Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alidhamiria kuifanya Tanzania kuwa paradiso.

“Mwalimu alitaka kujenga paradiso ya hapa duniani katika nchi hii. Kama tungetekeleza misingi aliyotuwekea, Tanzania ingekuwa paradiso.” Haya ni maneno ya Ibrahim Kaduma (76).

 

Kaduma ameshika nyadhifa mbalimbali, zikiwamo za ukurugenzi na uwaziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza. Katika mahojiano na JAMHURI akiwa nyumbani kwake Makongo Juu, Dar es Salaam, Kaduma anaeleza kutofurwahishwa na namna misingi ya maadili iliyoachwa na Mwalimu inavyobomolewa. Kaduma, mmoja wa wafuasi wa Mwalimu Nyerere na waumini wakuu wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, anasema kwenda kombo kwa mambo mengi nchini ni matokeo ya viongozi kuweka kando misingi ya uongozi bora iliyowekwa na mwasisi huyo wa Taifa.

 

Anamsifu Mwalimu kwa kusema, “Mwalimu mambo mengine yalikuwa ya Mungu, siyo yake mwenyewe.”

 

Anaongeza: “Mwalimu hakutufundisha kugombania na kunyang’anyana mali na vyeo, alitaka tuwe na viongozi wenye uwezo wa kutuongoza na kwa uadilifu ili hatimaye wote tunufaike.”

 

Anasema Azimio la Arusha liliasisiwa na Mwalimu Nyerere ili kuwezesha rasilimali za nchi zitumike kwa maslahi ya wananchi wote na kujenga Taifa la watu huru, sawa, wanaojitegemea, wanaomiliki uchumi na wanaoongozwa na viongozi bora.

 

Anasema katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi, Azimio la Arusha liliuawa kwa kuanzishwa kwa Azimio la Zanzibar lililowaziba midomo viongozi wanaotetea misingi iliyowekwa na Mwalimu Nyerere.

 

“Mwalimu alililea Taifa hili kama mzazi aleavyo mtoto. Alianza na neno ‘Uhuru’ kuwaandaa Watanganyika kujitawala. Alipoona Uhuru unakaribia, akagundua Waswahili wanaweza kudhani tukipata Uhuru tunaweza kuchukua cha mtu yeyote na kufukuza watu kwenye majumba yao. Ndipo akaleta Uhuru na Kazi. Kwa hiyo, watu wakaanza kuelewa kuwa katika Uhuru kuna Kazi.”

Ubinafsi

Kwa mujibu wa Kaduma, taswira ya ubaguzi wa kupata huduma mbalimbali za kijamii nchini kama vile elimu, ni matokeo ya baadhi ya viongozi kutanguliza masilahi binafsi kinyume cha malengo ya Mwalimu Nyerere.

 

“Tatizo hili ni kwa sababu tumetanguliza ubinafsi badala ya masilahi ya Taifa. Tumeruhusu ubinafsi utawale badala ya masilahi ya Taifa. Si haki hata kidogo wanyonge kukosa mikopo ya kugharimia elimu.

 

“Kila anayefaulu kwenda chuo kikuu anastahili kupewa mkopo. Tuna sababu na uwezo wa kusomesha kila mtu katika nchi hii ila shida yetu hatuna nia ya kufanya hivyo, nia imepotoshwa na ubinafsi,” anasisitiza.

Dhana ya kujiuzulu

Kaduma anasema kujiuzulu ni jambo la hekima, na kwamba hata Mwalimu Nyerere aliwahi kujiuzulu ualimu na uwaziri mkuu kwa lengo la kufundisha Watanzania uongozi imara.

“Uongozi si lelemama, unataka mtu kujitoa mhanga na kuwa tayari kupoteza vitu fulani kwa masilahi ya Taifa. Kuongoza ni kuonesha njia ya kujenga, kiongozi lazima awe mfano wa kuigwa katika jamii.

 

“Ahadi 10 za TANU zililenga kutukomboa kifikra, lakini Azimio la Arusha lilikuwa kutukomboa kiuchumi. Misingi aliyoiweka Mwalimu kwa ajili ya ukombozi wa kiuchumi ni pamoja na kuwa na watu walio sawa, kwa maana kwamba hakuna matabaka ya watwana na mabwana, wala mapato yetu yasitofautiane sana.

 

“Mwalimu alitaka tujitegemee, tujenge watu huru wanaojitegemea, wasio tegemezi. Ukiwa ombaomba utajenga mradi wa anayekusaidia, huwezi kutengeneza mradi wako. Ili tusiwe ombaomba lazima tutawale uchumi wa nchi, rasilimali za nchi zitumike kwa manufaa ya Taifa, siyo kwa faida ya mtu mmoja.

 

“Kwa hiyo, kasumba ya kukataa kujiuzulu kutokana na matatizo ya uzembe ndiko kunatuharibia nchi,” anasema Kaduma na kuendelea:

 

“Jambo baya linapotokea katika eneo fulani, ili kuokoa heshima ya Serikali na nchi, kiongozi husika anapaswa kujiuzulu- awekwe mtu mwingine- bila kujali hajakosa, lakini kwamba kwanini limetokea na yeye yupo. Kwamba lazima yeye alizembea mahali na kwa uzembe huo lazima alipe kwa kujiuzulu.

 

“Kwa mfano, wafungwa waliotoroka Ukonga mwaka 1983, makamishna walijiuzulu siyo kwamba wametenda kosa, lakini kwamba lilitokea mikononi mwao. Natepe (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alijiuzulu. Kina Kisumo… nani awajibike sasa, awajibike rais? Hapana. Unawajibika uliyepewa dhamana ya kuangalia mahali pale.

