*Uamuzi wa Mahakama ya Rufaa wapuuzwa na viongozi

*Wanaopinga kuhama wabambikiwa kesi mahakamani

*Mwanamke afungwa miezi 6 jela, mtoto alelewa na bibi

Wananchi kadhaa katika eneo la Maramboi, Kijiji cha Vilima Vitatu, Wilaya ya Babati mkoani Manyara, hawana makazi baada ya nyumba zao kuchomwa moto ili kumpisha mwekezaji raia wa Ufaransa.

Waliofikwa na maafa hayo ni Watanzania wafugaji wa jamii ya Kidatoga. Kampuni ya Kifaransa ya Un Lodge En Afrique Limited (ULEA), imepewa kinyemela ardhi ya wafugaji hao ili kuendesha shughuli za utalii kupitia Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Burunge.

Kampuni hiyo inamilikiwa na Nicolas Negre (hisa 99) na Stephanie du Marroussem ambaye ana hisa moja. Raia hao wawili pia ndiyo wakurugenzi wa kampuni hiyo wakiwa na mwenzao, Antonio Haji ambaye ni raia wa Uswisi.

Wazungu hao wanakilipa kijiji dola 5,000 (Sh milioni 8) kwa mwaka. Kuchomwa kwa makazi ya wananchi hao kumefanywa licha ya kuwapo hukumu ya Mahakama ya Rufani iliyotamka bayana kuwa Kampuni ya ULEA ipo eneo hilo kinyume cha sheria na hivyo wananchi waachwe waendelee na maisha yao kama kawaida.

Hata hivyo, ULEA imefanikiwa kuwatumia viongozi kadhaa wa kijiji, wilaya na Mkoa wa Manyara kuwaminya wananchi hao na kupuuza amri halali ya Mahakama ya Rufani. Wakili mwakilishi wa wananchi hao, Mayomba Duncan, akiwa na baadhi ya wananchi hao, alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mwishoni na wiki na kusema wananchi hao wanahitaji msaada wa haraka wa chakula na makazi.

“Nia ni kuwaeleza ninyi (waandishi wa habari), na umma wa Tanzania uvunjaji mkubwa wa Katiba na sheria za nchi yetu, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kiraia, na kutotekelezwa kabisa kwa dhana ya utawala bora na utawala wa sheria kwa kuachia vyombo vyenye mamlaka ya kutekeleza sheria kuingilia uhuru na uamuzi wa Mahakama,” alisema Mayomba.

 

Historia ya mgogoro

Makazi ya wanajamii wa Kidatoga na maboma yao yalichomwa moto na watu wanaosemekana hawajulikani asubuhi ya Septemba 4, mwaka huu. Uchomaji na uharibifu mkubwa wa mali ulitokana na ushindi wa kesi ya madai ya ardhi iliyofunguliwa na Halmashauri ya Kijiji cha Vilima Vitatu, na WMA ya Burunge, dhidi ya wanajamii ya wafugaji ya Wadatoga waishio katika eneo la Maramboi wakiongozwa na Mama Udaghwenga Bayay na wengine 16.

 

Shauri dhidi ya wanajamii hao lilifunguliwa kwa mara ya kwanza katika Baraza la Ardhi na Nyumba Mkoa wa Manyara-Babati-na lilisajiliwa kama Maombi Na. 70 ya Mwaka 2008. Ufunguzi wa shauri hilo ulitokana na uamuzi wa Mkutano wa Kijiji cha Vilima Vitatu wa Desemba 4, 1999 uliotenga eneo wanaloishi wanajamii hao kwa ajili ya malisho ya mifugo na wanyamapori. Uamuzi huo wa kijiji uliwezesha kuanzishwa kwa Burunge WMA mwaka 2004.

