Kwa zaidi ya wiki sasa nipo hapa Nairobi, Kenya, nikihudhuria mafunzo ya uandishi wa habari za masuala ya kifedha, hasa bajeti ya Serikali. Mafunzo haya ni ya muda wa wiki mbili. Katika mafunzo haya tunapewa mifano kutoka sehemu mbalimbali na wakubwa kutoka Serikali ya Kenya wanawasilisha mada.

Yapo mambo tuliyozitangulia nchi za Afrika Mashariki. Kwa mfano, wakati Tanzania ilipunguza madaraka ya Serikali Kuu na kuyapeleka mkoani, mwaka 1972, miaka 40 baadaye Kenya ndipo wanafanya utaratibu huu kuwa ifikapo mwakani Aprili, wataanzisha majimbo 47 na hivyo kupeleka madaraka mikoani.


Zipo sheria mbalimbali ambazo karibu nchi nyingine za Afrika Mashariki kwa ndo kwanza zinaanza kuzitumia, wakati Tanzania tunazo kwa wastani wa muongo mmoja sasa. Moja ya sheria hizo ni Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2004, ambapo sasa Kenya nao wanayo, Uganda, Rwanda na Burundi, pia nao wameanzisha sheria hii.

 

Sitanii, ninayoyashuhudia hapa Kenya ni makubwa ajabu. Hapo kwetu Tanzania tunayo mipango lukuki. Ikiwamo MKUKUTA, MKU, MDG, Vision 2025 na mingine mingi. Tanzania kwa mipango na taarifa (reports) za kuwasilisha kwa wafadhili hatujambo. Wenzetu wakianza kusimulia unaona woga ulivyowajaa dhidi ya Tanzania. Wakisoma mipango wanaona uchumi unapaa.


Baada ya mifano kutoka katika nchi hizi nimevuta pumzi na nikalinganisha kinachoendelea hapo kwetu. Kwanza hapo kwetu tunalo tatizo la msingi la ukosefu wa taarifa. Taarifa nyingi za Serikali zinatolewa kama bangi, kwa siri. Wananchi na hata waandishi wa habari hatupatiwi taarifa za kutosha.

 

Mfano ni mdogo tu, kwamba kwa sasa kuna ujenzi wa barabara ya kisasa unaoendelea kati ya Kimara na Magogoni Dar es Salaam. Hata mimi ukiniuliza leo sijui Ubungo na makutano mengine kama Lango la Jiji (Magomeni), Fire na Bibi Titi iwapo watajenga barabara za madaraja au la.

 

Tunachokiona ni ujenzi unaendelea. Kwa hapa Kenya wanafanya ujenzi wa barabara kwa ajili ya maandalizi ya Kenya kuwa taifa lenye viwanda vya kati ifikapo mwaka 2030. Mkakati wao wa Vision 2030 unaushuhudia kwa macho ukitekelezeka.

 

Nimepata kuwa hapa Nairobi mara kadhaa miaka ya nyuma, lakini safari hii nimebaki mdomo wazi. Kila sehemu ya Jiji la Nairobi, kuna kinachoitwa ‘Asante Kibaki’, Rais Mwai Kibaki hajafanya mchezo. Amejenga barabara usipime.

 

Tena si tu kwamba anajenga barabara. Rais Kibaki ameweka sera iliyo wazi kabisa. Kila mkandarasi anayepewa ujenzi wa barabara, sehemu yoyote yenye makutano ni lazima ajenge barabara za maghorofa (flyovers). Katikati ya Jiji la Nairobi sasa hapana tofauti na katikati ya Jiji la Cairo, Misri.

 

Sitanii, nimesafiri kwa barabara kutoka Nairobi kwenda Nakuru, wastani wa kilomita 300 hivi kutoka Nairobi, lakini ni ajabu ya mwaka. Barabara hiyo yaani umbali wa sawa na Dar es Salaam hadi Gairo, kila makutano kuna flyover na kila penye kilima kuna njia tatu hadi nne.

 

Picha za aina ya barabara wanazotaka ziwepo Nairobi kufikia mwaka 2020 tayari zimechapishwa na kubandikwa kama mabango kwenye sehemu mbalimbali za Jiji la Nairobi, sawa na viongozi wetu wanavyotangaza sura zao wakati wa uchaguzi kwenye mabango makubwa.

 

Inawezekana hunielewi ninachosema mpendwa msomaji, narudia. Wakati viongozi wetu wanatumia fedha za umma kubadika sura zao kwenye mabango sehemu mbalimbali za nchi, hapa Kenya wanabandika picha za mipango na mikakati ya maendeleo. Kisha wanawapa wananchi fursa ya kutoa mawazo yao juu ya ni wapi mipango hiyo iboreshwe na mawazo yao yanatiliwa maanani.


Sitanii, waheshimiwa wabunge na serikali yetu someni kwa makini ujumbe unaofuata hapa chini. Nchi za Kenya, Uganda na Rwanda zinatuacha kwa kasi. Sisi hatuzungumzi maendeleo tumetumbukia kwenye kujadili udini, ukabila na siasa. Tunashindana kuchungulia Mwislamu au Mkristo yupi kateuliwa kushika wadhifa upi, na si barabara ipi ya kufikisha mahidi ya wakulima sokoni yakitokea shambani.


