Kampuni ya Kamal Group inayomiliki kiwanda cha kuzalisha nondo cha Kamal Steel inatuhumiwa ‘kupoka’ vipodozi vyenye thamani ya Sh milioni 109 mali ya Barbanas Joseph, mkazi wa Dar es Salaam.

Jengo la ghorofa tisa mali ya Kampuni ya Kamal lililopo Mtaa wa Zaramo, Kata ya Upanga, Manispaa ya Ilala linatajwa kuwa chanzo cha Barnabas kupokwa vipodozi hivyo.

Jengo hilo ambalo ujenzi wake umeanzia ardhini kwa ghorofa moja kwenda chini, wakati wa kuandaa msingi wake lilileta athari kwa majengo mengine  likiwemo jengo la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ambalo Barnabas ni mpangaji wake.

Barnabas ambaye anajishughulisha na biashara ya kuuza vipodozi katika Mtaa huo wa Zaramo amesema tangu vipodozi hivyo vichukuliwe miaka saba iliyopita hadi leo haoni dalili za kuvipata.

Ameeleza kuwa vipodozi hivyo vilichukuliwa mwaka 2012 na wafanyakazi wa Kampuni ya Kamal waliokuwa wasimamizi wa ujenzi wa jengo hilo.

Amesema wafanyakazi hao walivichukua kwa makubaliano kwamba wangevihifadhi hadi ukarabati wa ukuta wa pango lake utakapofanyiwa ukarabati.

Pango hilo lipo kwenye jengo la NHC, kiwanja namba 1286/84, chumba namba 005, ambacho kimepakana na jengo hilo linalomilikiwa na Kampuni ya Kamal.

“Wakati wa kuandaa msingi wa ghorofa hili walichimba chini shimo lenye urefu wa ghorofa moja,  shimo walilokuwa wamechimba lilisababisha duka langu kubakia juu juu.

“Tulimueleza Ibrahim ambaye alikuwa msimamizi wa ujenzi huo kwa niaba ya Kamal Group kuwa shimo litaleta madhara, lakini akakataa,” ameeleza Barnabas.

Usiku baada ya shimo hilo kuchimbwa madhara yalijitokeza kwenye jengo la NHC, ukuta uliporomoka na kusababisha vipodozi vilivyokuwa kwenye pango la Barnabas kuporomokea kwenye shimo hilo.

“Mwakilishi wa Kamal alishuhudia tukio hilo na kutuomba tuvikusanye vipodozi vyote vilivyokuwa vimeporomokea kwenye shimo hilo na kwamba tutafute sehemu ya kuviweka  ili wafanye ukarabati.

“Vipodozi vyangu walishauri vitunzwe Dar Express, lakini pale gharama za kutunza mzigo kwa siku zilikuwa kubwa, kwa siku tulikuta ni Sh 120,000.

“Wahindi walikataa kutunza mali zangu kwa gharama hiyo, wakakubali zitunzwe kwenye maghala yao ambayo hawakunieleza yako sehemu gani,” amesema Barnabas.

Kwa mujibu wa Barnabas, walikubaliana kutunza vipodozi hivyo  kwa siku 90 na baada ya siku hizo vingerudishwa baada ya ujenzi wa msingi kukamilika na ukuta kukarabatiwa.

Hata hivyo siku 90 zilipita na ukuta huo haukujengwa na kwamba hali hiyo ilisababisha Barnabas kuanza kufuatilia kwa kumshirikisha mwanasheria wake ili wafungue shauri mahakamani.

Inaelezwa Mwanasheria, Sylivester Aligawesa, wa Kampuni ya Millennium Law Chambers Advocates, ndiye aliyewekwa na Barnabas lakini hakufungua kesi mahakamani, badala yake alijiondoa kabla ya kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.

“Mwanasheria wangu alikwenda kukutana na wamiliki wa Kampuni ya Kamal bila kunifahamisha, alivyorudi akaanza kunishawishi tusiende mahakamani.

“Hali ile ilinipa wasiwasi. Kwanza alikwenda peke yake bila kunipa taarifa; pili, akagoma tusiende mahakamani kwa hoja kwamba Wahindi watakuwa majirani zangu na sitakiwi kuanzisha migogoro na majirani zangu.

“Ilibidi nimshtaki kwenye Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na wakamuita na kumtaka apeleke shauri langu mahakamani, lakini baadaye alijiondoa,” amesema Barnabas.

Kwa upande wake Sylivester Aligawesa amesema sababu za kujiondoa ni kukosa ushirikiano alioutarajia kutoka kwa Barnabas.

