Wiki iliyopita makala haya yalihoji kwa nini hakuna anayeingia mgodini kupinga uchimbaji wa kasi kubwa bila udhibiti. Leo tunakuletea sehemu ya pili ya makala haya. Endelea…

Pamoja na Serikali kujua kwamba Taifa linakabiliwa na tatizo kubwa la macro-economics (uchumi mkuu), inaonekana uchimbaji usiodhibitiwa si tatizo lake. Serikali inadhani tatizo la uchumi mkuu ni tatizo la wananchi wenyewe, kitu ambacho si sahihi kabisa. Serikali nyingi duniani zimeondolewa madarakani na wananchi wenye hasira, baada ya kushindwa kumudu uchumi wa nchi.


Kuhusu sekta ya ajira, Serikali imeshindwa kuzilinda ajira zilizopo kwenye migodi yetu zidumu kwa muda mrefu, na kuhakikisha kwamba migodi hiyo inadumu kwa miaka mingi iendelee kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania.


Kulingana na ushahidi huu, inaonekana Serikali ina njama za siri na kampuni zinazochimba madini nchini, kwa vile pamoja na kulipwa asilimia ndogo kuliko wote duniani, bado Serikali inaonekana imewafumbia macho wawekezaji matapeli wanaochimba dhahabu kwa fujo kama vile wanaiba, jambo linalojenga mazingira hatarishi kwa ajira za Watanzania katika kipindi kifupi kijacho.

 

Serikali yetu imekuwa ikifanya mambo kijeuri kwa kutojali hatima ya ajira za Watanzania, kwa vile hawana desturi na mila za kuzipumzisha serikali zisizowajibika kwa raia wake. Jirani zetu kule Zambia, serikali inapumzishwa kwa mfumuko wa bei, tena si asilimia thelathini (30%) kama sisi, hapana.


Kule Zambia serikali yaweza kupumzishwa kama unga unapanda bei kwa senti kumi tu! Hivyo kulingana na hali hiyo serikali za wenzetu zinawaogopa na kuwatii wananchi zikijua kwamba wao ndiyo waajiri. Hapa kwetu sisi wananchi ndiyo waajiri wa serikali lakini imetugeuka kuwa watumwa wake!

 

Tukirudi kwenye migodi yetu ya dhahabu ni kwamba uchimbaji wa madini hayo hapa nchini tangu umezinduliwa na Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa, imekuwa ni sekta ya siri ya hali ya juu kama ilivyokuwa mikataba ya madini ya almasi, hasa kwa wananchi wa kawaida.

 

Mwaka 2007 wakati nilipokuwa nikifundisha kule Chuo Kikuu Mzumbe, kuna mwanafunzi wangu mmoja alipangiwa kufanya ‘field’ katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).


Alipofika huko hakupokewa vizuri kwani tangu siku ya kwanza alipoingia alijikuta hatakiwi kabisa kwenye maeneo hayo, watu wote aliowakuta – Wazungu na Watanzania wote hawamtaki – na wakati wote wana wasiwasi na yeye kwamba asije akayaona au kuyajua ambayo hatakiwi kuyajua mtu mwingine zaidi ya wale wafanyakazi wa pale na wakubwa walioko Dar es Salaam, ambao hasa ndiyo wamiliki wakubwa wa migodi hiyo.

 

Pia mwanafunzi huyo baada ya kufika mgodini kilifanyika kikao cha dharura kwa wafanyakazi wote isipokuwa yeye kuwatahadharisha kwamba wawe makini wasijisahau kwa kusema au kumwachia mtu (mwanafunzi huyo mgeni) kujua siri za mgodi!


Mwanafunzi huyu alifanya ‘field’ yake kwa miezi mitatu akamaliza, lakini hakujisikia kama Mtanzania kwa vile alibaguliwa. Alipokuwa huko alipata taarifa kwamba Wazungu wanaogopa watu wageni kwa vile kwenye migodi hiyo wao wanahamisha utajiri wa nchi hii wakishirikiana na watawala, hivyo hawataki siri zao zijulikane kwa watu wa kawaida!


Sasa kama hizi kampuni za kuchimba dhahabu ni wawekezaji wa kweli, kwanini wanafanya siri hata kwa Watanzania ambao ndiyo wenye nchi? Kama wanalipa kodi, na kama kweli wanatoa hiyo asilimia tatu wanahofia nini tena?


Katika kipindi cha utawala wa Mkapa, waziri wake wa Nishati na Madini aliwahi kufanya ziara ya kikazi kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Geita, alipofika mgodini hapo alipokewa kwa shingo upande. Akaruhusiwa kutembelea sehemu zote za mgodi isipokuwa alipofika kwenye ghala yanapohifadhiwa matofali ya dhahabu akaambiwa ‘stop’, huko huruhusiwi kuingia! Akahoji“Kwanini siruhusiwi kuingia? Kwani kuna nini cha siri ambacho sitakiwi kukiona? Mimi ni Waziri wa Madini hamwezi kunizuia nisiingie huko, lazima niingie!”


Je, unajua nini kilichotokea? Usikose sehemu ya tatu ya makala haya wiki ijayo.

Mwandishi wa makala haya, Dk. Noordin Jella (PhD in Economics), ni Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu Huria, Chuo Kikuu cha Kampala (KIU) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

 

Kwa sasa ni Mwandishi wa Kujitegemea na Mchambuzi wa masuala ya siasa. Anapatikana kwa email: norjella@yahoo.com

Simu: +255 782 000 131


1178 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!