 

Uamuzi wa Mkutano Mkuu wa Kijiji wa mwaka 1999 ulipingwa vikali na Mkutano Mkuu uliofuata wa kijiji hicho hicho ulioitishwa Mei 10, 2006. Katika Mkutano huo, kijiji kilipinga kuanzishwa kwa Burunge WMA kwa maelezo kwamba lengo lake lilipotoshwa, na kwamba wanakijiji wakazi hawakushirikishwa, bali viongozi wachache kwa kushinikizwa na Afisa Wanyamapori wa Wilaya.

 

Baada ya uamuzi huo wa kijiji, Mwenyekiti wa Kijiji, Belela Erasto, alimwandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Wanyamapori mnamo Mei 12, 2006 akimweleza Mkurugenzi wa Wanyamapori kuhusu uamuzi wa kijiji wa kujiondoa kwenye WMA na JUHIBU (yaani Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge). Uamuzi uliotolewa baada ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kupokea barua hii ya Kijiji haujulikani.

Pamoja na pingamizi zote za uanzishwaji wa Burunge WMA, na pingamizi za kutoa ardhi ya kijiji kwa Burunge WMA, Februari 23, 2007 Burunge WMA iliingia mkataba wa uwekezaji katika eneo la Burunge WMA na Kampuni ya Kifaransa ya Un Lodge En Afrique Limited (ULEA). Katika mkataba huo, Burunge WMA walitoa haki yote ndani ya eneo la Burunge WMA kwa ULEA ili kuiwezesha ULEA kuendesha biashara ya kambi na matembezi ya kitalii kwa muda wa miaka mitatu.

 

Katika mkataba huo, moja ya mambo ambayo Burunge WMA ilitakiwa kufanya ni kuhakikisha kwamba eneo lote la Burunge WMA haliishi watu kwa muda wote wa mkataba. Hayo yote, na utoaji wa ardhi yote iliyoko ndani ya Burunge WMA yalifanyika kwa malipo ya dola elfu tano tu za Marekani kwa mwaka!

 

Mkataba huo pia uliainisha bayana kwamba uwekezaji wowote na maendeleo yoyote ndani ya WMA inayohusu utumiaji na ukazi katika ardhi utatakiwa kufuata Sheria za Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999. Hilo halikufuatwa, na badala yake uvunjifu mkubwa wa Sheria za Ardhi ulifanyika.

 

Kutokana na kuingia kwa mkataba huo, Aprili 11, 2008 uongozi wa Kijiji cha Vilima Vitatu na uongozi wa Kata ya Nkaiti ulikutana na Mkuu wa Wilaya ya Babati kujadili taarifa ya mpango wa matumizi bora ya ardhi. Katika taarifa hiyo pungufu mbalimbali ziliainishwa, na kikao kikahamia eneo la Maramboi ambako wanajamii hao wanaishi. Katika eneo la Maramboi, kikao kilikutana na wanajamii 84 waishio Maramboi, na kuwataarifu kuwa eneo hilo limetengwa kwa ajili ya malisho na wanyamapori na si eneo la makazi. Wakaelezwa utaratibu wa uhamiaji kutoka kijiji kimoja kwenda kingine.

 

Mkuu wa Wilaya ya Babati alitoa maelekezo kuwa mwekezaji amepewa ekari 45 tu ambazo ataweka kambi ya kulaza wageni wa kitalii, na kuwaagiza kuwa wale wote waliojenga katika eneo la mwekezaji waondoke mara moja na wapewe maeneo mengine katika eneo la Mfulu wa Ng’ombe na maeneo mengine hapo hapo Maramboi. Wafugaji 17 waliainishwa kuwapo ndani ya eneo la mwekezaji.

 

Mkutano huo na Mkuu wa Wilaya ulifuatiwa na mkutano mwingine Mkuu wa Kijiji wa Aprili 14, 2008 uliohudhuriwa na watu mbalimbali akiwamo Luteni Kanali mstaafu Werema akiiwakilisha ULEA kutoka Arusha. Kichojadiliwa katika Mkutano huo Maalum ni eneo la mwekezaji. Kijiji kiliazimia kuwa mwekezaji apokewe, na kwamba familia 17 za wafugaji waishio ndani ya eneo la mwekezaji waondoke mara moja na kupewa maeneo mengine ya kujenga makazi yao .

