iko katika hali nzuri kupambana Waasi wa Rwanda FDLR (Democratic forces for the liberation of Rwanda) na ADL, hivyo kuwataka wananchi wa Congo wategemee mambo mazuri muda si mrefu.

Amewataka wananchi wa Congo na Tanzania kutosikiliza propaganda zinazoenezwa katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa hali ni mbaya kwa Jeshi la MUNISCO.

Chanzo kingine cha habari kutoka Mjini Beni  kimelieleza JAMHURI kwamba JWTZ imepewa jukumu la kupambana na waasi wa ADF ambayo imendelea kutoa kichapo kikali  kwa waasi hao bila kupata upinzani.

“Huku hakuna kazi tumeendelea kutoa kichapo kwa waasi wa ADF, kila siku wanakimbia kwenda Sudan Kusini, mwanzo walikuwa katika Mlima Ruwenzori  tukawafuata huko huko nako wamekimbia,” amesema mtoa habari huyo.

Hata hivyo, mtoa habari huo amesema kwamba kazi ngumu  itabaki kwa waasi wa Rwanda (FDRL) ambao suala lao liko kisiasa, hivyo inakuwa vigumu kuwarudisha Rwanda hata kama watawanyang’anya silaha.

“Hili la waasi wa Rwanda liko katika hali ya kisiasa mno kwani hawa jamaa hata kama tukiwanyang’anya silaha kuondoka hapa ni mpaka Rais Paul Kagame akubali kuwasamehe, lakini kama  hatafanya hivyo wataendelea kubaki katika ardhi ya Congo,” amesema mtoa habari huyo.

Mtoa habari huyo amesema kutokana na kutulia kwa misukosuko ya vita sasa wako kwenye maandalizi ya kurudi nchini na kupisha askari wengine kujiunga na Brigedi hiyo kwani UN kukiongezea muda wa kukaa nchini humo.

Amesema kikosi  cha kwanza kinatarajiwa kurudi nchini Mei 30 hado Mei 5, mwaka huu na waliopangia kuondoka kwenda Congo wanatarajiwa kuondoka katika tarehe hizo.

Operesheni ya kuwanyang’anya silaha waasi wa FDRL,  na ADF – NALU ilianza mwaka jana ikiwa ni mwezi mmoja tangu kufurushwa kwa waasi wa kundi la M23 waliokuwa wakidhibiti baadhi ya maeneo na kuhatarisha usalama wa raia.

Kamanda wa kikosi kinachoendesha oparesheni hiyo, Carlos Dos Santos Cruz, amethibitisha kuwa oparesheni hiyo inafanyika umbali wa kilometa 90 Kaskazini Magharibi mwa mji wa Goma.

Serikali ya DRC imesema huu ni mwanzo wa shughuli ya kuyapokonya silaha makundi yote yanayozorotesha usalama Mashariki mwa DRC.

2898 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!