Viongozi Maziwa Makuu waufanye kwa uangalifu

 

Je, ulipata kujua undani wa kisaikolojia na mazingira-mali vilivyosababisha dunia kuingia kwenye Vita Kuu ya Pili miaka ya 1939-1945?

Kama unajua karibu tutafakari. Kama hujui naomba nikueleze kwa kifupi. “Sera ya huruma iliyofanywa na nchi za Marekani, Uingereza na Ufaransa kumbeba Mzungu mwenzao, Ujerumani, zilitengeneza uendawazimu wa kifashisti chini ya jinamizi ‘unazi’.

Baadhi ya Wajerumani ‘wapuuzi’ wakawa viburi na kudhani wangelipizia uharibifu walioupata katika Vita Kuu ya Kwanza. Hili likasababisha Vita Kuu ya Pili ambayo ilitisha kuliko vita zote duniani.

Naam, tukiwa tumejaaliwa na Mungu kuwa wasomi na wanahistoria wapembuzi, hatuna budi kujifunza masomo adhimu kutokana na Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kisha tukafanya ulinganishi mpana na anuai na mazingira yetu.

Kwa kiwango kikubwa historia ni mwalimu kiongozi! Yanayotokea katika nchi za Maziwa Makuu, hasa Rwanda na majirani zake yanahitaji jicho la tatu.

Rais wa sasa wa Rwanda, Paul Kagame, aliitwa shujaa mkubwa baada ya kutwaa nchi akiwa Kamanda wa Majeshi ya Rwanda Patriotic Front (RPF). Maana ya RPF ni ‘Baraza la Wazalendo la Rwanda.

Kwa kiasi kikubwa ushindi wake ulikuwa ni matokeo ya nguvu za Yoweri Museveni, Rais wa Uganda, ambaye aliamua kutafuna mamilioni ya walipakodi wa Uganda kumsaidia rafiki yake na mfanyakazi wake mtiifu Mnyarwanda aitawale Rwanda.

Hata hivyo, nguvu za Marekani na Uingereza zilikuwa na ushawishi mkubwa katika hilo, kwani walihitaji kumtengeneza kibaraka wao mpya wa ukoloni mamboleo baada ya kuwa wazi kuwa ‘kijana’ wao wa muda mrefu, Yoweri Museveni, alikuwa akielekea mwisho wa enzi zake – umri unamtupa.

Vikosi vya Umoja wa Mataifa vilivyokuwa Rwanda miaka hiyo ya 1990 chini ya Kamanda Mkanada, Romeo Dallaire, vilifanya rada ya RPF kuitwaa Rwanda na kuhakikisha inageuzwa ‘satelaiti’ ya wadhalimu wa Kimagharibi. Lilikuwa ni fumbo nzito sana mwaka 1994.

Ndugu msomaji, najua vizuri kuwa kama wewe ni Mwafrika mzalendo na mwenye uwezo wa kuelewa, tena usiyetumia maoni tu kuungana na upande wowote bali unayetumia upembuzi wenye utafiti na weledi utasikitishwa na ukweli ulioko kwenye makala haya.

Utafikiria kwa kina na kuogopa ukijiuliza, je, tumekosa nini Waafrika? Tumewapoka nini mataifa ya Magharibi sisi watu wa Maziwa Makuu? Kwanini sisi? Mpaka lini tutateswa hivi jamani?

Jibu lake ni dogo! Mpaka hapo utajiri wa rasilimali zetu utakaposhikiliwa na watu wa nje au kuporwa utakapoisha! Huu ni mtihani mkubwa ambao wataalamu wanauita laana ya kuwa na rasilimali, kwa kizungu – the resource curse.

Naomba ujue kuwa niyaandikayo humu ni matokeo ya utafiti ambao unaendelea. Nakuibia tu kile kilichomo kwenye ‘article’ ndefu ambayo inatarajiwa kuchapishwa kwenye jarida kubwa la kimataifa juu ya siasa za Afrika. Juwa kabisa kuwa haya ni matokeo ya utafiti na siyo stori au hisia. Ushahidi wa haya mambo ni mkubwa mno.

Mwaka 1994 wakati Kagame anaitwaa Rwanda alikuwa kwa muda mrefu kabla ya hapo mkuu wa upelelezi jeshini nchini Uganda. Kwa kifupi naomba ujue kuwa alikuwa ameishi akiwa ndiye mtu anayemuweka salama Rais Yoweri Museveni kwa kuhakikisha anazima na kutokomeza uasi na vitisho jeshini.