 

Uamuzi huo ulirudiwa na uongozi wa kijiji katika taarifa yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara ya Aprili 21, 2008. Cha kushangaza ni jinsi kijiji, chini ya uongozi wa Mwenyekiti Belela Erasto, kilivyobadili uamuzi wake wa mwaka 2006 na kuamua kurudia tena Burunge WMA.

 

Wananchi wafunguliwa kesi

Baada ya uamuzi huo, yaliyofuata ni kwa wanajamii wa Kidatoga kufunguliwa kesi za jinai, zikiwamo za uvunjaji, wizi wa fedha taslimu, wizi wa baiskeli, na wizi wa shati; mali zilizodaiwa kuwa za mwekezaji au wafanyakazi na wapambe wake. Katika kesi nyingine, wanajamii hao hao walishitakiwa kwa kutishia kumpiga mmoja wa wafanyakazi wa mwekezaji.

 

Mashauri hayo yalifunguliwa katika Mahakama ya Mwanzo Magugu. Baada ya wakili wa Kampuni ya F K Law Chambers kuingilia, yalihamishiwa Mahakama ya Wilaya Babati. Mashauri yote mawili yaliishia kwa wanajamii hawa kuachiwa huru kwa kukosekana ushahidi.

 

Wakati mashauri hayo ya jinai yakiendelea, Mei 9, 2008 Halmashauri ya Kijiji cha Vilima Vitatu na Burunge WMA walifungua shauri la madai ya ardhi katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, Mkoa wa Manyara – Maombi Namba 70 ya mwaka 2008 – dhidi ya wanajamii 17 wanaodaiwa kuwa ndani ya eneo la mwekezaji wakiongozwa na mama Udaqwenga Bayay.

 

Wanajamii walipoteza shauri hilo katika Baraza la Ardhi na, kwa kutoridhika, walikata rufani Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi. Rufaa yao ilisikilizwa na Jaji Ngwala. Akaitupilia mbali. Kwa kutoridhika, wanajamii walikata rufani katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania, ambacho ni chombo cha mwisho cha utoaji haki nchini.

 

Mahakama ya Rufani yatenda haki

Machi 15, 2013 jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Jaji Msoffe, Jaji Sauda Mjasiri, na Jaji Profesa Ibrahim Juma, walitoa uamuzi uliowapa ushindi wanajamii hao. Katika uamuzi wao, Majaji wa Mahakama ya Rufani waliweka bayana kwamba:

(i)    Katika utoaji na ugawaji wa ardhi kwa Burunge WMA, kijiji hakikufuata maelekezo ya Sheria kwa maana ilikuwa lazima kwa wajibu rufani (Halmashauri ya Kijiji cha Vilima Vitatu na Burunge WMA) kuonesha kwa ushahidi kwamba kijiji kiligawa ardhi kwa Burunge WMA kwa kufuata taratibu zilizoainishwa na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori kabla kesi dhidi ya wanajamii haijaamuliwa; na

(ii)   Kwa kuangalia taarifa zilizokuwa mbele ya Mahakama ya Rufani, hakukuwa na Information Data Sheet na Land Use Plan ambavyo ni muhimu katika maombi ya kufanya eneo husika kuwa eneo la hifadhi ya wanyamapori. Kwa maana hiyo, kifungu cha 13 cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori kilikiukwa.