Nchi nilizozitaja zimebuni mbinu ambazo ni chimbuko la maendeleo ya kasi. Rais Mwai Kibaki kwa kushirikiana na Waziri Mkuu, Raila Odinga, wameanzisha utaratibu mpya wa ajira kwa watumishi wa umma. Kila Waziri, Katibu Mkuu, Kamishna, Mkurugenzi, Meneja au Mkuu wa Idara yoyote ya Serikali, mbali ya kutumia sheria ya utumishi wa umma kama ilivyo ya kwetu hapo nyumbani, wameanzisha utaratibu wa mikataba.


Rais au Waziri Mkuu wanakutana na viongozi hawa, sawa na hapo kwetu walivyokwenda katika Hoteli ya Ngurdoto, Arusha, kisha wanaingia mikataba ya utumishi. Kwa Kenya wanaingia mikataba ya siku 100. Kila baada ya siku 100 Waziri au viongozi niliowataja hapo juu anapaswa kutoa taarifa ya nini amefanikiwa kufanya katika kitengo anachokisimamia.


Katika kikao cha kupanga, wanaweka malengo. Utekelezaji ni ndani ya siku 100. Kwa mfano Waziri wa Maji aseme atachimba visima 10 vya maji kwa kila mkoa (jambo linalowezekana). Kisha baada ya siku 100 anapaswa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji serikalini (si visingizio).


Sitanii, anayewasilisha visingizio kwa mfano akisema; Ohooo! Hazina walichelewesha fedha, mvua zilinyesha mno magari yakashindwa kupita na vingine vya aina hii, kinachomkuta hakisahau. Uteuzi wake unatenguliwa, kazi hii anakabidhiwa mtu mwingine naye anaposhindwa hali inakuwa hivyo hivyo. Kilichotokea ni kwamba wote wameweza kutimiza malengo.


Hii ina maana gani? Kwa mfano, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, anapaswa kumwambia Rais na waingie mkataba kuwa ndani ya siku 100 atapima viwanja vingapi. Akishindwa, anateuliwa Waziri mwingine. Akiweza, wanaweka malengo mapya ya siku 100 nyingine.


Uganda Rais Yoweri Museveni yeye ameamua kuanzisha utaratibu mpya. Makatibu Wakuu wa Wizara zote, amefuta utaratibu wa kuwa watumishi wa kudumu (permanent secretary). Makatibu Wakuu wote wanapewa mkataba wa miaka mitatu mitatu.

 

Ndani ya mkataba huo, kuna vifungu na masharti ya kazi. Kwa mfano, ukipewa ukatibu Mkuu na ukakubali kwamba Wizara ya Fedha itadhibiti uuzaji wa bidhaa na huduma bila kutoa risiti kwa asilimia 30 kwa kuanzia ndani ya siku 100, taarifa inayotakiwa kwenye kikao cha utekelezaji ni kufikiwa kwa asilimia 30 halisi na si vinginevyo. Anayeshindwa mkataba unafutwa.

 

Nchini Rwanda, Rais Paul Kagame ndiye aliyevunja rekodi. Kenya na Uganda wamejifunza kutoka kwake. Yeye ana utaratibu unaoitwa ‘Umuhigo’. Huu ni mkataba anaoingia Rais Kagame na kila mkuu wa Idara.

 

Unapoteuliwa kushika idara anakupa mwezi mmoja, unajifunza idara ile ina nini ndani yake na unaandaa mkataba wa malengo, yaani unachokusudia kukifanya. Kisha unakiwasilisha kwa Rais Kagame mnakaa meza moja, unajieleza na kukitetea na kumweleza jinsi utakavyofanikisha utekelezaji wake.

 

Hii ni pamoja na mawaziri, mameya wa miji, makatibu wakuu na wakuu wote wa idara nyeti kama hapo kwetu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na nyingine za aina hiyo wote wanaingia mkataba na Rais.

 

Sitanii, Rais Kagame anapokubaliana na mpango uliouwasilisha, unatia saini na yeye anatia saini. Anakupa nakala moja na yeye anabaki na nakala. Siku ya kuwasilisha ripoti yako ya utekelezaji, ambayo kwa Kagame ni mara moja kwa mwaka, kila mtu anakuja na nakala ya makubaliano mezani.

 

Mnapitia moja baada ya nyingine na unaeleza umetekeleza kwa kiwango gani mkataba mlioingia. Mambo hayaishii mezani. Bila kumpangia wapi unataka akague, kulingana na ripoti yako anakushitukiza mnapanda kwenye gari na kwenda kukagua ama yote au mawili au matatu kati ya yale uliyomweleza.

 

Ikiwa hujatekeleza na umemdanganya hatua anayochukua ni kukufuta kazi na kuelekeza ushitakiwe na kufungwa gerezani. Je, hapo kwetu hali ikoje? Tunao usimamizi wa kazi zetu? Rais Jakaya Kikwete anaingia mikataba na mawaziri wake kisha wanawasilisha ripoti sahihi? Tafakari, Chukua hatua.


1327 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!