Kwa muda sasa nimefuatilia kinachoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nimefuatilia kwa karibu kitu kinachoitwa mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia chama hicho kikongwe. Bila kuuma maneno, nasema mchakato umejaa mizengwe. Bila kupepesa macho nasema inawezekana Rais Jakaya Kikwete ana mgombea wake kwenye koti.


  Nimeyasikia maelezo ya Nape Nnauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, akiwajibu wanaohoji kulikoni mchakato unacheleweshwa kiasi hiki! Mmoja kati ya waliohoji kucheleweshwa kwa mchakato ni Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Balozi Khamis Kagasheki. Amehoji kupitia akaunti yake ya mtandao wa twitter.


  Nape ametoa majibu mepesi akidai Chama hakishinikizwi na mtu, na akaenda mbali zaidi kuhoji hata Kauli ya Katibu Mkuu wa CCM ambaye ndiye Mtendaji (accounting officer) na Msemaji Mkuu wa Chama kuwa hata hiyo kauli aliyoitoa kuwa mchakato unaweza ukawa Juni, mwaka huu, si kauli rasmi kwani haikutokana na vikao. Hakutueleza za kwake zimetokana na vikao vipi.


  Nimepata taarifa kuwa huenda leo na kesho Kamati Kuu ya CCM ikakutana kwa siku mbili mjini Dodoma kujadili uwezekano wa kuanzisha mchakato. Leo ni Aprili 28, 2015. Mnamo Machi 10, 2005, Philip Mangula akiwa Katibu Mkuu wa CCM, alimkabidhi Balozi Patrick Chokala fomu ya kugombea urais katika mchakato sawa na huu. Inawezekana Mangula amelisahau hili.


  Sitanii, mwaka 1995 na mwaka 2005 mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM ulianza Februari. Sina uhakika Nape katika miaka hiyo alikuwa na umri gani na alikuwa wapi, ila nayazungumza haya kwa kumbukumbu ya kushiriki kikamilifu nikiwa mwalimu wa shule za sekondari mwaka 1995, na baada ya mwaka mmoja kama mwandishi wa habari hadi leo ninavyoandika makala hii.


  Ni wazi kwa kauli ya Nape kuwa chama hakijawahi kuchelewa au kuwahi, anarejea uteuzi wa mgombea wa CCM mwaka 2010. Mkutano Mkuu wa CCM Juni 21, 2010 uliruhusu uchukuaji fomu na mwisho wa kurejesha fomu hizo ukaagiza iwe Julai 1, 2010 saa 10:00 jioni. Mwanachama wa CCM pekee aliyejitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni Ndugu Kikwete.


  Kanuni za Uteuzi wa Wagombea wa CCM katika vyombo vya dola, toleo la Februari 2010, Kanuni ya 17 fasili ya (viii) (1), inamtaka mgombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kudhaminiwa na jumla ya wanachama wa CCM wasiopungua 250 kila mkoa katika mikoa isiyopungua 10 ya Tanzania, mikoa minane ikiwa ni ya Bara na miwili ya Zanzibar.


Sitanii, hapa ndipo Nape na wenzake wanapoona bora watumie uzoefu wa mwaka 2010 kuendesha mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2015.
 Wanachosahau wakubwa hawa ni kuwa kwanza mgombea wa CCM aliyejitokeza mwaka huo alikuwa mgombea pekee, na kwamba mgombea huyo alikuwa Rais aliyeko madarakani na Mwenyekiti wa Chama.


  Pamoja na mteremko huo, mbio za kutafuta fomu ‘ligwaride’ lilimshinda akaishia kumpatia fomu mtoto wake, ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Chalinze (CCM) ili azizungushe katika mikoa kadhaa. Wapo waliohoji uhalali wa yeye kumtuma mtoto, akajibu na kusema “Urais ni jambo binafsi hivyo kumtuma mwanae hakufanya kosa.”


  Sisemi yupo atakayeshindwa kukimbia nchi nzima na kupata wadhamini 2,500 ikiwa muda utafupishwa, lakini naanza kupata wasiwasi kuwa huenda kuna mpango wa kuvunja Katiba ya CCM ikiwa vikao vyote vitalazimika kukaa. Huenda CCM wataamua kutoa majina kwenye Kamati Kuu na kuyapeleka kwenye Mkutano Mkuu bila kupitia Halmashauri Kuu kwa lengo la kupunguza muda.