 

Viongozi wa kijiji, WMA waipuuza Mahakama ya Rufani

 

Kwa kuzingatia ukiukwaji wa Sheria ulioainishwa, Mahakama ya Rufani ilikubali rufaa ya wanajamii na kutaka Kijiji cha Vilima Vitatu na Burunge WMA kulipa gharama zote za kesi. Wanajamii, walipeleka maainisho ya gharama za kesi na kuomba Mahakama, kupitia Baraza la Ardhi la Wilaya, kukaza hukumu ya Mahakama ya Rufani. Wakati haya yakisubiriwa, uvunjifu wa haki za binadamu na kiraia, vilianza. Licha ya kukiuka haki za binadamu na utawala bora, uamuzi wa Mahakama ya Rufani ulipuuzwa kuanzia hapo.

Halmashauri ya Kijiji cha Vilima Vitatu, pamoja na Burunge WMA, badala ya kutekeleza na kufuata maelekezo yaliyotolewa kwenye hukumu ya Mahakama ya Rufani, waliitisha vikao mbalimbali kujadili hukumu hiyo na kutoa uamuzi unaopingana na hukumu ya Mahakama ya Rufani.

Waliamua yafuatavyo:

(i) Walipitisha uamuzi wa kumgawia tena mwekezaji eneo la ardhi lenye ukubwa wa ekari 45 likizungukwa na eneo la kilometa moja kila upande, yaani jumla ya kilometa za mraba zaidi ya nne na ekari 45; na

(ii)   Walipitisha uamuzi wa kuwaondoa kwa nguvu, na kuwachomea nyumba wanajamii ya kifugaji kinyume na uamuzi wa Mahakama ya Rufani. Uamuzi ulifanywa katika vikao rasmi na visivyo rasmi ndiyo uliosabababisha kuchomwa moto kwa nyumba za wafugaji hao.

 

Sheria zilivyovunjwa

Sheria ya Ardhi hairuhusu kijiji kugawa ardhi inayozidi ekari 50 kwa mtu yeyote yule. Mwekezaji katika Kijiji cha Vilima Vitatu amepewa haki juu ya ardhi inayozidi kiasi kilichainishwa kisheria

 

Utafiti uliofanywa katika ofisi ya Msajili wa Kampuni nchini (BRELA), Kampuni ya Un Lodge En Afrique Limited ni kampuni ya kigeni iliyosajiliwa Tanzania, na ambayo hisa zake zote zinamilikiwa na wageni wawili – Nicolas Negre (hisa 99), na Stephanie Planteau Du Marroussem (hisa 1) – wote wakiwa raia wa Ufaransa. Sheria za Ardhi haziruhusu mtu asiye raia wa Tanzania kumilikishwa ardhi isipokuwa tu kama ardhi hiyo itatolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa ajili ya uwekezaji pekee. ULEA amemilikishwa ardhi na Kijiji cha Vilima Vitatu na kupewa haki juu ya ardhi ya Burunge WMA kinyume cha Sheria ya Uwekezaji na Sheria za Ardhi.

 

Kwa mujibu wa kifungu cha 107A cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama inatamkwa kuwa ndiyo mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mahakama ya Rufani – ambacho ndicho chombo cha mwisho cha utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – imeshatamka bayana kwamba Burunge WMA haikuwa imeanzishwa kwa kufuata sheria na taratibu, na kwamba ardhi iliyopewa na Kijiji cha Vilima Vitatu haikupewa kihalali na ilikiuka misingi ya Sheria.

 

Kwa hukumu hiyo ya Mahakama ya Rufani, mkataba uliowekwa kati ya Burunge WMA na mwekezaji wa ULEA ni batili. Kitendo cha Burunge WMA na kijiji kuendelea kukumbatia, jambo ambalo tayari Mahakama imetamka kuwa ni batili, ni kitendo cha kuvunja Katiba ya nchi yetu na kinaonesha dharau kubwa na udhalilishaji kwa Mahakama.