 

“Mwinyi (Ali Hassan, Rais Mstaafu) aliwajibika kwa kujiuzulu mpaka akaja kuwa rais. Unapojiuzulu unaonesha uzalendo wako, kwamba nchi isiharibike kwa sababu yako.”

CCM kupoteza mwelekeo

Kaduma anasema misingi ya CCM ambayo ilitokana na vyama vya TANU na ASP imeachwa.

 

“Sasa hivi misingi ya CCM imeachwa. Wakati fulani nilipoona Serikali ya Awamu ya Tatu imeanza ubabaishaji niliacha… mpaka juzi hapa waliposema wameanza kujivua magamba, nikahamasika nikalipia mpaka mwaka huu (2012). Lakini sitegemei kulipia tena.

 

“Kwa kweli sitegemei kulipia tena mpaka nione viongozi wanaotaka kurudisha misingi ya Nyerere, lakini hivi hivi haina maana. Niko radhi nichange Sh 10,000 kwa ajili ya mbio za Mwenge kuliko kuchangia CCM Sh 1,200 kwa sababu imeondoka kwenye misingi yake,” anasema.

Alilia Nyerere mwingine

Kaduma anasema nchi imepoteza mwelekeo na misingi iliyowekwa na Mwalimu Nyerere. Kwa sababu hiyo, anatoa mapendekezo yake.

 

“Kwa hali ilivyo sasa nchi yetu inahitaji atokee Nyerere mwingine atakayesema hapa tumekosea na lazima tusahihishe. Lazima tuseme tumevuruga na tumejiharibia kiasi cha kutosha na sasa tunataka mapinduzi turudishe nchi kwenye mstari wake,” anasema na kuongeza:

 

“Kama likitokea kundi au chama kitakachotekeleza kwa ukamilifu misingi iliyowekwa na Mwalimu, basi chama hicho kitatawala nchi hii forever (milele) kwa sababu ilikuwa misingi ya utu.

 

“Itikadi ya Nyerere ilikuwa kuwainua wanyonge wafanane na waliyo juu… Natafuta chama kitakachokuwa na itikadi ya aina hiyo. Kwa sasa hivi hakuna chama chenye itikadi hiyo, itikadi ya vyama vyote sasa hivi ni kushika dola, basi. Wataifanyia nini hiyo dola? Hakuna.

 

“Nyerere alitaka kushika dola ainue maisha ya wanyonge waende mbele, na hapo ndipo ninawambia someni Zaburi 1:41-42, inasema, ‘Heri amkumbukaye mnyonge maana Bwana atamwokoa siku ya tabu, Bwana atamlinda na kumhifadhi, naye atafanikiwa…’

 

“Inua mnyonge aje juu ya mwamba. Hiyo ndiyo itikadi tuliyoitafuta. Tukifanya hivyo tutakuwa tunamuenzi Nyerere. Waumini wa kweli wa Nyerere waungane warudishe misingi yake, vinginevyo hakuna amani.

 

“Kwa hiyo, mimi ninachomkumbuka Mwalimu ni hicho, na kwamba angalau angekuwepo angekuwa anakemea maovu kila wakati. Itikadi kubwa ya Mwalimu ilikuwa kuwainua wanyonge waondokane na shida zao. Sasa hivi hakuna kiongozi mwenye itikadi hiyo, hata wapinzani hawana itikadi hiyo, wana itikadi ya kutaka madaraka tu,” anasisitiza Kaduma.

Katiba mpya

Kaduma anapendekeza Katiba mpya iundwe kwa Watanzania kubainisha maadili na misingi ya Taifa letu, utekelezaji wake na adhabu kwa atakayekiuka.

 

“Katika hili vyama vya siasa vitofautiane katika kuitekeleza misingi hiyo, lakini haiwezekani vitofautiane juu ya masilahi ya Taifa. Kipimo cha sheria nzuri ni uhuru wa kujitegemea, usawa, kumiliki uchumi na kuwa na viongozi waadilifu na waaminifu kama Mwalimu Nyerere,” anasema.

Mwito kwa Watanzania

“Nchi hii ni yetu sote, hakuna mwenye haki ya nchi hii kuliko Watanzania wote, lazima viongozi wote wajue wapo kwa niaba yetu sote. Wasimamie misingi ya kujenga Taifa letu. Bila hivyo, siku moja tutagombana, naomba Mungu isiwe hivyo wakati wa uhai wangu.

 

“Mwalimu aliongoza nchi hii kwa niaba yetu. Tunaomba viongozi waongeze nchi hii kwa niaba yetu, kwa faida yetu, siyo kwa faida yao binafsi, wala kwa faida ya wageni. Suala kubwa tutetee Taifa letu. Ukitenda haki unamtukuza Mungu. Ukisimamia misingi ya Nyerere you never go wrong (hautakosea).

 

“Vyombo vya habari ni watu huru kabisa, msiegemee upande wowote, ninyi mnatakiwa muegemee kwenye masilahi ya Taifa. Ukuta wenu ni masilahi ya Taifa. Kwa hiyo, viongozi wanaokwenda kinyume cha misingi inayotetea masilahi ya Taifa, lazima wazungumzwe na kukemewa,” anasema Kaduma.


Kinachomkera Kaduma

“Jambo linalonikera zaidi katika nchi hii bwana ni ubinafsi. Ubinafsi tu ndiyo shida yangu. Ninakerwa mno na ubinafsi,” anasisitiza. Anasema kwa hulka yake hataki kuonewa. Anarejea msimamo huo wakati akiwa shuleni Njombe ambako aliongoza mgomo kupinga wanafunzi kuonewa.

 

“Kwa hulka yangu sipendi kuonewa. Mimi kwanza si mwanasiasa, ninashindwa siasa kwa sababu wanasiasa wengi waongo, mimi sipendi uongo,” anasema.


By Jamhuri