Kwenye nchi kama Uganda ambayo ilikuwa na matatizo ya kiukabila na mtifuano kuhusu madaraka, nadhani unaona Kagame alibeba umuhimu mkubwa kiasi gani kwa usalama wa rais!

Katika hili tunajifunza kitu kimoja kikubwa – huyu Kagame alikuwa mwaminifu mno! Alitumiwa akatumika! Angefaa kuwa kibaraka – agent. Hatari ni kwamba hakuwa raia wa Uganda, alikuwa mkimbizi Mnyarwanda, tena anayejulikana hivyo.

Je, kuna sheria duniani ya kumruhusu jasusi wa nafasi hiyo awe ana uraia wa kushadadia kihivyo? Alinde usalama wa rais na nchi kwenye nchi ya wengine huku akiwa amekimbizwa kutoka nchi yake isiyo na usalama? Hapana. Hapa kuna jambo ambalo hatulijui — alilolijua Museveni tangu enzi hizo.

Bila kujali  ni kiasi gani Kagame alikuwa si raia wa Uganda na elimu yake ikawa ndogo ya “Ntare sekondari”, lakini alipata kuwa mwana-usalama mkubwa anayeogopeka Uganda.

Jamani, Museveni alipata kuwa rais akitokea vichakani alikoendeshea mapambano yake kumng’oa Milton Obote. Je, wakati huo wote akiwa muasi alipata kumfunzia wapi Kagame ujasusi?

Je, Kagame alikuwa jasusi kiutaalamu au kwa namna ya kiunafiki tu kutekeleza matakwa? Hapa pana fumbo. Kizuri cha kujifunza ni kuwa mtu mwenye akili sana (intelligent) na msomi mzuri wa haja kwa kipindi hicho, mwanasheria Patrick Karegeya (kwa sasa ni marehemu), alikuwa ni msaidizi wa Kagame katika nafasi hiyo ya ujasusi.

Huyu Karegeya, aliyekuwa ndiye msiri toka nitoke na Kagame, amepata kunena kuwa sifa kubwa ya bosi wake ni kuwa alikuwa hasamehe kitu na anapokusudia jambo yeye huamini fikra zake tu mpaka mwisho – he never forgive an insult, never forget a slight.

Kwa mjibu wa makala mbalimbali za kimahojiano na maofisa wa Jeshi la Rwanda wa sasa na wa zamani, waandishi wa Kimagharibi wameandika mno wakidai kuwa tatizo hilo limesababisha ‘kila aliyepingana na uamuzi wa Kagame nchini Uganda kupoteza maisha.

Na akishafanya jambo lolote baya yeye hupinga kuhusika nalo, huonesha ukali na kuwashambulia wanaomsema kwa maneno makali na kejeli. Anadhihaki na kusema ‘the claim is baseless and politically motivated’.

Hili wanalijua sana makachero wa Marekani na Uingereza, ndiyo maana hata Kagame akikataa vipi kuhusika na mauaji fulani wao wanamtuhumu moja kwa moja – ni modus operandi yake. Yaani ndiyo utaratibu wake wa kiutendaji. Ndiyo.

Jumapili ile mwezi Januari pale kanisani Kigali, mbele ya waumini madhabahuni alitaja waziwazi “betray Rwanda, face consequences” akimaanisha ‘isaliti Rwanda, kabiliana na madhara yake’.

Kuna kitu ambacho mara zote kinashangaza kuhusu madai ya Kagame juu ya usaliti. Je, mwanasiasa akitofautiana na mwajiri wake, akasema, “Huyu kiongozi si mkweli, ni myanyasaji na anadanganya jamii za kimataifa.” Je, anakuwa amesaliti nchi?

Kutokubaliana na mwanasiasa mwenzako ukajitenga naye kunazalisha usaliti kwa taifa? Hapana, labda iwe tu ni tafsiri ya Kagame mwenyewe juu ya neno ‘usaliti’.

Zaidi ya chochote kingine, katika hili, utaona ni jinsi gani ambavyo Kagame ana tafsiri za vitu kwa kadiri aonavyo yeye na kuyafanya mawazo yake kuwa ndiyo mawazo ya Wanyarwanda, wakati huo huo, ampingaye akifanywa kuwa mpinga Rwanda.

Hii ni hatari hasa kwa nchi kama Rwanda yenye historia ya viongozi kujitwalia madaraka na fikra za raia wake.

Itaendelea…

[email protected]

By Jamhuri