 

Wananchi wateswa, wabambikiwa kesi

Kabla na baada ya uchomaji nyumba, wananchi hao wamekuwa wakifunguliwa kesi mbalimbali za jinai, kuwekwa kizuizini, na kuhukumiwa kwa makosa ya kutungwa. Kwa sasa, tayari kesi kadhaa zimefunguliwa dhidi yao katika Mahakama ya Mwanzo Magugu, Wilaya ya Babati. Miongoni mwa kesi hizo ni:

(i)Shauri la Jinai Namba 112/ 2013 – Mshitakiwa: Ghinyanga Gidamajod na Mabee Giyamu. Mabee ni mtoto wa Giyamu Marish.

(ii) Shauri la Jinai Namba 174/2013 – kati ya Lekshon Laiza na Gaudence Diwani. Huyu Gaudence ni kijana wa chini ya umri unaoruhusiwa kushitakiwa katika Mahakama za kawaida, lakini alishahukumiwa kifungo cha miezi sita jela bila faini. Kwa sasa ametoka baada ya kukata rufaa na kuweka wakili.

(iii) Shauri la Jinai Namba 264 la 2013 – mshitakiwa Bujaji Gisima. Huyu ni mzee wa miaka 70 na alishatumikia kifungo cha miezi sita jela. Yupo nje kwa sasa.

(iv) Shauri la Jinai Namba 268/2013 – mshitakiwa, Wakim Giyamu. Huyu ni kijana wa Giyamu Marish. Kesi yake bado ipo mahakamani.

(v)Shauri la Jinai Namba 273/2013 – mshitakiwa Dagabonga Mabe. Huyu ni mke wa Mabee Giyamu – mwenye Shauri la Jinai Namba 112/2013. Mama huyu alihukumiwa miezi sita jela bila faini, na ametumikia kifungo akimwacha mtoto wake mchanga wa miezi sita tu akiwa na nyanya yake.

(vi)  Shauri la Jinai Namba 277/2013 – mshitakiwa Bukuchan Giyamu. Huyu ni mke wa Giyamu Marish. Kwa hiyo, katika familia hii mama, kijana wake na mkwewe; wote wanashitakiwa au wameshahukumiwa na kutumikia vifungo.

(vii) Shauri la Jinai Namba 278/2013 – mshitakiwa Kipara Giyamu – huyu pia ni mtoto wa Giyamu Marish ambaye shauri lake linaendelea .

(vii)  Shauri la Jinai Namba 422/ 2013 – mshitakiwa, Saidi Qamunga. Shauri lake linaendelea.

(ix)  Shauri la Jinai Namba 423/2013 – mshitakiwa Julius Nduruu. Shauri hili linaendelea.

(x) Shauri la Jinai Namba 424/2013 – mshitakiwa Goerge Sikarika. Shauri linaendelea mahakamani.

Familia moja tu ya Mzee Giyamu Marish inakabiliwa na kesi nne – moja dhidi ya mama yao, mbili dhidi ya watoto wao, na moja dhidi ya mke wa mtoto wao.

 

Ukimya wa viongozi wa Serikali

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Erasto Mbwilo, bado hajachukua hatua za kuhakikisha wawekezaji na viongozi wengine wanaheshimu uamuzi wa Mahakama ya Rufani.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ ambaye amewahi kukaimu nafasi kama hiyo katika Wilaya ya Babati, Christina Mdeme, alishatoa msimamo akiwataka viongozi wa WMA na kijiji waheshimu uamuzi wa Mahakama ya Rufani.

Alisema kama Mahakama ya Rufani imewaona wananchi hao wana haki, waachwe waendelee kuishi hapo, na kwamba uamuzi wa aina hiyo hauhojiwi.

Wakati huo Mkuu wa Wilaya ya Babati, Khalid Mandia, alikuwa mgonjwa. Aliporejea ofisini akaendelea na msimamo wa kuwataka wananchi hao waondolewe ili kumpisha mwekezaji.

Katika sakata hili, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Mandia na Mbwilo wapo upande wa mwekezaji.

2289 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!