  Napata taabu kweli kuona CCM sasa inaendeshwa kwa matamko badala ya Katiba, kanuni na ratiba ya wazi. Najiuliza, usiri huu unalenga nini ndani ya CCM? Najiuliza je, usiri huu unatokana na ushauri ambao pengine Kikwete kama Mwenyekiti amepewa na Makamu wake, Mangula? Je, Kikwete ni wa kumwamini Mangula asilimia 100?


  Mangula hana historia nzuri katika siasa tukichukulia tukio la hivi karibuni tu aliposhindwa na mtu asiye na historia ya msingi ndani ya CCM alipotaka kugombea Ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) kupitia Mkoa wa Iringa, unapata taabu kumwamini. Unamwaminije mtu aliyekuwa Katibu Mkuu akiongoza mikoa yote, kisha akaenda kushindwa na Deo Sanga, aliyekuwa ameandikishwa kwa kalamu ya risasi!
  Nikumbushe tu kuwa katika mchakato wa mwaka 1995 ulioanza Februari, walijitokeza wafuatao kuomba chama kiwateue kuwania kiti cha urais: Joseph Warioba, Mark Bomani, Cleopa Msuya, John Malecela, Edward Lowassa, Jakaya Kikwete, Kighoma Ali Malima, Horace Kolimba, Rose Lugendo, Pius Msekwa, Tuntemeke Sanga, Njelu Kasaka, Fred Rutakyamirwa na Benjamin Mkapa.


  Kabla ya uteuzi, Mwalimu Julius Nyerere ‘aliwaengua’ Kolimba na Malecela kwa madai walishindwa kumshauri vyema Rais Ali Hassan Mwinyi. Aliwatungia kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania. Ukikisoma kitabu hiki utaona anamsema wazi Malecela kuwa hafai kuwa kiongozi. Alikwenda mbali ndani ya kitabu hiki na kumwelekeza Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa alistahili kumfuta kazi Malecela.
  Sitanii, Kikwete angekuwa wa mwisho kuanzisha mizengwe katika uchaguzi. Angekuwa muumini wa uwazi katika michakato ya kupata mgombea. Nakumbuka siku chache kabla ya Mkutano Mkuu wa CCM mwaka 1995, Kikwete aliitisha mkutano na waandishi wa habari akamlalamikia aliyekuwa Katibu Mkuu, Lawrence Gama, kwa upendeleo.


  Nyota ya Kikwete iliishaonekana kung’ara. Baada ya kumlalamikia Gama, upinzani ukaanza kupiga jaramba. Ukamwinda kila kona. Zikapigwa kura awamu ya kwanza baada ya mchakato uliowaacha watatu kwenye kinyang’anyiro. Kikwete aliongoza kwa kura 534 akifuatiwa na Mkapa aliyepata kura 459 huku Msuya akipata kura 336. Kwa kuwa kanuni inataka mshindi apate zaidi ya asilimia 50 yaani asilimia 50+, Kikwete hakuwa mshindi. Katika kura za marudio, Mkapa alipata kura 686 na Kikwete kura 639. Kura 50 tu zikawatenganisha.
  Nimepata kuzungumza na watu kadhaa walioshiriki mchakato huu na Kikwete akiwamo. Ukiwauliza kuwa hakukutokea uchakachuaji, linabaki kuwa “fumbo la imani”. Msiba ulikuwa mkubwa kwa wafuasi wa Kikwete, mara kauli kwamba bado ni kijana asubiri kidogo ikapenyezwa. Upepo ukapungua vifuani mwa wafuasi kwa tumaini la miaka 10 baadaye.