“Mimi nilifanya kazi ya ziada nikaenda hadi kiwandani nikaonana na mwanasheria wa Kamal, tukaongea na kufikia pazuri, lakini hao wateja wangu hawakuonyesha ushirikiano,” amesema Aligawesa.

Hata hivyo ilipita miezi minne mingine bila kupata ufumbuzi wa suala lake, hali iliyomfanya kumtafuta mwanasheria mwingine ili amsaidie namna ya kufungua kesi mahakamani.

Mwanasheria aliyemtafuta kwa ajili ya kushughulikia tatizo lake anafahamika kwa jina la Dennis Ssebo wa Kampuni ya GLITZ Services Limited.

“Dennis Ssebo alijitolea kunisaidia kisheria, aliwaandikia barua ya kuwashtaki Kamal na Shirika la Nyumba mahakamani.

“Baada ya kuona barua ya Wakili Ssebo, NHC walituita ofisini kwao, tukakaa kikao na Kamal Group walikubali kukarabati sehemu iliyobomoka.

“Pia walikubali kunilipa Sh milioni 50, nusu ya gharama ya vipodozi vyangu na kunirudishia vile ambavyo havijaisha muda wake wa matumizi.

“Walifanya ukarabati ikapita miezi tisa mingine, baada ya kusumbuana nao wakakubali kunipeleka walikotunza vipodozi vyangu ili tuvichukue,” amesema.

Amesema mwakilishi wa Kampuni ya Kamal Group aliwapeleka Magomeni vilipotunzwa vipodozi hivyo lakini hawakuweza kuvichukua.

“Ibrahimu alitupeleka Magomeni kwenye jengo la ghorofa akatufungulia moja ya chumba kilichopo ghorofa ya pili na kuniambia nitambue mali zangu.

“Wakati nikiendelea kuvitambua vipodozi vyangu walikuja watu wanane na kututuhumu kwamba tumevunja jengo na tunataka kuiba mali,” amesema Barnabas.

Ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea mwaka 2013 na ilibidi kufanya mbinu za kuwatoroka kwani watu hao anahisi walikuwa wameandaliwa na Kampuni ya Kamal Group ili kukwamisha juhudi za kupata vipodozi hivyo.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kisutu, Magreth Mwandri, amesema amewahi kuzungumza na kampuni hiyo juu ya suala hilo na kudai kuwa inashindwa kumlipa Barnabas kwa sababu hana vielelezo.

“Kamal wanaweza kumlipa hela yake yote anayodai lakini hana vielelezo vinavyoonyesha kama kweli madai yake yako sahihi,” amesema Mwandri.

Gazeti hili limepata nakala yenye majina na sahihi ya  mwakilishi wa Kampuni ya Kamal akiwa amezitambua mali hizo kwa niaba ya Ravindor anayedaiwa kuwa kiongozi kwenye  Kampuni ya Kamal Group.

JAMHURI lilifika kwenye kiwanda cha Kamal na kukutana na Victor Martin, msimamizi mkuu wa shughuli za kiwandani hapo na kulieleza kuwa anayetakiwa kulizungumzia suala hilo hayupo, hivyo mwandishi arudi siku nyingine.

Baada ya JAMHURI kurudi kiwandani hapo, mwandishi alipewa kikaratasi chenye anwani ya ofisi za mawakili wa kiwanda hicho ili walizungumzie suala hilo.

Hata hivyo ilibainika siku kadhaa zilizofuata kwamba, ofisi hizo zilizokuwa Mtaa wa Samora Avenue katika jengo la Harbour View zimehamishwa.

JAMHURI limefanya mawasiliano na Mwanasheria wa kiwanda hicho, Dola Mwanri, na kusema: “Ndugu mwandishi, nataka uniletee hayo maelezo kimaandishi, siwezi kuzungumza kienyeji enyeji,” amesema Mwanri.

Naye Mwanasheria Dennis Ssebo anayesimamia masuala ya kisheria ya Barnabas Joseph amelieleza JAMHURI kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo.

“Mimi ni mwanasheria, ninapokuwa ninamsimamia mteja wangu sizungumzi na magazeti, kazi yangu ni kumsimamia mteja mahakamani na si vinginevyo. Kama unahisi taarifa alizokupa ziko sahihi, wewe andika unachotaka kuandika na kama taaluma yako inakutuma kuandika unachotaka kuandika, andika tu,” amefoka Ssebo.

By Jamhuri