Miaka kadhaa iliyopita mwanafalsafa, Glenn Tinder, aliandika makala ambayo ilijadiliwa sana kwenye  Gazeti  la Atlantic Monthly isemayo: “Je, tunaweza kuwa wema bila Mungu?” Majibu ya wachangiaji wengi yalisema: “Hapana.” 

Ni kweli hatuwezi kuwa wema kwa nguvu zetu wenyewe. Hatuwezi kupenda kwa nguvu zetu wenyewe. Hatuwezi kufanikiwa kwa nguvu zetu wenyewe. Hatuwezi kwenda mbinguni kwa nguvu zetu wenyewe. 

Mwandishi Douglas Coupland katika kitabu chake cha “Life After God” anasema: “Siri yangu ni kwamba ninamhitaji Mungu. Siwezi kufanikisha jambo lolote mimi peke yangu. Ninamhitaji Mungu anisaidie kutoa, kwa sababu ninaona sina tena uwezo wa kutoa, anisaidie kuwa mwema kwa sababu ninaona sina tena uwezo wa wema, anisaidie kupenda kwa sababu ninaona nimefikia kikomo cha kuweza kupenda.”

Siku moja Frederick Ozanam alikuwa ana mahangaiko ya kiroho. Akaingia katika kanisa moja huko mjini Paris, Ufaransa. Alifikiri kwamba yuko peke yake. Kumbe ndani ya kanisa hilo kulikuwa na mzee Ampere, mwanasayansi mashuhuri.

Alipomwona Ampere hakuweza kuamini. Alimwona mwanasayansi huyu akiwa amelala kifudifudi, huku akiutumia mkono wake wa kulia kujipiga kifuani. Akashangaa sana. Akamsubiri atoke kanisani. Alipotoka kanisani alimwendea na kumuuliza swali hili: “Mheshimiwa profesa, inawezekanaje mtu mkubwa kama wewe unasali?”

Ampere akamjibu kwa moyo uliojaa unyenyekevu na kumwambia: “Rafiki yangu, mimi ni mkubwa ninaposali tu.” Alimjibu jibu lililojaa hekima sana. 

Sala inakufanya uwe mkubwa kiroho, kimaadili, kifamilia, kiuchumi na kiuongozi. Unaweza kusali mahali popote bila gharama yoyote. Mwanateolojia na Mwalimu wa Kanisa Katoliki, Augustino wa Hippo anasema: “Mungu anaongea kila mahali.”

Nakushauri sali kila wakati. Sali kwa ajili ya mafanikio ya familia yako. Sali kwa ajili ya mafanikio ya taifa lako. Sali kwa ajili ya mafanikio ya kazi yako. Sali kwa ajili ya mafanikio ya ndoa yako. Sali kwa ajili ya mafanikio ya kanisa lako. Sali kwa ajili ya mafanikio ya watoto wako.

Charles de Foucauld anasema: “Kusali ni kumtazama Yesu na kumpenda.” Tumtazame Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai kwa kusali. Tumtazame Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu kwa kusali. Tumtazame Yesu wa Ekaristi kwa kusali. Tusali bila kuchoka.

Mt. Katarinna wa Sienna siku moja alikuwa katika sala ya taamuli, Yesu alimtokea na kumwambia: “Ukinifikiria nami nitakufikiria.” Tumpende Kristo naye atatupenda.

Mwanafalsafa wa karne ya kwanza, Epitetto anasema hivi: “Nifanye nini isipokuwa kuimba utukufu wa Mungu? Ningalikuwa kasuku ningefanya kazi ya kasuku. Ningalikuwa bata ningefanya kazi ya bata. Lakini mimi ni kiumbe chenye akili, ninapaswa kumshangilia Mungu. Hii ndiyo kazi yangu, jukumu langu. Nami nitatekeleza kazi hii vizuri kabisa, nawaalika nanyi kuimba pamoja nami.”

Mt. Padri Pio alisema: “Tunamtafuta Mungu katika vitabu lakini tunampata katika sala.” Sala ni harufu nzuri ya maisha. Ni harufu inayotuonyesha alipo Mwenyezi Mungu aliyetuumba kwa sura na mfano wake. Unabaki kuwa ukweli usiopingika kuwa hakuna maana nzuri ya maisha bila sala. Mkristo ama mtu yeyote yule asiyesali ni sawa na ‘taa isiyowaka.’

Tunasoma hivi katika Maandiko Matakatifu: “Ninyi ni chumvi ya dunia. Chumvi ikipotewa na ladha yake, itakolezwa na nini? Haifai kitu tena, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni mwanga wa ulimwengu. Mji uliojengwa juu ya mlima haufichiki. Kadhalika watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kinara, ipate kuwaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo mwanga wenu uangaze mbele ya watu wapate kuona mienendo yenu miema na kumtukuza baba yenu aliye mbinguni.” (Mt 5:13-16).

Profesa Giuseppe Lazzati anafundisha kuwa: “Mkristo ni Mkristo au si Mkristo kadiri anavyosali.” Kama haujaelewa thamani ya sala katika maisha yako, basi bado haujaelewa undani wa Ukristo wako kabisa. 

Sala ni jambo muhimu kwa kila Mkristo. Wewe ni Mkristo kama unaweza kusali. Ni vigumu sana kwetu kuongoka kwa sababu maisha yetu hayana utambulisho wa sala.

Mang’amuzi ya maisha yanaweka bayana ukweli kwamba  kuongea ni rahisi kuliko kutenda. Ni rahisi kuhubiri juu ya upendo hata kama maisha yetu yanahubiri chuki. Ni rahisi kuhubiri kunywa maji wakati wewe unakunywa mvinyo. Bila maisha ya mfano bora, maisha yetu hayawezi kumponya yeyote. Watu wanaweza wasikuelewe pale utakapokuwa mtu wa sala, lakini watakuelewa pale wao watakaposhindwa kuishi maisha ya sala.

Maisha yetu ya hapa duniani yana ukomo! Tena yana ukomo. Unapojiandaa kufanikiwa hapa duniani, kumbuka pia kujiandaa kufanikiwa mbinguni.

739 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!