  Wapinzani wakasubiri kauli ya Kikwete mwaka 1995. Mzee Augustine Lyatonga Mrema akawa anachanja mbuga. Wakatamani Kikwete aongeze petroli ila yeye akashikilia ‘ahadi ya ndani ya chama’. Chadema walisubiri kutokana na taarifa zisizo rasmi kuwa angehamia kwao hadi wakachelewa kusimamisha mgombea urais. Habari zikavuma Kolimba kutaka kuhamia upinzani baada ya kuikosoa CCM kuwa imekosa dira. Profesa Malima akahamia NRA, Sanga alitishia kuanzisha chama chake.
  Taarifa zinasema kuwa kuelekea mwaka 2005, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilifanya mazungumzo ya siri na Kikwete na inadaiwa angejiunga nao kama jina lake lingekatwa na vikao vya uteuzi. Hilo halikutokea kwani alikabidhiwa bendera ya CCM aipeperushe, baada ya kupenya katika msitu wa wagombea 11 ndani ya chama.


  Alioshindana nao Kikwete mwaka 2005 ni wale wa tano bora —  Kikwete mwenyewe, Dk. Salim Ahmed Salim, Profesa Mark Mwandosya, Frederick Sumaye na Dk. Abdallah Kigoda. Waliochujwa awali ni John Malecela, John Shibuda, Patrick Chokala, Ali Karume, Dk. William Shija na Iddi Simba. Ni katika hatua hii ninapotaka kumkumbusha Kikwete mambo mawili au matatu.


  Sitanii, jambo la kwanza ni maneno aliyoyatoa katika mkutano wa NEC kabla ya uteuzi kule Zanzibar. Aliwaambia wanamfitini kupita kiasi. Akaongeza kuwa kama Mungu amempangia mwanadamu jambo liwe litakuwa tu. Sina uhakika kama Mangula hakuwa mmoja wa waliokuwa wanamfitini. Kundi la Mangula linadaliwa kuwa karata yao ilikuwa kwa Abdallah Kigoda.
  La pili linaenda sambamba na la kwanza. Kama si Mkapa kupewa taarifa sahihi siku chache kabla ya uchaguzi; mawili, ama Kikwete angekuwa Rais kupitia upinzani au angekuwa analima mananasi Msoga kwa mpango ulivyokuwa umesukwa na wabaya wake. Sina uhakika kama Mangula hakuwa mmoja wao. Sisi tuliokuwa na taarifa za kina kisha tukawa ukumbini pale Chimwaga, hotuba ya Mkapa ilituacha vinywa wazi. Alimpigia debe la wazi Kikwete.


  La tatu, Mangula ndiye aliyekuwa anaongoza Sekretariati ya CCM. Kikwete kama Mwenyekiti anakumbuka kwa nini alinunua magari binafsi na kufungua ofisi ya kampeni pale Mtaa wa Mindu, maeneo ya Muhimbili. Si Mangula alikupa ushirikiano mzuri ehee? Si alikuchapia vipeperushi na kuratibu matangazo yako ehee? Si ndiye aliyeongoza mkakati wa kampeni mwanzo hadi mwisho ehee? Akili ya kuambiwa…


  Leo napata shida kweli. Hata kama Kikwete unaye mgombea wako kwenye koti kama alivyokuwa Mkapa na Kigoda, basi ungeruhusu utaratibu wa vikao ndani ya chama kufanya kazi. Kazi inayofanywa na baadhi ya watu wanaohusishwa na kaulimbiu ya BMW, inayeyusha uwepo wa chama. Kipimo cha 2010 kisitumike kuteua mgombea mwaka 2015.


  Nilikuwa Mhariri Mkuu wa Gazeti Tanzania Daima mwaka 2005. Najua fika mchakato ulivyokwenda ndani ya CCM na muda mlioutumia kukusanya saini za wadhamini. Atakayeteuliwa kupitia CCM atapaswa kutumia fursa ya kukusanya saini za wadhamini kujinadi japo kidogo. Mkifinyanga mchakato na kudhani mtawauzia mbuzi Watanzania kwenye gunia, hakika Rais Kikwete utaingia kwenye historia.


  Na wala historia si nyingine. Historia ni wewe kukabidhi nchi kwa wapinzani kama alivyofanya Rais Daniel arap Moi wa Kenya, alipowalazimisha Wakenya wamchague Uhuru Kenyatta mara ya kwanza mwaka 2007. Kubwa tunalokuomba; uliipokea Tanzania ikiwa na amani, naomba uturejeshee Tanzania yenye amani utakapomaliza muhula wako wa pili Oktoba. Mungu ibariki Tanzania.

4932 Total Views 2 Views Today
||||| 3 I Like It! |||||
Sambaza!